Rais mpya wa Ujerumani aapishwa
2 Julai 2010Christian Wulff, mwenye umri wa miaka 51, ameapishwa kushika wadhifa wa urais nchini Ujerumani leo Ijumaa akiwa rais wa 10. Waziri mkuu huyo wa zamani wa jimbo la Lower Saxony , kutoka chama cha kansela wa Ujerumani Angela Merkel cha Christian Democratic Union, alichaguliwa kushika wadhifa huo siku ya Jumatano wiki hii, baada ya duru tatu za uchaguzi.
"Naapa kutumia uwezo wangu kuitumikia jamii ya Wajerumani, kuwaongezea neema na kuwaepusha na madhara. Nitailinda katiba na sheria za nchi hii, na kutekeleza majukumu yangu kwa kadiri ya uwezo wangu, na kumtendea haki kila mtu. Mungu nisaidie."
Hayo ni maneno ya kuapa aliyoyasema rais mpya wa Ujerumani Christian Wulff mjini Berlin leo katika kikao cha pamoja cha mabaraza ya bunge la wawakilishi wa majimbo, Bundesrat na lile la shirikisho la Bundestag.
Rais huyo mpya wa Ujerumani Christian Wulff aliapishwa leo Ijumaa baada ya uchaguzi mapema wiki hii uliogeuka kuwa pigo kwa kansela wa Ujerumani Angela Merkel.
Kwa mara nyingine tena kumekuwa na uchaguzi wa kweli kwa wadhifa wa rais wa shirikisho la Ujerumani, amesema Wulff kutoka chama cha kihafidhina cha Christian Democratic.
Kila unapofanyika uchaguzi wa haki ni kitu kizuri kwa ajili ya demokrasia yetu.
Rais huyo mpya Christian Wulff anapendelea kuona ukuaji wa pamoja wa sekta mbali mbali za jamii ya Ujerumani. Nguvu kubwa ya Ujerumani ni watu wake, amesema Wulff.
Anataka kuimarisha mshikamano baina ya vijana na wazee, baina ya watu kutoka mashariki na magharibi ya Ujerumani, wahamiaji na watu wenye asili ya Ujerumani, waajiri na waajiriwa pamoja na wale ambao hawana ajira, watu wenye ulemavu na wasio walemavu.
Wulff amedai kuwa unahitajika mshikamano zaidi badala ya mtengano. Kwa hiyo kutapatikana kitu kipya kizuri kutokana na utamaduni wa nidhani ya Kijerumani ukichanganywa na uwezo wa kupenya penya wa Kituruki kwa mfano, urithi wa utamaduni wa Kiprasha wa nidhamu ya uwajibikaji na mchanganyiko wa utamaduni wa Kiingereza na Kijerumani, usiohitaji hali ya kuharakishwa, msingi wa maisha ya watu wa eneo la kati la Ujerumani, pamoja na aina ya maisha ya Kitaliani.
Kwa upande wa vyama ametoa wito kupambana na hali ya mivutano ya kisiasa.
Na pia raia ambao hawajishughulishi na vyama, wanapaswa kupewa kwa wepesi uzoefu, wawapo katika kazi zinazohusu vyama.
Waziri mkuu huyo wa zamani wa jimbo la Lower Saxony alichaguliwa katika wadhifa huo baada ya mtangulizi wake Horst Koehler kutangaza kujiuzulu ghafla mwezi mmoja uliopita.
Spika wa bunge la Ujerumani Norbert Lammer alimsifu rais wa zamani Koehler na kusema kuwa aliyachukulia matatizo ya watu na mahitaji yao kwa dhati, na wanampa shukrani kwa mapenzi ambayo hayatakwisha.
Mwandishi: Sekione Kitojo / DPAE / RTRE
Mhariri : Josephat Charo