Ripoti ya kanisa kuhusu biashara ya silaha ya Ujerumani nchi za nje | Matukio ya Kisiasa | DW | 14.12.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Ripoti ya kanisa kuhusu biashara ya silaha ya Ujerumani nchi za nje

Makanisa ya Ujerumani yaikosoa serikali kuu kwa kutanguliza mbele masilahi ya kiuchumi

default

Msemaji wa shirika linalopigania amani nchini Ujerumani Jürgen Grässlin na kampeni ya kusitisha mbio za kutengeneza silaha

Ujerumani inashikilia nafasi ya tatu ya nchi zinazosafirisha silaha kwa wingi ulimwenguni,baada ya Marekani na Urusi.Mnamo mwaka 2008 serikali iliidhinisha biashara ya silaha iliyokua na thamani ya yuro bilioni nane,na katika mkataba wa muungano wa serikali mpya ya CDU/CSU na waliberali wa FDP,hakuna ishara kama biashara hiyo itapungua.

Makanisa mawili makuu ya humu nchini yamekosoa vikali hali ya kuzidi biashara ya silaha za Ujerumani nchi za nje. "Serikali mpya ya shirikisho inaelekea kutanguliza mbele masilahi ya kiuchumi badala ya amani au maendeleo" amesema askofu wa kanisa katoliki Karl Jüsten

"Anaetaka kuzuwia mbio za kujirundukia silaha katika eneo la mashariki ya kati,kusini na kusini mashariki ya Asia au Amerika ya kusini,hastahiki kupalilia hali hiyo kwa kufanya biashara ya silaha."

Ripoti ya biashara ya silaha kwa mwaka 2008, iliyochapishwa na makanisa ya Ujerumani,imeikosoa kwa mara nyengine tena serikali kuu ya Ujerumani kwa kutoa kibali cha biashara ya silaha.Kwa mtazamo wa siku za mbele ripoti hiyo imeonya zaidi dhidi ya kuzidi kupata nguvu biashara ya nyambizi za Ujerumani katika soko la asilaha ulimwenguni.

Mtaalam anaechunguza vyenzo vya mizozo Bernhard Moltmann amezungumzia umuhimu wa kuzuwia kusambaa biashara hiyo.Katika wakati ambapo jeshi la wanamaji la Ujerumani limeagizia nyambizi 36 hadi sasa,nyambizi zilizouzwa nchi za nje zimepindukia mara tatu kiwango hicho.Bernhard Moltmann anasema:

"Katika kipindi cha hivi karibuni,nyambizi zinatazamiwa au zimeshaagiziwa kutoka Ugiriki,Uturuki,Ureno,Pakistan,Afrika Kusini,Israel,Italy na Korea ya kusini.Na kiwanda cha HDW mjini Kiel kimeshatangaza wiki iliyopita hawana nafasi kabla ya mwisho ya mwaka 2017.Kwa hivyo biashara inaendelea."

Ingawa biashara ya silaha haifikii asili mia moja ya biashara ya nje ya Ujerumani,lakini serikali mpya ya muungano wa nyeusi na manjano,kwa mujibu wa mkataba wa muungano,inataka kuondowa vizingiti ili kuyawezesha makampuni yanayotengeneza silaha yaweze kushindana katika daraja ya kimataifa na kurahisisha biashara ya bidhaa hiyo kwa matumizi tangu ya kiraia mpaka ya kijeshi.

Mnamo mwaka uliopita Ujerumani ilisafirisha silaha zake zaidi katika nchi za Ulaya,Uturuki,Afrika Kusini,Korea ya kusini na Australia..Hata hivyo ripoti ya makanisa imesifu ile hali kwamba biashara ya silaha za Ujerumani kwa nchi zinazoinukia imepungua mnamo mwaka 2008.Kwa mara nyengine tena makanisa yanataka bunge lishirikishwe zaidi katika kupitisha maamuzi kuhusu biashara ya silaha.Ripoti ya kanisa imekosoa ile hali kwamba bado serikali haijachapisha ripoti yake kuhusu biashara ya silaha kwa mwaka 2008.

Mwandishi:Gräßler,Bernd/ZR/ Hamidou Oummilkheir

Mhariri:Abdul-Rahman

 • Tarehe 14.12.2009
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/L1yq
 • Tarehe 14.12.2009
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/L1yq
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com