Nato yafiifiisha mvutano pamoja na Urusi kuhusu Georgia | Matukio ya Kisiasa | DW | 28.08.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Nato yafiifiisha mvutano pamoja na Urusi kuhusu Georgia

Rais wa ufaransa Nicholas Sarkozy asema "hakuna anaetaka vita baridi virejee"

Katibu mkuu wa jumuia ya NATO de Hoop Scheffer na rais Medvedev wa Urusi

Katibu mkuu wa jumuia ya NATO de Hoop Scheffer na rais Medvedev wa UrusiMataifa kadhaa ya Umoja wa Ulaya yanazingatia haja ya kuwekewa Urusi vikwazo kufuatia mzozo wa Georgia.Lakini lakini jumuia ya kujihami ya magharibi NATO inakanusha ripoti za kuimarisha manuwari zake katika bahari nyeusi.Jumuia ya kujihami ya magharibi NATO imesema hii leo manuari zake nne zilizoko katika bahari nyeusi zinashiriki katika luteka zilizopangwa muda mrefu uliopita na kwamba kuwepo kwa manuari hizo hakumaanishi hata kidogo kuzidi makali mzozo wa Georgia.Jumuia ya kujihami ya magharibi NATO,tangu wiki iliyopita ilitangaza inatuma manuari tatu,moja ya Hispania,ya Ujerumani na ya Poland kujiunga na manuari ya Marekani kwaajili ya kufanya luteka na kuzizuru bandari za Rumania na Bulgaria.


Jana lakini naibu kiongozi wa vikosi vya wanajeshi wa Urusi alisema mjini Moscow "jeshi la wanamaji la Urusi linachunguza kwa makini" kuimarishwa vikosi vya NATO katika eneo hilo."


"Nato haijiimarishi katika bahari nyeusi" amejibu hii leo kamanda Kevan McHale wa kutoka uongozi wa NATO barani Ulaya.


Jumuia ya kujihami ya magharibi NATO imesema katika taarifa yake "walituma maombi ya luteka hizo tangu mwezi June uliopita,hata kabla ya mzozo wa Georgia kuripuka.


Nae mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa ulaya,rais Nicholas Sarkozy wa Ufaransa ameitolea mwito Urusi iwaondowe haraka wanajeshi wake kutoka Georgia.Hata hivyo amesisitiza kwamba NATO si hasimu bali mshirika wa Urusi.


Rais Nicholas Sarkozy ameendelea kusema:


"Hakuna yeyote anaependelea vita baridi virejee.Jumuia ya kujihami ya magharibi NATO si mpinzani,ni mshirika wa Urusi."


Wakatri huo huo lakini waziri wake wa mambo ya nchi za nje Bernard Kouchner,akizungumza na waandishi habari pembezoni mwa mkutano wa 16 wa mabalozi wa Ufaransa mjini Paris hii leo amesema nchi kadhaa za umoja wa Ulaya zinafikiria uwezekano wa kuwekewa vikwazo Urusi kwa sababu ya mzozo wa Georgia.


"Kuna wanaoshauri vikwazo na wengine wanaopinga" amesema waziri huyo wa mambo ya nchi za nje na kuongeza kwamba nchi yake,Ufaransa itafanya kila liwezekanalo kusaka ridhaa ya wanachama wote 27 wa Umoja wa ulaya,mkutano wa dharura utakapoitishwa jumatatu ijayo.


Ufaransa,Ujerumani na Italy hazijasema chochote kuhusu madai ya kuwekewa vikwazo Urusi,katika wakati ambapo Uengereza ikiungwa mkono na nchi za mashariki,inapigania uamuzi mkali upitishwe jumatatu ijayo mjini Brussels dhidi ya kuzidi makali mvutano kati ya Moscow na Georgia.


Akiwa ziarani Tadjikistan,waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi Serguei Lavrov amekosoa kile alichokiita "matafaruku wa kina miongoni mwa nchi za magharibi".


Waziri huyo wa mambo ya nchi za nje wa Urusi alikua Djunabe nchini Tadjikistan kuhudhuria mkutano wa jumuia ya ushirikiano wa washirika wa Moscow katika bara la Asia inayojulikana kama "jumuia ya ushirikiano ya Shangai".


Rais Dmitri Medvedev pia alihudhuria mkutano huo wa kilele mjini Djunabe.


Jumuia hiyo inazileta pamoja Urusi,Uchina,Tadjikistan,Uzbewkistan,Kirgizistan na Kazakhstan.


Kinyume na viongozi wa Urusi walivyotarajia wajumbe mkutanoni hawakuelezea kinaga ubaga kuunga mkono uamuzi wa Urusi wa kutambua uhuru wa majimbo yaliyojitenga ya Georgia Ossetia ya kusini na Abkhasia.
 • Tarehe 28.08.2008
 • Mwandishi Hamidou, Oumilkher
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/F6dk
 • Tarehe 28.08.2008
 • Mwandishi Hamidou, Oumilkher
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/F6dk
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com