Medvedev asema juhudi zitaendelea Mashariki ya Kati.
23 Juni 2009
Rais Dmitry Medvedev wa Urusi
amesema mchakato wa kufufua juhudi
za kuleta amani ni mgumu katika
Mashariki ya Kati lakini ameahidi kuwa
nchi yake itaendelea na juhudi hizo hadi
mafanikio yapatikane.
Rais Medvedev amesema hayo leo mjini Cairo baada ya mazungumzo yake na rais Hosni Mubarak wa Misri.
Misri ni kituo cha kwanza katika ziara yake barani Afrika.
Rais Medvedev aliwaambia waandishi habari baada ya mazungumzo yake na mwenyeji wake rais Hosni Mubarak wa Misri kwamba suala la Mashariki ya Kati ni gumu sana lakini amesema licha ya hayo Urusi ipo tayari kuendelea na juhudi za ,kutafuta ufumbuzi.
Kwa upande wake rais Hosni Mubarak amesisitiza umuhimu wa Urusi katika juhudi hizo lakini amesema kuwa ufumbuzi hautapatikana kutokana na juhudi za nchi moja tu.
Urusi na Misri zimetiliana saini makubaliano ya ushirikiano wa muda mrefu.
Rais Medvedev na mwenyeji wake rais Hosni Mubarak wa Misri pia wamejadili njia za kuimarisha uhusiano katika baina ya nchi zao katika sekta za uchumi na biashara.
Kwa mara ya mwisho ziara ya rais wa Urusi barani Afrika ilifanyika miaka mitatu iliyopita.
Rais Medvedev anafanya ziara barani Afrika muda mfupi baada ya rais Barack Obama wa Marekani kutoa hotua yake ya kihistoria mjini Cairo hivi karibuni, ambapo alijaribu kuweka msingi wa uhusiano mpya na nchi za kiislamu.
Baada ya ziara ya nchini Misri rais Dmitry Medvedev pia atazitembelea Nigeria, Namibia na Angola kuanzia kesho.
Mwandishi:A.Mtullya/AFPE
Mhariri:AbdulRahman