Rais Obama alihutubia bunge kwa mara ya kwanza.
25 Februari 2009WASHINGTON.
Rais Barack Obama amesema utawala wake unaanzisha enzi mpya ya kidiplomasia ya kujizatiti katika kuleta amani Mashariki ya Kati ,sambamba na kuendeleza harakati za kupambana na ugaidi.
Rais Obama amesema hayo leo katika hotuba yake muhimu ya kwanza bungeni, tokea aingie madarakani.
Rais huyo pia ameahidi kuimarisha mifungamano iliyopo na kuanzisha mipya duniani kote.
Katika hotuba yake Obama pia amesisitiza umuhimu wa mazungumzo ili kuondoa tofauti.
Juu ya mgogoro wa kiuchumi rais huyo wa 43 wa Marekani ameahidi kushirikiana na nchi zingine zenye nguvu kubwa za kiuchumi ili kuepusha uwezekano wa kuenea kwa sera za kujenga vizingiti vya kibiashara duniani.
Katika kufikia lengo hilo Marekani itakuwa pamoja na nchi za G 20 ili kurejesha imani katika mfumo wa fedha na kuhamasisha utashi wa bidhaa za Marekani kwenye masoko ya dunia.
DPAE.