Mataifa ya Euro yaipatia Ureno bilioni 78 | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.05.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mataifa ya Euro yaipatia Ureno bilioni 78

Mawaziri wa fedha wa mataifa ya umoja wa sarafu ya Euro wameidhinisha mkopo wa euro bilioni 78 kwa Ureno jana katika mkutano wao mjini Brussels.

default

Wazitri wa fedha wa Hispania Elena Salgado,kushoto akizungumza na waziri wa fedha wa Italia Giulio Tremonti, kati ,pamoja na waziri wa fedha kutoka Sweden Anders Borg.

Jioni ya jana Jumatatu mawaziri wa fedha wa mataifa ya eneo la Euro wanaokutana mjini Brussels, kwa kauli moja waliidhinisha mpango wa umoja wa Ulaya na shirika la fedha la kimataifa IMF wa kuiokoa Ureno wenye thamani ya euro bilioni 78. Baada ya Ireland na Ugiriki, Ureno ni nchi ya tatu kupewa mkopo huo. Hali nchini Ugiriki hata hivyo wamesema mawaziri hao wa fedha kuwa ni ngumu, na hakuna uwezekano wa kupatiwa mkopo wa ziada.

Licha vyama kadha kukabiliwa na uchaguzi mwezi wa Juni, wameweza kukamilisha mpango mgumu wa kubana matumizi kwa ajili ya Ureno, na kutimiza ahadi yao ya kulisaidia taifa hilo ambalo limetumbukia katika madeni makubwa. Jean-Claude Junker, msemaji wa mataifa 17 wanachama wa umoja wa sarafu ya Euro anasema.

"Tumefikia makubaliano, kwamba Ureno itasaidiwa katika muda wa miaka mitatu ijayo. Mpango huo unajumuisha kiasi cha euro bilioni 78."

Jean Claude Junker Premierminister Luxemburg

Waziri mkuu wa Luxembourg Jean-Claude Junker

Fedha hizo zitatoka katika mataifa ya umoja wa sarafu ya euro, pamoja na shirika la fedha la kimataifa IMF. Kwa kuiokoa Ureno eneo lote la mataifa yanayotumia sarafu ya euro litaimarika, anasema kamishna wa umoja wa Ulaya anayeshughulika na uchumi na fedha Olli Rehn kupitia ushauri. Shirika la fedha la kimataifa IMF, liliwakilishwa na mwakilishi wa mkuu wa shirika hilo ambaye anakabiliwa na mashtaka ya matumizi ya nguvu dhidi ya mfanyakazi wa kike wa hoteli moja mjini New York, Dominique Strauss-Kahn.

Kiongozi wa Luxemburg Jean Claude Junker , anasema amesikitika sana alipoona uso wa rafiki yake Strauss-Kahn katika televisheni.

"Sikupenda picha niiyoiona katika televisheni. Ilikuwa inasikitisha sana. Strauss Kahn hivi sasa yuko mikononi mwa mahakama za Marekani. Sikupenda kuzungumzia lolote kuhusu hilo, lakini inanifanya nijisikie mwenye masikitiko."

Hali nchini Ugiriki, ambayo katika mwaka mmoja uliopita umoja wa Ulaya na shirika la fedha ulimwenguni IMF, zimekuwa zikiishughulikia, hali inabaki kuwa mbaya na ngumu, anasema mwenyekiti wa kundi hilo la mataifa ya euro, Jean Claude Junker. Serikali ya Ugiriki inapaswa kubana matumizi zaidi kuliko hivi sasa. Vyama vya kisiasa nchini Ugiriki vinapaswa kujiweka pamoja na kuunga mkono kwa pamoja mpango huo wa kubana matumizi, anasema kamishna wa masuala ya uchumi na fedha wa umoja wa Ulaya, Olli Rehn.

Olli Rehn

Kamishna wa umoja wa Ulaya anayeshughulikia masuala ya uchumi na fedha Olli Rehn

"Kuna nafasi ya utekelezaji, hususan katika suala la bajeti pamoja na ubinafsishaji wa mali za taifa. Ugiriki inalazimika kuongeza kasi ya kurekebisha bajeti ya taifa. Mpango wa ubinafsishaji wenye thamani ya euro bilioni 50 unapaswa kuimarishwa bila kucheleweshwa."

Kupatiwa Ugiriki mkopo wa ziada ili kulipia deni la taifa kwa gharama ya taifa na wakopeshaji wa binafsi hilo limekataliwa, amesema mkuu huyo wa kundi la mataifa ya euro Jean Claude Junker.

"Suala la deni kubwa zaidi halipo katika mada. Hakuna aliyelizungumzia hilo leo. Mpango mwingine hata hivyo haujafutwa kabisa. Lakini kwanza ni suala la hatua kadha, ambazo serikali ya Ugiriki inapaswa kuzitekeleza. Na mwishoni kabisa, inawezekana kufikiria kuhusu mabadiliko katika mfumo wa deni."

Katika mkutano huo wa mawaziri wa fedha wa eneo la euro, hata hivyo hakukuwa na cha kushangaza baada ya kuidhinisha pia jina la mkuu wa benki ya Italia Mario Draghi kuwa mgombea wa wadhifa wa mkuu wa benki kuu ya umoja huo. Rais wa sasa wa benki hiyo Jean-Claude Trichet anamaliza muda wake mwezi Novemba mwaka huu. Draghi anatarajiwa kuchaguliwa katika wadhifa huo na viongozi wa serikali na taifa wa umoja huo mwezi Juni.

Mwandishi : Bernd Riegert / ZR / Sekione Kitojo

Mhariri: Josephat Charo

 • Tarehe 17.05.2011
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/11Hb1
 • Tarehe 17.05.2011
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/11Hb1

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com