1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Mkutano ujao wa BRICS huenda ukafanyika Urusi

Mohammed Khelef
23 Agosti 2023

Rais Vladimir Putin wa Urusi amewaalika viongozi wenzake wa Umoja wa Nchi Zinazoinukia Kiuchumi, BRICS, kufanya mkutano wa kilele ujao nchini mwake, huku mwenyewe akishindwa kushiriki mkutano wa Johannesburg.

https://p.dw.com/p/4VVjt
Südafrika Johannesburg | Brics-Gipfel | Präsident Vladimir Putin
Picha: picture alliance / ASSOCIATED PRESS

Kwenye hotuba yake iliyorushwa kwa njia ya video katika ukumbi wa mikutano jijini Johannesburg, Putin aliwaalika wawakilishi wa mataifa mengine wanachama wa BRICS: Brazil, India, China na mwenyeji wa mara hii, Afrika Kusini, kwenye mji wa Kazan mwezi Oktoba mwakani.

Ingawa tarehe mahsusi haijatajwa, Putin alitangaza kwamba kutakuwa na matukio zaidi ya 200 ya kisiasa, kiuchumi na kijamii chini ya uwenyekiti wa nchi yake kwa BRICS mwaka ujao. Mkutano wa mwaka huu unamalizika kesho Alkhamis.

Waranti ya kukamatwa Putin

Mkutano wa BRICS 2023 Afrika Kusini
Rais Luiz Inacio Lula da Silva wa Brazil, Xi Jinping wa China, Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini, Waziri Mkuu wa India Narendra Modi na waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov.Picha: Alet Pretorius/REUTERS

Hati ya kumkamata Putin iliyotolewa na Mahakama ya ICC kwa shutuma za kuhusika na uhalifu nchini Ukraine inamaanisha kuwa kiongozi huyo angekabiliwa na uwezekano wa kukamatwa lau angelihudhuria mkutano nchini Afrika Kusini, kwani nchi hiyo ni mwanachama wa ICC.

Rais Xi Jinping wa China, Luiz Inacio Lula da Silva wa Brazil, Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi wanahudhuria wenyewe mkutano huo wa kilele.

Mjadala wa leo ulijikita kwenye jinsi jumuiya hiyo inavyoweza kuwasajili wanachama wapya wakati huu ikijipambanuwa kama taasisi ya kilimwengu mbali ya zile zinazodhibitiwa na mataifa ya Magharibi.

China, ambayo ndiyo yenye uchumi mkubwa zaidi kwenye umoja huo, inataka kuandikisha wanachama wapya kuharakishwe wakati huu ushindani na Marekani ukizidi.

Tayari mataifa 40 yamejipanga yakingojea kusajiliwa kuwa wanachama wa BRICS, lakini kwa sasa kikwazo kikubwa ni India, mwanachama mwengine mwenye nguvu, ndiyo yenye wasiwasi na kutanuka haraka kwa jumuiya hiyo.

Soma hii pia: Mkutano wa jumuiya ya BRICS waanza mjini Johannesburg

New Delhi inaamini kuwa Beijing inapigania kutanuka kwa BRICS ili kutanuwa himaya yake binafsi ya kiuchumi duniani kwa kutumia mgongo wa jumuiya hiyo.

BRICS Johannesburg
Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov aliyemwakilisha Rais PutinPicha: Gianluigi Guercia/Reuters

Brazil na Afrika Kusini zinaunga mkono utanukaji huo, ambapo Rais Lula da Silva wa Brazil amesema yuko tayari kuipokea Argentina.

Mataifa mengine yaliyo mbioni kujiunga ni Saudi Arabia, Algeria, Ethiopia na Iran.

Asilimia 40 ya watu wote waliopo ulmwenguni wanaishi sasa kwenye mataifa matano waanzilishi wa BRICS, ambayo kwa pamoja yanahodhi robo nzima ya uchumi wa dunia.Afrika Kusini na China zina maoni sawa kuitanua BRICS

Lengo la kutanuwa uwanachama ni kuiruhusu jumuiya hiyo kuyaleta pamoja mataifa yenye chumi kubwa ama ndogo, yenye serikali za kidemokrasia ama kidikteta ili kujenga chombo mbadala kinachofuata utaratibu tafauti wa kilimwengu na ule uliowekwa na kusimamiwa na mataifa ya Magharibi.

Vyanzo: dpa, AFP