1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Bush ziarani Ulaya

Hamidou, Oumilkher10 Juni 2008

Rais George Bush anaanza kuwaaga viongozi wenzake wa Ulaya

https://p.dw.com/p/EH6Q
Rais wa Marekani George W. Bush,katika mkutano wa waandishi habari pamoja na m,wenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa ulaya Barroso (kushoto) na waziri mkuu wa Slovenia Janez Jansa (kati)Picha: Reuters


Rais George W. Bush wa Marekani anaendelea na ziara yake ya wiki moja katika nchi za Umoja wa ulaya.Hii leo anatazamiwa kuwasili  nchini Ujerumani kwa mazungumzo pamoja na kansela Angela Merkel.


Kabla ya hapo rais George W. Bush alikuwa ziarani mjini BRDO PRI KRANJU,nchini Slovenia alikohudhuria mkutano wa kilele kati ya Marekani na umoja wa Ulaya.Katika mkutano pamoja na waandishi habari,mwishoni mwa mazungumzo yake pamoja na mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya José Manuel Barroso na waziri mkuu wa Slovenia Janez Jansa,rais George W. Bush amesisitiza umuhimu wa kuzidi kushinikizwa Iran iachane na mradi wake wa kinuklea.Rais Bush ameitolea mwito jumuia ya kimataifa akisema


"Iran itahatarisha sana amani ya dunia pindi ikiachiwa imiliki silaha za kinuklea."


Rais Bush amependekeza ushirikiano wa dhati ili kuitanabahisha Iran ichague kati ya kujikuta ikitengwa kimataifa au kuwa na uhusiano mzuri pamoja na jumuia ya kimataifa ikiamua kusitisha mpango wa kurutubisha maadini ya uranium.


Hali nchini Zimbabwe,sawa na Myanmar na matumaini ya amani ya mashariki ya kati,ni miongoni mwa mada zilizojadiliwa pia katika mkutano huo wa kilele kati ya Umoja wa ulaya na Marekani.


Rais George w. Bush ametetea haja ya kukubaliwa Uturuki kua mwanachama wa Umoja wa Ulaya akisema:


"Tunaamini moja kwa moja kwamba Uturuki inabidi ijiunge na Umoja wa ulaya."


Kuhusu suala la mabadiliko ya hali ya hewa,Umoja wa Ulaya umeshauri kwa mara nyengine tena kuwa na ushirikiano wa dhati pamoja na Marekani.Mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Ulaya,waziri mkuu wa Slovenia Janez Jansa amesema mjini Brdo tunanukuu: "tatizo la mabadiliko ya hali ya hewa ni la ulimwengu mzima,hakuna anaeweza pekee kulipatia ufumbuzi."Mwisho wa kumnukuu.


Rais George W. Bush amesema anaamini makubaliano ya kupambana na kuzidi hali ya ujoto duniani yanaweza kufikiwa kabla ya mhula wake kumalizika january mwakani.


Rais George w. Bush ameshaondoka Brdo kuelekea Brandenburg karibu na Berlin ambako amepangiwa kua na mazungumzo pamoja na kansela Angela Merkel katika kasri la Meseberg.


Mada mazungumzoni mjini Brandenburg ni pamoja na mzozo wa mashariki ya kati,Iran na Afghanistan.Rais George W. Bush na mwenyeji wake kansela Angela  Merkel wanatazamiwa pia kuzungumzia mkutano wa kilele wa mataifa tajiri kiviwanda G-8 nchini Japan na mkutano ujao wa kimataifa kuhusu Mashariki ya kati mjini Berlin.


Hii ni ziara yake ya tano na ya mwisho tangu alipochaguliwa kua rais wa Marekani mnamo mwaka 2001.


Kwa mara ya mwisho rais George w. Bush alikua ziarani mwezi June mwaka jana alipohudhuria mkutano wa kila mwaka wa viongozi wa mataifa manane tajiri kiviwanda-G8 mjini Heiligendam.


Baada ya Ujerumani rais George W. Bush anapanga kufika ziarani nchini Uengereza,Italy,Vatikan na Ufaransa.








►◄