1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelensky asema yuko tayari kuzungumza na Rais wa Urusi.

Zainab Aziz Mhariri: Mohammed Khelef
13 Mei 2022

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amesema yuko tayari kufanya mazungumzo na Rais wa Urusi. Zelenskiy ametoa tamko hilo baada ya kusema kuwa nchi yake haitalitambua jimbo la Crimea kuwa ni sehemu ya Urusi.

https://p.dw.com/p/4BH7r
Ukraine | Präsident Selenskyj
Picha: John Moore/Getty Images

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amesema yuko tayari kufanya mazungumzo na Rais Putin peke yake bila ya wapambe wake na katika msingi wa mdahalo na siyo wa kutoleana masharti. Rais wa Ukraine katika matamko yake ya hivi karibuni ameeleza kuwa nchi yake haiko tayari kuachia sehemu yoyote ya ardhi yake na ameitaka Urusi iondoke kwenye sehemu inazokalia tangu ilipoanza uvamizi mwezi Februari, amesema huo ndio msingi madhubuti wa kuweza kuzungumzia juu ya kila kitu.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky
Rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskyPicha: Präsidentschaft der Ukraine/ZUMA/dpa/picture alliance

Urusi na Ukraine mpaka sasa hazijafanya mazungumzo ya ana kwa ana tangu tarehe 29 mwezi Machi. Kiongozi wa ujumbbe wa Urusi kwenye mazungumzo Vladimir Medinsky amekaririwa na shirikka la habari la Interfax akisema kuwa mazungumzo yanafanyika lakini siyo ana kwa ana.

Soma:Vikosi vya Ukraine vyauzuwia msafara wa Urusi kuvuka mto

Wakati huo huo kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na rais wa Urusi Vladimir Putin leo wamejadili hali ya nchini Ukraine kwa njia ya simu. Mazungumzo kati ya viongozi hao wawili yamefanyika baada kuwepo na ukimya wa zaidi ya wiki sita.

Mapema leo kansela Olaf Scholz aliwafahamisha wabunge wa Ujerumani kuhusu azma yake ya kumpigia simu rais wa Urusi hayo ni kwa mujibu wa washiriki katika kikao cha kamati ya ulinzi katika bunge la Ujerumani huko mjini Berlin. Msemaji wa serikali ya Ujerumani Steffen Hebestreit amesema lengo la mazungumzo hayo lilikuwa ni kutafuta njia za kuvimaliza vita kati ya Urusi na Ukraine ambavyo vimesababisha  maangamizi makubwa.

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz
Kansela wa Ujerumani Olaf ScholzPicha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Ikulu ya Urusi nayo imeeleza kuwa rais Putin ametoa habari za kina kuhusu malengo ya Urusi nchini Ukraine, yakiwemo maswala ya kibinadamu. Viongozi hao wamekubaliana kuwa majadiliano yataendelea kupitia njia mbalimbali.

Wakati huo huo wizara ya mambo ya nje ya Urusi leo imewatahadharisha raia wa Urusi dhdi ya kuanya safari nchini Uingereza kutokana na msimamo wa Uingereza ambao umetajwa kuwa usio wa kirafiki pamoja na kucheleweshwa mno kwa maombi ya warusi wanotaka visa kuingia nchini humo. Wizara ya mambo ya nje ya Urusi imesema itawafanyia hivyo hivyo raia wa Uingereza wanaotaka kwenda Urusi hadi hali itakapokuwa nzuri.

Rais wa Urusi Vladimir Putin
Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: Kremlin Press Service/Handout/AA/picture alliance

Angalia:

Ulaya kuipatia Ukraine msaada wa euro milioni mia tano

Na nchi za Umoja wa Ulaya zimeahidi msaada wa kijeshi wa dola nusu bilioni kwa Ukraine leo hii wakati ambapo Sweden na Finland zinakaribia kujiunga na jumuiya ya NATO huku vita vya Ukraine vikiwa vimeingia katika wiki ya 12. Katika mkutano wa nchi zenye nguvu zaidi duniani, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell ameiahidi Ukraine nyongeza ya euro milioni 500 sawa na dola milioni 520, na kufanya jumla ya msaada wa kijeshi wa umoja huo kufikia euro bilioni mbili.

Vyanzo: RTRE7DPA/AFP