Msiwe na hofu! yasema EU kuhusu virusi vya H1N1
1 Mei 2009Kauli hiyo imetolewa baada ya Ufaransa kupendekeza hatua ya kupiga marufuku safari za ndege hizo kama njia moja ya kuzuia usambaaji wa virusi vya homa hiyo katika bara la Ulaya.Maafisa wa Afya wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya walikutana Luxembourg hapo jana ili kujadili mbinu za pamoja za kuzuia ueneaji wa virusi hivyo zinazojumuisha kushirikiana katika masuala ya dawa za kupambana na virusi hivyo pamoja na chanjo.
Mkutano huo ulifanyika baada ya Shirika la Afya Ulimwenguni WHO kuongeza makali ya tahadhari ya kusambaa kwa virusi vya H1N1 hadi awamu ya tano.Hata hivyo bado halijakuwa janga la kimataifa.Virusi hivyo vimebainika katika mataifa 29 na mabara manne kote ulimwenguni.Canada imethibitisha kuwa mtu mmoja ameambukizwa virusi hivyo na binadamu.
Visa vipya vya maambukizi barani Ulaya vimeripotiwa Holland na Switzerland.Ujerumani,Uingereza,Uhispania na Austria kadhalika zimethibitisha kuwa virusi vya H1N1 vimeingia katika nchi zao nayo mataifa mengine ya bara hilo yako chonjo.
Mwandishi:Thelma Mwadzaya /RTRE,DPA,AFPE