1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Palestina yalaani ziara ya waziri wa Israel eneo la Al-Aqsa

Mohammed Khelef
3 Januari 2023

Palestina imeikosoa vikali ziara iliyofanywa leo na Waziri wa Usalama wa Taifa wa Israel karibu na Msikiti Mtukufu wa Al-Aqsa, huku mataifa mengine ya Kiarabu yakiita 'uchochezi usiokubalika.'

https://p.dw.com/p/4Lh8C
Israel Jerusalem | Itamar Ben-Gvir
Picha: Atef Safadi/REUTERS

Waziri Mkuu wa mamlaka ya ndani ya Palestina, Mohammad Shtayyeh, aliliambia baraza lake la mawaziri mchana wa Jumanne (Januari 3) kwamba ziara hiyo ya Itamar Ben-Gvir, waziri wa usalama wa taifa wa Israel, kwenye eneo hilo tukufu linalowaniwa na pande zote mbili ni mbinu za kuugeuza Msikiti Mtukufu wa Al-Aqsa kuwa "hekalu la Kiyahudi." 

Ben-Gvir alilitembelea eneo tu linalouzunguka Msikiti huo bila kuufika msikiti wenyewe, akiwa chini ya ulinzi mkali. Hadi anaondoka kwenye eneo hilo, hakukushuhudiwa machafuko yoyote. 

Umoja wa Falme za Kiarabu, moja kati ya nchi chache za Kiarabu zilizorejesha mahusiano na Israel chini ya ushawishi wa Marekani mwaka 2020, ilikiita kitendo hicho kuwa ni "uvamizi dhidi ya eneo la Al Aqsa." 

Israel I West Jerusalem
Eneo la Msikiti wa Al-Aqsa mjini Jerusalem.Picha: Ahmad Gharabli/AFP/Getty Images

Jordan, ambayo ndiyo yenye dhamana ya usimamizi wa msikiti huo, iliilaani vikali ziara hiyo ya Ben-Gvir, huku Misri ikionya kile ilichokiita "matokeo mabaya ya hatua kama hiyo kwa usalama na utulivu kwenye maeneo yanayokaliwa kimabavu na eneo zima la Mashariki ya Kati, na kwa mustakabali wa mchakato wa amani."

Marekani yasema kukiuka hadhi ya Al-Aqsa hakukubaliki

Marekani, ambayo kawaida ni muungaji mkono mkubwa wa Israel, ilisema kupitia ubalozi wake mjini Jerusalem kwamba Balozi Thomas Nides "ameweka wazi kwenye mazungumzo yake na serikali ya Israel juu ya suala la kudumisha hali ya sasa ya maeneo matakatifu mjini Jerusalem na kwamba vitendo vinavyokwenda kinyume na hilo havikubaliki."

Israel | Zusammenstöße auf dem Tempelberg in Jerusalem
Vijana wa Kipalestina wakirusha mawe dhidi ya wanajeshi wa Israel katika eneo la Msikiti wa Al-Aqsa mwezi Aprili 2022.Picha: AHMAD GHARABLI/AFP/Getty Images

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema bado amedhamiria kudumisha hali ya sasa ya eneo hilo.

Kwa mujibu wa afisa mmoja kwenye ofisi yake aliyenukuliwa na shirika la habari la Reuters, "ziara kama hii zimewahi kufanywa huko nyuma na mawaziri wengine wakizingatia hali ya sasa ambayo inawaruhusu Waislamu pekee wanaoruhusiwa kuabudu hapo, ila haiwazuwii waumini wa dini nyengine kutembelea."

Msimamo wa Ben-Gvir

Kwa muda mrefu, Ben-Gvir amekuwa akitaka Mayahudi wawe na fursa kubwa zaidi ya kulitumia eneo hilo, msimamo unaochukuliwa na Wapalestina kuwa uchokozi na kisingizio cha Israel kutwaa udhibiti kamili wa eneo hilo tukufu kwa dini zote kubwa duniani. 

Israel | Zusammenstöße auf dem Tempelberg in Jerusalem
Wakati machafuko yalipojiri mwezi Aprili 2022 kati ya waandamanaji wa Kipalestina na vyombo vya ulinzi vya Israel.Picha: Mahmoud Illean/AP Photo/picture alliance

Viongozi wengi wa dini ya Kiyahudi wanawakataza waumini wa dini yao kusali kwenye eneo hilo, lakini katika miaka ya hivi karibuni vuguvugu la Mayahudi wanaounga mkono wazo la kuabudu kwenye eneo hilo limezidi kupata nguvu.

Kiongozi wa upinzani, Yair Lapid, ambaye mpaka wiki iliyopita alikuwa ndiye waziri mkuu wa Israel, aliipinga azma ya Ben-Gvir anayeongoza chama cha siasa kali za Kiyahudi, Jewish Power, na mwenye historia ya kutoa kauli za kichochezi dhidi ya Wapalestina, kutembelea eneo hilo, akisema ingezuwa machafuko yanayoweza kuhatarisha maisha ya watu." 

Vyanzo: Reuters, dpa