Mzozo wa Gesi, kati ya Urusi na Ukraine. | Matukio ya Kisiasa | DW | 07.01.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mzozo wa Gesi, kati ya Urusi na Ukraine.

Urusi imesema iko tayari kuanza tena mazungumzo na Ukraine, katika juhudi za kumaliza mzozo wa Gesi kati ya nchi hizo mbili ambao tayari umeathiri nchi mbalimbali barani Ulaya.

Mitambo ya gesi ya Urusi nchini Ukraine.

Mitambo ya gesi ya Urusi nchini Ukraine.

Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya gesi ya Urusi Gazprom, Alexandra Medvedev amesema leo kwamba wako tayari kuanza mazungumzo wakati wowote na Ukraine.

Amesema kuwa hali inazidi kuwa mbaya, ambapo jana usiku Ukraine ilifunga mabomba yote ya gesi inayosafirishwa kwenda Ulaya kupitia nchini humo.

Naibu Mkurugenzi huyo wa Gazprom amesema matatizo zaidi yanayweza kutokea, hususan katika kipindi hiki cha majira ya baridi iwapo mabomba hayo yanayopitishia gesi hayatatumika.

Kwa upande wake Ukraine nayo pia imeishutumu Urusi kufunga mabomba yake yanayopitisha gesi hiyo kuelekea Ulaya.

Msemaji wa kampuni ya gesi ya Ukraine ya Naftogaz Valentyn Zemlyansky amesma kampuni ya Gesi ya Urusi, kuanzia leo asubuhi imeacha kabisa kutuma gesi hiyo kwa wateja wake barani Ulaya.

Tayari Bulgaria,l Ugiriki, Romania, Croatia, Serbia, Uturuki na Slovakia zimeripoti kwamba zimekatiwa usambazaji huo wa gesi, wakati Ufaransa, Austria, Poland, Hungary na Ujerumani zikithibitisha kushuka kwa kiwango kikubwa cha usambazaji wa gesi.

Viongozi wa nchi hizo tayari wametoa kauli mbalimbali kutokana na kukatiwa gesi hiyo, ambayo inaweza kuleta madhara zaidi kiuchumi katika nchi zao.

Akizungumzia kuhusu mzozo huo, Waziri wa Uchumi wa Ujerumani Michael Glos ametaka nchi hizo mbili kutatua mzozo wao, kutokana na kwamba unaleta athari zaidi kwa nchi nyingi.

Amezitaka Urusi na Ukraine kukaa pamoja na mwishowe zianze kutekeleza wajibu wao wa kutuma gesi.

Amesema hayuko katika hali ya kuamua nani mwenye haki na nani asiye na haki, lakini ameongeza kwamba nchi nyingine nyingi zitajikuta kama mateka katika mabishano haya baina ya Ukraine na Urusi.

Nao Umoja wa Ulaya umesema hali hiyo haikubaliki na umeitaka Urusi iendelee kusafirisha gesi yake kama kawaida.

Maelfu ya watu wanakabiliwa na baridi majumbani, ikiwa ni athari za kukatwa kwa gesi hiyo, hususan katika kipindi hiki cha baridi, ambacho wateja wengi barani Ulaya hutegemea gesi hiyo katika kuleta hali ya Ujoto majumbani mwao.

Urusi ilifunga mabomba yake yanayosambaza gesi nchini Ukraine Januari mosi, baada ya nchi hiyo kushindwa kutatua mzozo wao juu ya malipo inayotakiwa kulipia, gesi hiyo ya Urusi.

Urusi pia inaishutumu Ukraine kwa kuiba gesi yakei inayosafirishwa kwa wateja wa barani Ulaya kupitia nchi hiyo.


 • Tarehe 07.01.2009
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GTWC
 • Tarehe 07.01.2009
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GTWC
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com