Rais Bush akiri kuwa uchumi wa Marekani uko taaban | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 25.09.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Rais Bush akiri kuwa uchumi wa Marekani uko taaban

Rais George W Bush wa Marekani amekiri kuwa uchumi wa nchi yake uko hoi na leo hii anakutana na wagombea wawili wa nafasi yake, kuzungumzia suala hilo

Rais George W. Bush

Rais George W. Bush

Rais Bush atakutana na Seneta Barack Obama wa Democratic na Seneta John McCain wa chama chake cha Republican kuzungumzia mpango wa kuingiza kiasi cha dola billioni 700 katika soko hilo kama njia za kuliokoa.


Rais Bush amewaalika wagombea hao kujaribu kutafuta hekima zao katika mpango wake huo wa kurejesha utengamavu katika soko la fedha la Marekani la Wall Street.


Barack Obama na John McCain kwa kiasi fulani wamekubaliana katika kufikiwa kwa hatua hiyo ya kuunusuru uchumi wa Marekani, ambapo Rais Bush akiliomba bunge la Congress kuidhinisha kiasi hicho cha fedha, alikiri kuwa nchi hiyo kwa sasa inakabiliwa mgogoro mkubwa sana wa kiuchumi, kiasi cha kupoteza imani ya wananchi.


Kwa upande wake mgombea wa chama cha Republican seneta McCain ametangaza kusitisha kwa muda kampeni zake na kurejea Washington kushughulikia mzozo huo uliyoyakumba mabenki na mashirika makubwa ya fedha nchini Marekani.


Akionekana kutumia mwanya huo kuvutia wapiga kura, seneta McCain ameomba kuahirishwa kwa mdahalo kati yake na mpinzani wake Seneta Obama uliyokuwa ufanyike kesho na kusema kuwa yuko tayari kushirikiana na kambi ya Seneta Obama pamoja na tume ya Rais Bush katika kushughulikia mgogoro huo.


Hata hivyo Seneta Obama ameukataa wito huo unaonekana kama chambo kwake na kutaka mdahalo huo kati yao uliyopangwa kufanyika kesho katika chuo kikuu cha Mississippi, ufanyike kama ulivyopangwa.


Obama akinadi sababu za kukataa kwake kuahirishwa kwa mdahalo huo alisema kuwa marais wanapaswa kushughulikia masuala zaidi ya moja kwa wakati mmoja..


Amesema kuwa huu ndiyo wakati haswa wananchi wa Marekani wanapaswa kujua ni nani mwenye uwezo wa kutatua tatizo hilo la kiuchumi.


Mjini Berlin Waziri wa fedha wa Ujerumani Peer Steinbrueck, ameonya kuwa madhara ya mzozo huo yataifanya Marekani kupoteza nguvu yake kama taifa kubwa kiuchumi duniani.


Lakini pia aliwatoa hofu wananchi wa Ujerumani kuhusiana na mzozo huo wa fedha duniani.


Kuyumba huko kwa masoko ya fedha duniani limekuwa suala linalogubika kikao cha kilele cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kinachoendelea hivi sasa mjini New York.

 • Tarehe 25.09.2008
 • Mwandishi Liongo, Aboubakary Jumaa
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/FOqN
 • Tarehe 25.09.2008
 • Mwandishi Liongo, Aboubakary Jumaa
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/FOqN
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com