MINSK: Belarus na Urusi zafikia makubaliano ya kusafirisha mafuta | Habari za Ulimwengu | DW | 10.01.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Habari za Ulimwengu

MINSK: Belarus na Urusi zafikia makubaliano ya kusafirisha mafuta

Nchi ya Belarus inatangaza kuwa imefikia makubaliano na taifa la Urusi ili kumaliza mvutano uliosababisha kusitishwa kwa usafirishaji wa mafuta hadi Ulaya.Rais wa Belarus Aleksander Lukashenko amekuwa akijadiliana na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin wakiwa na lengo la kumaliza tatizo hilo.Kulingana na Rais Lukashenko makubaliano yamefikiwa ili kuanzisha tena kusafirisha mafuta machafu kutoka Urusi kupitia bomba la Druzhba.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi kutoka afisi ya kiongozi huyo mawaziri wakuu wa pande zote mbili wameagizwa kukamilisha mapendekezo yatakayowasilishwa kwa viongozi hao ili kumaliza mvutano huo ifikapo Ijumaa.Mpaka sasa Urusi haijatoa kauli yoyote kuhusu swala hilo.

Kulingana na wadadisi huenda taifa la Urusi lina tashwishi na lile la Belarus na kuwa pengine Rais Lukashenko alichukua hatua hiyo ili kufurahisha mataifa ya magharibi wakati inashinikiza Urusi kuridhia.

Wakati huohuo Tume ya Umoja wa Ulaya imetangaza maelezo zaidi kuhusu sera yake mpya ya nishati kwa bara la Ulaya.Katika mkutano mjini Brussels,maafisa wa ngazi za juu wameonya kuwa makampuni ya gesi na nishati huenda yakachukuliwa hatua za kisheria endapo zitakiuka sheria za biashara.

Kwa mujibu wa Kamishna anayehusika na mashindano ya kibiashara Neelie Kroes,uzembe,bei za juu vilevile hatua ya baadhi ya kampuni kutaka kutawala soko la wanunuzi vimesababisha matatizo huku makampuni mampya yakizuiwa kufanya biashara.

Mwishoni mwa mwaka jana tume hiyo ilifanya ukaguzi wa ghafla katika baadhi ya makampuni ikiwemo E:ON ya Ujerumani na RWE zilizoshukiwa kukiuka sheria hizo za mashindano ya biashara.

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com