Mazungumzo ya Zimbabwe ; makubaliano hayajafikiwa. | Matukio ya Kisiasa | DW | 18.08.2008
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mazungumzo ya Zimbabwe ; makubaliano hayajafikiwa.

Viongozi wa mataifa ya kusini mwa Afrika wameshindwa kuvisukuma vyama vinavyopingana nchini Zimbabwe kufikia makubaliano.

Rais wa Afrika kusini Thabo Mbeki na rais wa Zimbabwe Robert Mugabe wakati rais huyo wa Afrika kusini akiwasili mjini Harare kwa mazungumzo ya upatanishi.

Rais wa Afrika kusini Thabo Mbeki na rais wa Zimbabwe Robert Mugabe wakati rais huyo wa Afrika kusini akiwasili mjini Harare kwa mazungumzo ya upatanishi.

Viongozi wa mataifa ya kusini mwa Afrika waliokusanyika kwa mkutano wa mwishoni mwa juma wameshindwa kuvisukuma , chama tawala nchini Zimbabwe pamoja na upande wa upinzani kufikia makubaliano ya kugawana madaraka , hatua ambayo inaweza kumaliza mzozo wa kisiasa wa baada ya uchaguzi nchini humo. Lakini wananchi wa nchi hiyo wako gizani juu ya kile kinachoendelea katika mazungumzo hayo.

Hali ya kutaka tamaa imetanda mitaani wakati mazungumzo hayo yanayoendelea huenda yakawa na maana ya kuwa na wakati mgumu huko mbeleni wakati uchumi wa nchi hiyo unaendelea kuporomoka.

Kwa Wazimbabwe wa kawaida , mazungumzo hayo kati ya makundi ya chama cha Movement for Democratic Change MDC, na chama tawala cha Zimbabwe African National Union – Patriotic Front, ZANU-PF ni matumaini pekee kwa ajili ya mwanzo mpya baada ya chaguzi mbili zilizokuwa na utata March na Juni mwaka huu.

Wiki kadha baada ya kutiwa saini rasimu ya maelewano ambayo inaweka wazi masharti kwa ajili ya mazungumzo, makubaliano ya kugawana madaraka bado ni kitendawili.

Mazungumzo yaliahirishwa August 12 baada ya siku tatu za mazungumzo ya ana kwa ana kati ya viongozi wa vyama hivyo vitatu kushindwa kufikia makubaliano yoyote ya maana, kikwazo kikubwa kikiaminika kuwa ni nani kati ya kiongozi wa ZANU-PF Robert Mugabe ama hasimu wake kutoka chama cha MDC, Morgan Tsvangirai , atashika madaraka makubwa katika serikali hiyo mpya ya mpito.

Tsvangirai , Mugabe na Arthur Mutambara , ambaye anaongoza kundi dogo la MDC wote walikuwapo katika mkutano wa SADC mjini Johannesburg. Na katibu mkuu wa chama hicho cha upinzani cha MDC amesema jana kuwa chama hicho kinaamini kuwa mazungumzo na chama tawala cha ZANU-PF yatakamilishwa hivi karibuni na kushindwa si suala linalotarajiwa.

Uchumi wa Zimbabwe umekuwa ukiporomoka kwa kasi, huku bei za bidhaa muhimu zikiongezeka kwa zaidi ya mara tano katika muda wa siku chache zilizopita.

Mwalimu wa shule Timothy Xaba mwenye umri wa miaka 42 amekuwa akiangalia nchi hiyo bila ya uwezo wa kufanya lolote ikitumbukia zaidi katika shimo. Ughali wa maisha ukinyofoa zaidi pato lake dogo, anahisi mazungumzo hayo yasiyokuwa na mwisho yanaishara mbaya kwa taifa hilo.

Tumesubiri kwa muda mrefu kuweza kuondoka katika giza la hali hii ya uchumi. Lakini wakati mazungumzo haya yanaburuza miguu, ina weza tu kuwa na maana kwamba hali mbaya inakuja, amesema Xaba, akiakisi mawazo ya watu wengi nchini Zimbabwe ambao wanaishi kwa pato la kiasi cha chini ya dola moja ya Marekani kwa siku.

Kwenda kazini limekuwa suala la kupoteza wakati, wakati hatufahamu chochote juu ya kile wanasiasa wanachozungumza ama iwapo mazungumzo haya yanaweza kuleta hali bora katika maisha yetu, amesema Xaba ambaye amekuwa akifundisha kwa zaidi ya miaka 20.

Afisa mmoja wa chama cha MDC amesema kuwa juhudi za upatanishi zitaendelea leo Jumatatu na Tsvangirai ataanza ziara ya kieneo katika hatua ya kupata ushauri kutoka kwa viongozi wa mataifa ya kusini mwa Afrika. Viongozi wa mataifa hayo walitarajia kuwa pande hizo zitapata makubaliano katika mkutano huo na kuanza juhudi za kuujenga uchumi ulioharibika nchini Zimbabwe.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com