Palestina yataka uanachama kamili ndani ya Umoja wa Mataifa
4 Aprili 2024Kiongozi wa ujumbe wa Palestina kwenye Umoja wa Mataifa, Riyad Mansour, amesema wanataka kura ya uanachama wa Palestina kwenye Umoja wa Mataifa ifanyike mwezi unaokuja.
Hadi sasa Palestina siyo mwanachama kamili wa Umoja wa Mataifa na kura yoyote ya kufanikisha hilo inapaswa ipitie kwanza Baraza la Usalama na Umoja wa Mataifa.
Hata hivyo Marekani iliyo mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama ikiwa pia kura ya turufu inapinga juhudi hizo. Imesema ingawa inaunga mkono kuundwa kwa taifa la Palestina lakini ingependelea hilo lifanyike baada ya mazungumzo na Israel.
Kwa miongo kadhaa juhudi za kuundwa taifa huru la Palestina zimegongwa mwamba. Mnamo mwaka 2012 Palestina ilipata mafanikio madogo kwa kupewa hadhi ya uangalizi kwenye Umoja wa Mataifa.