Rais wa Zimbabwe na wa Iran washutumiwa kwa kuhudhuria kikao cha FAO mjini Rome | Matukio ya Kisiasa | DW | 02.06.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Rais wa Zimbabwe na wa Iran washutumiwa kwa kuhudhuria kikao cha FAO mjini Rome

Kikao kuhusu chakula na kilimo kinafanyika mjini Roma Italy huku nchi za magharibi zikizua shutuma kali dhidi ya Mugabe anaedaiwa kusababisha upungufu wa chakula nchini mwake

Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe akiwasili katika kikao cha Umoja wa Ulaya na Afrika nchini Ureno mwaka uliopita

Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe akiwasili katika kikao cha Umoja wa Ulaya na Afrika nchini Ureno mwaka uliopita

Kikao cha kimataifa kuhusu chakula na kilimo lichoandaliwa mjini Rome Italy kinaanza leo huku Uingereza ikishutumu hatua ya Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe ya kuhudhuria kwa madai kwamba amesababisha tatizo la chakula nchini mwake.


Wakati huo huo mwanasiasa mmoja wa mrengo wa kushoto nchini Italy amepanga mgomo wa kushinikiza kuondolewa kwa Mugabe na Rais wa Iran Mahamud Ahmedinejad ambaye anarajiwa kufanya ziara yake ya kwanza magharibi mwa ulaya kama Rais wa Iran.


Mugabe aliwasili mjini Roma jumapili usiku tayari kwa kikao cha leo kitakachochukua tatu na ambacho kinahudhuriwa na viongozi 60 wa mataifa mbali mbali ulimwenguni.


Ziara yale mjini Roma ni ya kwanza katika nchi za ngambo tangu kufanyika kwa uchaguzi nchini humo ambao nchi za magharibi na upinzani zinasema ulikumbwa na udanganyifu.


Anatarajiwa kuhudhuria kikao hicho kitakachojadili kuongezeka kwa bei ya chakula na jinsi hali hiyo inavyoathiri maskini.


Msemaji wa waziri wa nchi za kigeni wa Uingereza Gordon Brown amesema anasikitishwa na hatua aliyochukua Mugabe ya kuhudhuria kikao hicho haswa ikizingatiwa jinsi alivyosababisha kuzorota kwa kilimo na uhaba wa chakula nchini mwake.


Msemaji wa Brown amesema hakuna mpango wowote wa Rais huyo kukutana na mjumbe anaewakilisha Uingereza katika kikao hicho ambaye ni katibu wa maendeleo ya kimataifa Douglas Alexander.


Mugabe ambaye anatarajiwa kushiriki katika marejeleo ya uchaguzi wa Urais dhidi ya kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai ameandamana na mkewe pamoja na ujumbe mkubwa wa maafisa wa serikali.


Umoja wa Ulaya umemuwekea vikwazo vya usafiri Rais huyo ambaye anashutumiwa na upinzani kwa kutumia ghasia kushinda uchaguzi.


Hata hivyo Mugabe anaruhusiwa kuhudhuriwa kikao hicho ambacho kiko chini ya mwavuli wa Umoja wa Mataifa.


Mwaka wa 2005 Mugabe alihudhuria maadhimisho ya miaka 60 ya shirika la chakula na kilimo duniani FAO na akawashutumu Rais wa Marekani George W Bush pamoja na aliyekuwa waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair akiwaita magaidi wa kimataifa.


Mugabe ameitawala Zimbabwe tangu iliponyakuwa uhuru kutoka kwa Uingereza mwaka wa 1980. Tume ya uchaguzi nchini humo imeonyesha Kiongozi wa upinzani Tsvangirai akiongoza kwa wingi wa kura katika awamu ya kwanza ya uchaguzi lakini ushindi wake haukuzidi asilimia 50 inayohitajika kwa kiongozi kushinda Urais.


Uchumi wa Zimbabwe umo matatani kwani mfumuko wa bei umefikia asilimia laki moja na sitini na tano elfu. Upungufu wa kazi nao umefikia asilimia 80 na nchi hiyo imekuwa ikikumbwa na upungufu wa bidhaa muhimu kama chakula na mafuta.


Takriban watu milioni 3.5 wamekimbilia nchi jirani.


Mugabe mwenye miaka 84 anazilaumu nchi za magharibi kwa kupelekea kuzorota kwa uchumi wa nchi yake kwa madai ya kumuekewa yeye na viongozi wengine wachache wa serikali yake vikwazo.


Ziara yake ya mwisho ulaya ilikuwa mwezi disemba mwaka uliopita wakati alipohudhuria kikao cha Umoja wa Ulaya na Afrika nchini Ureno. Kuhudhuria kwake kulimfanya waziri mkuu wa Uingereza asusie kikao hicho.


Kwa upande mwengine Rais wa Iran Mahmoud Ahmadinejad amethibitisha kwamba atahudhuria kikao cha Roma.


Rais huyo alipanga kukutana na papa mtakatifu Benedict wa 16 lakini mkutano huo ukakatazwa na Vatican.


Vile vile Rais huyo hatarajiwi kukutana na waziri mkuu wa Italy Silvio Berlusconi lakini atakutana na wafanyibiashara nchini humo wenye tama ya kufanya biashara na nchi yake ya kiislamu.

 • Tarehe 02.06.2008
 • Mwandishi Mwakideu, Alex
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EBQn
 • Tarehe 02.06.2008
 • Mwandishi Mwakideu, Alex
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EBQn
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com