1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwanasiasa mwengine wa India ajiuzulu wakati hasira ikizidi kuchemka dhidi ya mashambulizi ya Mumbai

Mohamed Dahman1 Desemba 2008

Mwanasiasa mwengine mwandamizi wa India ameomba kujiuzulu leo hii kutokana na mashambulizi ya mji wa Mumbai ambayo yametibuwa uhusiano kati ya India na hasimu yake mwenye kumiliki silaha za nuklea Pakistan.

https://p.dw.com/p/G6n8
Hoteli ya Taj Mahal ni mojawapo ya sehemu mashuhuri za Mumbai zilizoshambuliwa na Waislamu wa itikadi kali.Picha: AP

Mashambulizi hayo pia yamedhoofisha serikali ya nchi hiyo kabla ya uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika hapo mwezi wa Mei mwakani.

Waziri Mkuu wa jimbo la Maharashtra Vilasrao Deshmuk ambaye ni mwanachama wa chama tawala cha Congress amesema leo hii ameomba kujiuzulu kutokana na mashamaulizi hayo ya mji wa Mumbai yaliouwa watu 183 na kuufunga mji mkuu huo wa biashara nchini India kwa siku tatu.

Deshmukh amewaambia waandisbi wa habari kwamba ameomba kujiuzulu na kwamba anasuburi viongozi wa chama kutowa uamuzi wa mwisho.

Ombi lake la kutaka kujiuzulu linafuatia kujiuzulu kwa waziri wa mambo ya ndani wa India Shivraj Patil hapo Jumapili na tangazo la Waziri Mkuu wa India Manmohan Singh la kufanya mabadiliko makubwa kwa taasisi za taifa kukabiliana na ugaidi.

Mashambulizi hayo dhidi ya hoteli mbili mashuhuri za kifahari za Mumbai na sehemu nyengine mashuhuri za mji huo wenye wakaazi milioni 18 yametishia juhudi za kuboresha uhusiano kati ya India na nchi jirani ya Pakistan.

Gazeti la Financial Times limeripoti leo hii kwamba Rais Asif Ali Zardari wa Pakistana ameiomba India kutoiadhibu nchi yake kutokana na mashambulizi hayo ya juma lililopita kwa kusema kwamba wanamgambo wanaweza kuchochea vita.

Zardari ambaye mke wake Benazir Bhutto ameuwawa na wanamgambo wa itikadi kali za Kiislam mwaka jana ameonya kwamba uchokozi unaofanywa na wahuni wasio kwenye serikali unahatarisha kurudia vitani kwa nchi hizo mbili zenye kumilki silaha za nuklea.

Wachambuzi wa mambo wamesema mashambulizi hayo ya Mumbai ya wanamgambo wa itikadi kali za Kiislam yana alama ya kundi la Lashkar-e- Taiba lenye makao yake nchini Pakistan ambalo linalaumiwa kwa kufanya mashambulizi nchini India ikiwa ni pamoja na mripuko wa mwaka 2001 katika bunge ambao ulikuwa karibu kabisa kuzitumbukiza nchi hizo mbili katika vita vyao vya nne.

Maafisa wa India wamesema washambuliaji 10 ambao waliushikilia mateka mji wa Mumbai kwa mashambulizi ya wazimu kwa kutumia bunduki za rashasha na mabomu ya mkono wametokea Pakistan taifa la Kiislam lililoenguliwa kutoka taifa la India lenye wakaazi wengi wa Kihindu hapo mwaka 1947.

Wakaazi wa Munbai wamerudi mashuleni na maofisini leo hii kwa mara ya kwanza tokea kuzuka kwa mashambulizi hayo na wakaazi wa mji mkuu wa India New Delhi hapo jana wamekusanyika kwa kuwasha mishumaa na kushikana mikono,kuimba nyimbo na kubeba mabango kukumbuka wahanga na wengine wakipinga kile wanachokiona kama serikali kushindwa kuchukuwa hatua.

Ikulu ya Marekani imesema kwamba Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condoleezza Rice atakwenda India hapo Jumaatano.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani Dana Perino amesema katika taarifa kwamba ziara hiyo ya Rice ni kielelezo chengine cha kujizatiti kwa Marekani katika mshikamano na wananchi wa India kwa kuwa wote wanashirikiana kuwawajibisha watu wa itikadi kali.

Rice amekuwa katika mawasiliano na mawaziri wa mambo ya nje wa India na Pakistan katika siku za hivi karibuni kupunguza mvutano kati ya mataifa hayo mawili na suala hilo linategemewa kuwa mada kuu katika mikutano yake na maafisa wa serikali ya India.

Serikali ya India imesema hapo jana imeimarisha hatua zake za usalama na kuziweka katika kiwango cha vita na kwamba haina mashaka kuwa Pakistan ilikuwa na mkono wake katika mashambulizi hayo ya Mumbai.