Nchi za Magharibi zatoa miito ya kuachiwa Alexei Navalny bila ya masharti | Matukio ya Kisiasa | DW | 18.01.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Urusi

Nchi za Magharibi zatoa miito ya kuachiwa Alexei Navalny bila ya masharti

Mataifa ya Magharibi yanaitaka Urusi imwachilie mara moja kutoka kizuizini Alexei Navalny, mkosoaji mkubwa wa serikali ya rais Vladimir Putin baada ya kukamatwa kwenye uwanja wa ndege mjini Moscow.

Kiongozi huyo wa upinzani alikamatwa hapo jana Jumapili mara tu alipowasili katika uwanja wa ndege wa Sheremetyevo mjini Moscow akitokea nchini Ujerumani ambako alikuwepo kwa muda wa miezi mitano kwa ajili ya kupata matibabu kutokana na kushambuliwa kwa sumu inayoathiri mishipa ya fahamu. Kiongozi huyo wa upinzani amedai kuwa jaribio hilo la kumuua lilifanywa na serikali ya Urusi kwa amri ya rais Vladimir Putin.

Jumuiya ya Ulaya, serikali kadhaa za nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya, Uingereza, Canada na Marekani pamoja na msaidizi mwandamizi wa Rais mteule wa Marekani Joe Biden wametoa mwito wa kuachiwa Alexei Navalny mara moja, huku viongozi wengine wa nchi za Umoja wa Ulaya wakitaka Urusi iwekewe vikwazo vipya.

Soma Zaidi:Urusi yafungua uchunguzi mpya wa jinai dhidi ya Navalny

Makundi ya kutetea haki za binadamu pia yanatoa mwito kama huo wa kuachiwa Navalny. Shirika la Amnesty International limewalaumu viongozi wa Urusi kwa kuendeleza kampeni yenye lengo la kumnyamazisha kiongozi huyo wa upinzani.

Kwa upande mwingine msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Urusi Maria Zakharova ameandika kwenye ukurasa wa Facebook, akiwaambia viongozi wa nchi za nje "waheshimu sheria za kimataifa" na "washughulikie matatizo yaliyo kwenye nchi zao."

Polisi kwenye uwanja wa ndege wa mjini Moscow kabla ya kuwasili ndege iliyombeba Alexei Navalny

Polisi kwenye uwanja wa ndege wa mjini Moscow kabla ya kuwasili ndege iliyombeba Alexei Navalny

Idara yenye mamlaka ya watu wanaowekwa kizuizini wakiwa ni washukiwa au wale ambao tayari wameshahukumiwa FSIN kwenye taarifa yake imesema Navalny amezuiliwa kutokana na kukiuka sheria juu ya adhabu iliyomkabili kutokana na makosa ya ulaghai, iliyosimamishwa kwa muda mnamo mwaka 2014. Imeelezwa kwenye taarifa hiyo kwamba kiongozi huko wa upinzani atabaki kizuizini hadi uamuzi wa mahakama utakapotolewa.

FSIN imesema hapo awali ilimwonya Navalny juu ya uwezekano wa kukamatwa kwa sababu ya kukosa kutimiza masharti alipokuwa nchini Ujerumani, na pia kuhusu kutoripoti kwenye vyombo vya usalama mara mbili kwa mwezi kama alivyotakiwa.

Waziri wa Mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov amesema wanachokifanya nchi za Magharibi kuhusiana na makosa yanayomkabili Alexei Navalny, ni sawa na kujitwika mzigo usio kuwa wao ili kuzifunika shida zilizopo kwenye nchi hizo za Magharibi.

Vyanzo: RTRE/AFP