Mkutano kati ya serikali ya Ujerumani na Israel wakamilika Berlin | Matukio ya Kisiasa | DW | 19.01.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mkutano kati ya serikali ya Ujerumani na Israel wakamilika Berlin

Maswala nyeti hayakuzingatiwa

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu

Kwenye mkutano wa kwanza kati ya serikali ya Ujerumani na ya Israel mjini Berlin hapo jana, Ujerumani kwa maneno ya wazi kabisa, imejiepusha mbali na siasa za Mashariki ya Kati. Ni jambo la kusikitisha.

Tangu miaka miwili iliyopita, kumekuwepo mashauriano kati ya serikali mbili za Israel na Ujerumani. Yalianzishwa ili kuimarisha uhusiano katika ya nchi hizo mbili na pia kutokana na historia, kusisitiza jukumu la Ujerumani kwa wayahudi. Yanakamilisha mashauriano ambayo yamekuwepo kwa kipindi kirefu kati ya Israel na Ufaransa na kati ya Israel na Poland.

Ama kweli hilo ni wazo zuri. Ujerumani inaweka wazi kwamba inaelewa jukumu lake kwa wahanga wa mauaji ya Wayahudi kama inavyolielewa jukumu lake la leo ililo nalo barani Ulaya. Lakini hata baada ya mkutano kati ya serikali ya Ujerumani na Israel mjini Berlin kumalizika, bado kunabakia shaka shaka. Kwani huku serikali ya Ujerumani ikiwa inafurahia uhusiano wa chanda na pete na serikali ya Israel mjini Jerusalem, Wajerumani wengi zaidi wanajiuliza maswali kuhusu mshikamano huu usiokuwa na masharti yoyote.

Sera ya Israel kujenga makaazi ya raia wake haieleweki wala haikubaliki. Vita vya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza vimewaghadhabisha Wajerumani wengi zaidi na kusababisha maudhi. Lakini mada hizi hazikuwemo katika ajenda ya mkutano kati ya serikali ya Ujerumani na Israel.

Kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Berlin, kansela wa Ujerumani, Bi Angela Merkel, amekiri baada ya mkutano kumalizika kwamba hawakujadiliana maswala yoyote maalum kuhusu Gaza na waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.

Sera ya ujenzi wa makaazi ya walowezi pia hawakuigusia, ingawa tayari ujenzi unaendelea katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa mto Jordan, ingawa suluhu ya mataifa mawili inayoungwa mkono na kansela Merkel inakataza ujenzi wa makaazi hayo.

Je kansela Merkel na waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, wamejadiliana kuhusu nini hasa? Na je waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Guido Westerwelle na mwenzake wa Israel, Avigdor Lieberman, nao walizungumzia nini? Na waziri wa ulinzi wa Israel, Ehud Barak na mwenzake wa Ujerumani, Theodor zu Guttenberg, walizungumzia maswala gani?

Kuhusu Iran kansela Merkel amesisitiza kwamba wamezungumzia kitisho kinachoikabili Israel kutokana na mpango wa nyuklia wa Iran. Wamezungumzia pia kujenga ushirikiano wa kiuchumi na uhusiano wa karibu kati ya wanasayansi wa Ujerumani na Israel.

Na je pia wamezungumzia kuhusu Ujerumani kuipelekea Israel silaha zaidi? Tayari Israel imepokea nyambizi tano za kisasa kutoka Ujerumani. Hii ni silaha ya thamani kubwa zaidi inayomilikiwa na jeshi la Israel na ambayo inalipiwa ruzuku na serikali ya Ujerumani. Sasa serikali ya Israel mjini Jerusalem inataka nyambizi nyengine moja zaidi pamoja na manuari za kukabiliana na mashamulio ya makombora na manuari nyengine ndogo.

Silaha hizi zinaweza kutumiwa wakati Israel itakapolazimika kuishambulia Iran au wakati wa kushika doria katika hatua ya Israel kuuzingira Ukanda wa Gaza. Katiba ya Ujerumani inapiga marufuku uuzaji wa silaha za kivita kutumiwa katika maeneo ya mizozo. Lakini inaonekana kuhusu Israel sheria hizi zote hazifanyi kazi. Hapa maswala ya haki za binadamu na uhalifu wa kivita hayana umuhimu wowote kwa kuwa jambo linalotiliwa maanani sana ni usuhuba na Israel.

Rafiki mzuri ni yule asiyemruhusu mwenzake kuendesha gari akiwa amelewa chakari, ndivyo wasemavyo wanaharakati wa kupigania amani nchini Israel. Wanaitaka jumuiya ya kimataifa iingilie kati hususan kuhusu kupatikana suluhisho la amani Mashariki ya Kati. Wanaharakati hao wamewatolea mwito marafiki wa Israel waishawishi dhidi ya sera ya ujenzi wa makaazi ya wayahudi, kuusambaratisha mchakato wa kusaka amani, kuuzingira Ukanda wa Gaza na vitisho dhidi ya Iran.

Lakini katika mkutano wa mjini Berlin kati ya serikali ya Ujerumani ya Israel, mambo haya ya umuhimu mkubwa katika kufikia amani ya Mashariki ya Kati hayakuzingatiwa.

Mwandishi: Marx, Bettina/Charo, Josephat/ZR

Mhariri: Miraji Othman

 • Tarehe 19.01.2010
 • Mwandishi Josephat Nyiro Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/La4t
 • Tarehe 19.01.2010
 • Mwandishi Josephat Nyiro Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/La4t
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com