Mkutano wa kilele wa jumuia ya nchi za kiarabu mjini Doha Qatar | Matukio ya Kisiasa | DW | 30.03.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mkutano wa kilele wa jumuia ya nchi za kiarabu mjini Doha Qatar

Viongozi wa kiarabu wasaka umoja kati yao

Rais Bashar al Assad wa Syria akihutubia mjini Doha-Qatar

Rais Bashar al Assad wa Syria akihutubia mjini Doha-Qatar

Rais Omar el Bashir wa Sudan amepuuza amri ya korti ya kimataifa ya uhalifu na kuhudhuria mkutano wa kilele wa jumuia ya nchi za kiarabu mjini Doha nchini Qatar.Zaidi kuhusu mkutano huo wa kilele unaohudhuriwa pia na katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban-Ki-Moon .


Mnamo mkesha wa kuidhinishwa serikali mpya ya Israel itakayoongozwa na Benjamin Netanyahu,rais Bachar el Assad wa Syria amelitumia jukwaa la mkutano huo wa kilele kuonya akisema" waarabu hawana mshirika wa kweli wa amani nchini Israel."


Kwa upande wake katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon ameitolea mwito serikali mpya ya Israel "isitishe ujenzi wa makaazi ya wahamiaji wa kiyahudi,ikomeshe hatua za upande mmoja katika eneo la mashariki la Jerusalem na inedeleze mazungumzo ya amani pamoja na wapalastina.


Zaidi ya hayo katibu mkuu wa Umoja wa mataifa,aliyeamua kushiriki katika mkutano huo wa kilele wa jumuia ya nchi za kiarabu licha ya kuhudhuriwa na rais el Bashir ,ameisihi Sudan ibatilishe uamuzi wa kuyafukuza mashirika 13 ya kimataifa yasiyo milikiwa na serikali huko Darfour.


Sudan imeamua kuwafukuza watumishi wa mashirika hayo ya kimataifa pamoja na kuyafunga mashirika mengine matatu ya nchi hiyo baada ya korti ya kimataifa kutangaza rais Omar el Bashir akamatwe kwa tuhuma za kuhusika na uhalifu wa vita na uhalifu dhidi ya ubinaadam huko Darfour.


Akijibu hoja za korti kuu ya kimataifa kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi anasema:


O-Ton Gaddafi


"Si haki kuamuru kiongozi wa taifa akamatwe.Na tukiruhusu hivyo basi na waliouwa Irak na Gaza pia wakamatwe na wafikishwe mahakamani."


Viongozi wa kiarabu wametangaza kumuunga mkono rais El Bashir na wanatazamiwa kuitaka korti kuu ya kimataifa ibatilishe amri hiyo.


Rais Bashar el Assad aliyekua wa mwanzo kulizusha suala hilo ametilia mkazo zaidi pia,hali ya Mashariki ya kati,siku moja kabla ya serikali ya Benjamin Netanyahu kuapishwa nchini Israel.


"Kuingia madarakani serikali ya mrengo wa kulia haibadilishi chochote nchini Israel kwasababu,mrengo wa kulia ,sawa na mrengo wa shoto na wa kati,wote wanatoa picha moja nayo ni kwamba jamii ya Israel haiko tayari kwa amani"-amesema rais Bashir al Assad wa Syria,aliyeongeza tunanukuu "Inamaanisha wazi kabisa kwamba tangu tulipotia njiani juhudi za amani,hatuna mshirika wa kweli wa utaratibu wa amani."


Mustakbal wa mpango huo wa amani ulioshauriwa na Saud Arabia ambao Israel haujaukubali,ni miongoni mwa mada zitakazojadiliwa katika mkutano huu wa 21 wa kilele mjini Doha,sawa na utaratibu wa kuzisuluhisha nchi za kiarabu.


Uamuzi wa rais Hosni Mubarak wa Misri na viongozi wa nchi nne nyengine za kiarabu kutohudhuria mkutano huo wa kilele unazitia dowa juhudi za suluhu kati ya nchi za kiarabu. • Tarehe 30.03.2009
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/HMvc
 • Tarehe 30.03.2009
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/HMvc
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com