Rais wa Afghanistan Karzai ataka kujadiliana na Taliban | Matukio ya Kisiasa | DW | 18.11.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Rais wa Afghanistan Karzai ataka kujadiliana na Taliban

Ikulu ya Marekani imesema kuwa hakuna ishara yoyote kutoka kwa kiongozi wa Taliban anayetafutwa Mullah Mohammed Omar baada ya kutolewa pendekezo la mapatano lililotolewa na rais Karzai.

Ikulu ya Marekani imesema kuwa hakuna ishara yoyote kutoka kwa kiongozi wa Taliban anayetafutwa Mullah Mohammed Omar ama wapiganaji wake baada ya kutolewa pendekezo la mapatano lililotolewa na rais Hamid Karzai wa Afghanistan.

Hakuna ishara kuwa Mullah Omar yuko tayari kukana matumizi ya nguvu, na kuvunja mahusiano yote na kundi la al-Qaeda na kuunga mkono serikali na katiba ya Afghanistan.Msemaji wa Ikulu ya Marekani Gordon Johndroe amesema kuwa hakuna mtu aliyemuona Mullah Omar kwa muda sasa, na kutokana na mashambulio kama yaliyotokea wiki iliyopita wakati baadhi ya wataliban walipowamwagia tindikali wasichana wanaokwenda shule, wengi hawaonyeshi nia ya kutaka kujadiliana.

Wakati tunamatumaini kuwa Wataliban wanaokubali maridhiano wataweka silaha zao chini na kuchukua njia kutoa mchango wa maendeleo katika jamii ya Waafghanistan , kwa bahati mbaya bado wanaendelea na mashambulio yao dhidi ya raia wasio na hatia pamoja na majeshi ya muungano kila uchao amesema Johndroe.

Matamshi ya Johndroe yanakuja baada ya Karzai kusema wiki hii kuwa atakwenda umbali wa kumlinda Mullah Omar iwapo kiongozi huyo wa Taliban atakubaliana kuhudhuria mazungumzo ya amani.

Rais wa Afghanistan amekuwa kwa miaka kadha akisukumwa kufanya mazungumzo na Taliban kama njia ya kujitoa katika mapambano makali ya wapiganaji ambapo wapiganaji kutoka mataifa ya nje , ikiwa ni pamoja na wale wa al-Qaeda, wanasemekana wanashiriki.

Hata hivyo amekuwa akisisitiza kila mara kuwa serikali yake itafikiria kuwa na mazungumzo na Wataliban wa Afghanistan ambao hawana mahusiano na al-Qaeda na watakaokubali kuweka silaha zao chini na kukubali katiba ya baada ya utawala wa Taliban.

Mwenyekiti wa jopo la wakuu wa majeshi ya Marekani admirali Michael Mullen , wakati huo huo amesema kuwa kufanya mazungumzo na baadhi ya watu wa kundi la Taliban iwe sehemu ya mkakati wa muda mrefu lakini si wakati muafaka wa kuchukua hatua kama hiyo.

Katika wakati fulani , tutaweza kuingia katika hali ya kuweza kuwatenga wapiganaji ambao wanataka mapatano na nafikiri unaanza mazungumzo na wale ambao wanataka mapatano amesema Mullen.

Kwa mtazamo wangu amesema Mullen, bado hatujafika hapo. Mullen amesema utaratibu kama huo ulitumika kwa mafanikio nchini Iraq pamoja na mapambano dhidi ya wapiganaji kwingineko, akiongeza kuwa ni jambo linaloeleweka kama utatafuta mazungumzo na wapiganaji nchini Afghanistan.

Wakati huo huo msemaji wa Taliban amesema kuwa wapiganaji wamekataa ombi la rais wa Afghanistan Hamid Karzai la kuwa na mazungumzo ya amani hadi pale majeshi yote ya kigeni yatakapoondoka nchini humo.

Zabiullah Mujahid ambaye ni msemaji wa Taliban , ameliambia shirika la habari la Associated Press kuwa hakuna mazungumzo yatakayofanyika wakati majeshi ya kigeni yako nchini humo.

Karzai amekataa dai hilo , akisema kuwa majeshi ya kigeni ni muhimu kwa ajili ya usalama wa Afghanistan. Mujahid amesema kuwa Taliban wataendelea na mapigano dhidi ya majeshi ya kigeni pamoja na serikali ya Karzai.

►◄
 • Tarehe 18.11.2008
 • Mwandishi Samia Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/FxOc
 • Tarehe 18.11.2008
 • Mwandishi Samia Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/FxOc
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com