Mkutano wa kimataifa juu ya maradhi ya Ukimwi umemalizika mjini Sydney Astralia | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 25.07.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Mkutano wa kimataifa juu ya maradhi ya Ukimwi umemalizika mjini Sydney Astralia

Wito umetolewa kwa makampuni makubwa ya kutengeneza dawa kufanya juhudi za kutengeneza dawa za kupunguza makali ya Ukimwi kwa watoto walioambukizwa virusi vya HIV..

watoto walioambukizwa HIV kutengenezewa dozi ya kupunguza makali ya ukimwi

watoto walioambukizwa HIV kutengenezewa dozi ya kupunguza makali ya ukimwi

Wito huo umetolewa baada ya utafiti kuonyesha kwamba matibabu ya mapema kwa watoto wadogo walioambukizwa virusi vya HIV yanaweza kupunguza idadi ya vifo kwa asilimia 75.

Mkutano huo wa kimataifa juu ya maradhi ya ukimwi ukifunga pazia leo hii mtafiti wa Marekani Annette Sohn amesema watoto kiasi 78000 ulimwenguni wanahitaji dawa za kupunguza makali ya Ukimwi lakini ni asilimia 15 pekee ya watoto hao ambao wameweza kupata matibabu hayo.

Sohn ambaye ni Professa msaidizi katika kitengo kinachoshughulikia magonjwa ya watoto cha San Fransisco katika chuo kikuu cha Califonia amesema hakuna dawa maalum zilizotengenezwa kwa ajili ya watoto walio na virusi vya Hiv hali ambayo inawafanya kutumia dawa za watu wazima ambazo huzivunja mara mbili ili kufikia kiwango kidogo cha dozi inachohitajika kupewa watoto.

Sohn pia amebainisha kuwa utafiti unaonyesha mtoto akianzishiwa mapema matibabu ya ukimwi kuna uwezekano mkubwa wa mtoto huyo kuweza kuishi kwa muda mrefu.

Hata hivyo amekiri watu wengi huchukua muda mrefu kuanza kuwafikisha watoto hospitali kwa ajili ya kupokea matibabu ya Ukimwi.

Kwa upande wake rais wa jumuiya ya kimataifa inayohusika na kupambana na Ukimwi Dk Pedro Cahn amesema katika kikao cha leo kwamba lazima juhudi za haraka zifanyike kuokoa kikazi kijacho kwa kutafuta njia bora za kutibu watoto walioambukizwa virusi vya HIV.

Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanyika nchini Afrika Kusini imebainika vifo vya watoto wachanga walioanzishiwa matibabu ya kupunguza makali ukimwi wakiwa na umri wa miezi mitatu vimepungua kwa asilimia 75 ikilinganishwa na wale ambao hawajaanzishiwa matibabu hayo mapema.

Utafiti huo ulifanywa kwa watoto 377 katika miji ya Cape Town na Soweto.

Kulingana na wataalamu wa maradhi ya Ukimwi kwa kawaida watoto wanaozaliwa na wazazi walio na virusi vya HIV hawaanzishiwi matibabu katika kipindi cha miezi 12 ya mwanzo hii ni kwasababu watoto huzaliwa wakiwa tayari na kinga ya mwili kutoka kwa mama na huchukua muda mrefu kama huo kubainisha ikiwa mtoto ameambukizwa virusi hivyo au la.

Utafiti huo hata hivyo unamaanisha kuwa itabidi kufanyika juhudi za mapema kukabiliana na maambukizi kwa watoto wachanga.

Mkutano wa siku nne mjini Sydney Australia uliweza kutafakari tafiti zaidi ya 1000 juu ya maradhi ya ukimwi ambapo watalaamu 5000 walihudhuria.

Mkutano huo kwa mujibu wa mkurugenzi mtendaji wa jumuiya ya kimataifa ya kupambana na Ukimwi IAS Craig McClure ulifanikiwa kwa kiasi kikubwa ambapo pia uliweza kupata ufumbuzi juu ya dawa ambayo huenda ikatoa matumaini makubwa kwa watu wanaoishi na virusi na ugonjwa wa Ukimwi.

Mkutano mwingine kama huo utafanyika nchini Afrika kusini mwaka 2009.

 • Tarehe 25.07.2007
 • Mwandishi Saumu Mwasimba
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CB2S
 • Tarehe 25.07.2007
 • Mwandishi Saumu Mwasimba
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CB2S

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com