1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Rais Köhler anaijali Afrika"

Maja Dreyer15 Januari 2007

Sera mpya za Iraq za Rais Bush wa Marekani, kuchaguliwa kwa waziri Sarkozy wa Ufaransa kuwa mgombea wa urais wa chama cha kihafidhina pamoja na ziara ya rais Köhler wa Ujerumani nchini Ghana – haya ndiyo masuala ya kimataifa yanayozingatiwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.

https://p.dw.com/p/CHTy

Tunaanza na gazeti la “Frankfurter Allgemeine Zeitung” na maoni yake juu ya sera mpya za Iraq za Rais wa Marekani. Gazeti limeandika:
“Sehemu moja ya sera hizo mpya za rais Bush ni kuchukua msimamo mkali zaidi dhidi ya Syria na Iran. Iran tayari iliweza kuona sera hizo. Sababu za kuwakamata Wairan nchini Iraq siyo tu kwamba Wairan hao wanasemekana waliwasaidia wanamgambo wa Iraq. Bali lengo lingine la hatua hiyo ni kuwaonyesha Wairani athari za kujiingiza katika vita vya Iraq. Kutokana na Iran kuwa kaidi sana katika mzozo juu ya mradi wake wa kinyuklia, nchi jirani za Kiarabu zitakubali sera za Rais Bush. Wakati huo huo Bush anamuonyesha Rais Assad wa Syria chombo cha kumtia shindo.” - ni gazeti la “Frankfurter Allgemeine Zeitung”.

Nchini Ufaransa, chama cha kihafidhina UMP, baada ya mivutano mingi, kilimchagua waziri wa ndani, Sarkozy, kuwa ni mgombea wake wa urais. Gazeti la “Badisches Tagesblatt” linachambua hivi siasa za Ufaransa:
“Muhimu kuliko mvutano wa ndani ya chama ni ikiwa Sarkozy ataweza kuwashawishi Wafaransa kwamba almebadilisha sura yake ya siasa kali kuwa ni mwanasiasa anayeziwakilisha pande zote za jamii.”

Na gazeti la “Schwäbische Zeitung linakosoa jinsi wagombea wote wawili, Sarkozy na mgombea wa kisoshalisti, Ségolène Royal, wanavyoendesha kampeni za uchaguzi. Tunasoma:
“Siku ya uchaguzi inapokaribia, wagombea wote wawili wanajaribu kutuliza hali ya mambo. Wakiwa na hofu kuwashtusha wapigaji kura, wanazungumzia hali nzuri tu. Lakini hali halisi ni tofauti. Yule atakayeshinda uchaguzi huu atalazimika kuwaambia Wafaransa kwamba bila ya kufanya mageuzi makali, nchi yao itaporomoka chini. Kwa ajili hiyo lakini lazima waseme ukweli, yaani pia kabla ya uchaguzi kufanyika.”

Na tukimaliza udondozi huu wa magazeti sasa tunaelekea ziara ya rais Horst Köhler nchini Ghana iliyomalizika jana. Haya basi ni maoni ya mhariri wa gazeti la “Volksstimme” la mjini Magdeburg:
“Katika hotuba yake ya kuapishwa katika wadhifa wake, mwaka 2004, rais Köhler alisema hali ya ubinadamu duniani kote inategemea mustakabali wa bara la Afrika. Sera zake Köhler tangu kuingia madarakani zinaonyesha kuwa kweli Afrika inapewa umuhimu. Katika ziara yake ya kwanza, Köhler alitembelea bara la Afrika na sasa amekwenda tena. Kwa kweli, rais Köhler anaijali Afrika. Pia anaheshimika kutokana na ujuzi wake alioupata akiwa mkurugenzi wa shirika la fedha la kimataifa IMF.”