Muunganao mwingine mkubwa wafanyika katika sekta ya benki ya Ujerumani | Masuala ya Jamii | DW | 11.09.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Muunganao mwingine mkubwa wafanyika katika sekta ya benki ya Ujerumani

Benki ya Deutsche kununua asilimia 29.75 ya hisa za benki ya Posta

default

Mkuu wa benki ya Deutsche Josef Ackermann

Katika hatua ya kwanza benki ya Deutsche Bank itanunua asilimia 29.75 ya hisa za benki ya Posta, ambayo matawi yake karibu yote yako kwenye ofisi zake hapa Ujerumani. Hayo ni kwa mujibu wa vyanzo vya kifedha vilivyo karibu na mazungumzo hayo yaliyofanyika hapa mjini Bonn hapo jana.

Benki ya Deutsche Bank ilisema Jumanne wiki hii kwamba ilikuwa imefikia mbali katika hatua za mwisho za mazungumzo ya kutaka kuinunua sehemu ya benki ya Posta ya Ujerumani. Makubaliano yaliyofikiwa ambayo huenda yakawa ya thamani ya euro bilioni saba huenda yakaashiria hatua kubwa mbele kwa benki ya Deutsche Bank.

Kama kitengo cha posta ya Ujerumani, Deutsche Post, benki ya Postbank ina mtandao mkubwa wa wateja hapa Ujeruamni huku wateja wake zaidi ya milioni 14 wakiweza kupata huduma katika ofisi yoyote ya Posta nchini kote.

Benki ya Deutsche Bank ikiwa na wateja chini ya milioni 10 hapa Ujerumani, inatarajiwa kupata msukumo mpya kwa upande wa matawi na wateja kufuatia hatua ya benki ya Commerz kutangaza kuinunua benki ya Dredner kwa thamani ya euro bilioni 9.8 mnamo Agosti 31 mwaka huu.

Benki ya Deutsche Bank hata hivyo inabakia kuwa mkopeshaji mkubwa kulingana na thamani ya mali na kitengo chake cha uwekezaji kinaifanya kuwa benki pekee ya Ujerumani yenye nafasi kubwa kwenye masoko ya hisa ya Wall Street mjini New York Marekani na wilaya ya fedha ya Square Mile mjini London nchini Uingereza.

Baada ya miaka ya changamoto nyingi, makubaliano kati ya benki ya Deutsche Bank na Postbank yatakuwa ya hivi karibuni kufanywa katika sekta ya benki ambapo vyama vya ushirika na benki ya hazina ya Sparkasse inayomilikiwa na serikali bado ina ushawishi mkubwa.

Kabla benki ya Commerz kuungana na benki ya Dresdner, benki ya Ufaransa Credit Mutuel iligonga vichwa vya habari mwezi Julai mwaka huu ilipotangaza kwamba inainunua benki ya Ujerumani ya Citibank yenye wateja milioni 3.3 kwa kiasi cha euro bilioni 4.9.

Na katika makubaliano mengine mwezi uliopita benki ya IKB ilikuwa muhanga kwa mzozo wa mikopo ya nyumba nchini Marekani kwa kuuzwa kwa kampuni ya kibinafsi ya Marekani ya Lone Star kwa kiasi kinachosemakana kufikia euro milioni 150.

Posta ya Ujerumani Deutsche Post imekuwa ikitafuta mnunuzi wa hisa zake zaidi ya asilimia 50 katika benki yake ya Postbank. Na huku benki ya Commerz ikiwa imeinunua benki ya Dresdner hivi majuzi, haingeweza kununua hivyo kuiachia uwanja benki ya Deutsche Bank.

Ikiwa Deutsche Bank itakubali kununua asilimia 30 ya hisa za benki ya Posta, itatakikana kwa mujibu wa sheria za Ujerumani kuwasilisha ombi la kuzinunua hisa zitakazosalia ambazo zimesajiliwa kwenye masoko ya hisa.

Ikizingatiwa bei ya hisa za benki ya Posta za wakati huu, hii itakuwa na maana kwamba benki ya Deutsche Bank huenda ikalazimika kutumia euro bilioni saba zaidi, ambayo itaitaka kuchangisha fedha za kugharamia ununuzi huo.

Lakini vyombo vya habari vimeashiria kwamba benki ya Deutsche Bank inataka kuzuia kuwasilisha ombi la kuzinunua hisa zote za benki ya Posta kwa kununua hisa chini ya asilimia 30. Gazeti la General Anzeiger limeripoti kwamba benki ya Deutsche Bank inataka kununua asilimia 29.75 ya hisa za benki ya Posta.

 • Tarehe 11.09.2008
 • Mwandishi Charo, Josephat
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/FGHh
 • Tarehe 11.09.2008
 • Mwandishi Charo, Josephat
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/FGHh
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com