Mashambulizi dhidi ya Gaddafi kuwezekana kama Marekani itajihusisha tena kikamilifu | Matukio ya Kisiasa | DW | 14.04.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mashambulizi dhidi ya Gaddafi kuwezekana kama Marekani itajihusisha tena kikamilifu

Wakati mzozo wa Libya ukiendelea, wachambuzi wanasema hatua ya Marekani kujiingiza tena kikamilifu katika operesheni za kijeshi Libya inaweza kusaidia kuondoa mkwamo uliopo kati ya waasi na Kanali Muammar Gaddafi.

default

Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa, Gerard Longuet

Lakini Marekani inaonekana kusita kujihusisha kikamilifu katika mzozo huo ambao tayari umegeuka kuwa vita. Mapema, Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa, Gerard Longuet alisema mashambulizi yanayofanywa na Kanali Gaddafi hayatomalizika iwapo Marekani haitajihusisha kikamilifu katika operesheni za kijeshi nchini Libya, operesheni ambazo zinaonekana kusita baada ya Jumuiya ya Kujihami ya NATO kuchukua jukumu hilo tangu Machi 31 mwaka huu.

Huku ikisema hadharani kwamba ndege za kivita zipo iwapo zitahitajika, Marekani imekuwa ikisita kujiingiza katika mzozo mwingine kwenye ulimwengu wa mataifa ya Kiarabu. Wachambuzi wanasema kuwa suala la kutoa mafunzo ya kijeshi na kuwapatia waasi silaha huenda likawa linaendelea, lakini litabidi kuimarishwa na kuwepo mashambulizi zaidi ya anga ya Marekani ili kuepuka mkwamo wa muda mrefu ambao utaonekana kama kushindwa kwa operesheni za NATO.

Deutschland NATO Außenminister in Berlin Generalsekretär Anders Fogh Rasmussen

Katibu Mkuu wa NATO Anders Fogh Rasmussen

Juzi Jumatano, wizara ya ulinzi ya Marekani ilisema kuwa ndege zake za kivita zimeendelea kuvishambulia vikosi vya Kanali Gaddafi baada ya NATO kuchukua rasmi jukumu la operesheni hizo. Mchambuzi mmoja wa masuala ya kisiasa, Marko Papic anasema kukosekana kwa mashambulizi ya anga ya karibu pamoja na ujuzi mdogo wa kijeshi walionao waasi ndivyo vitu vikubwa vinavyokwamisha operesheni za NATO.

Hata hivyo, wachambuzi wana hofu iwapo Marekani itakuwa tayari kuchukua tena jukumu kamili la kuongoza operesheni za kijeshi nchini Libya. Barak Seener wa Taasisi moja ya London anasema kuwa Marekani itaendelea kutoa msaada wa kijasusi, lakini utawala wa Rais Barack Obama hautaki kuwa kiini cha mizozo mipya ya kigeni wakati ambapo inatafuta kuachana na mikakati iliyorithi kutoka kwa wengine.

Karl-Heinz Kamp wa Chuo cha mafunzo ya kijeshi cha NATO, anasema kuwa Libya kwa mara nyingine imeonyesha mapungufu ya kijeshi ya vikosi vya muungano. Anasema kwa sasa wako katika hali ambayo wote wana wasiwasi kuhusu aina ya mkwamo ambao waasi peke yao hawawezi kuutatua na utawala wa Kanali Gaddafi haudondoki. Kamp anasema vifaru chapa A-10 ndiyo madhubuti kutumika katika operesheni kama hiyo ya kushambulia vifaru vinavyozuia mitaa, lakini Marekani imekuwa ikisita.

Kamp anasema ili kumaliza mkwamo huo patahitajika kuongeza zaidi mashambulizi ya anga au ardhini, lakini nchi washirika wa NATO kama vile Uturuki, ambayo awali ilipinga uvamizi wa kijeshi nchini Libya, inapinga suala la kuongeza operesheni hizo za NATO. Hakuna nchi yoyote, ikiwemo Uingereza na Ufaransa ziko tayari kuendesha operesheni za mashambulizi ya ardhini, isipokuwa labda kwa vikosi maalum vya jeshi, ambavyo uwepo wake utakataliwa.

Karl Heinz Kamp KAS Leiter AG Außenpolitik

Karl Heinz Kamp wa chuo cha mafunzo ya kijeshi cha NATO

Barak Seener anabainisha kuwa washirika wa NATO wamesaidia kuanza kwa mkwamo huo kwa kulitafsiri azimio la Umoja wa Mataifa kama lenye kudhibiti malengo yao dhidi ya vikosi vya Kanali Gaddafi ambavyo vinawatishia raia. Wakati nchi wanachama 28 wa NATO wakiwa bado wamegawanyika kuhusu kuwapatia silaha na mafunzo waasi, hatua hiyo huenda isiwe kikwazo kwa nchi moja moja za Magharibi na mataifa ya Kiarabu kufanya hivyo.

Wachambuzi hao wanasema hatua ya mwisho ya NATO itakuwa kutangaza mamlaka yake ya operesheni za Umoja wa Mataifa ya kuwalinda raia kama yenye ushindi iwapo vikosi vya Kanali Gaddafi vitaacha mashambulizi na kumaliza operesheni zake. Lakini Kamp anasema ni lazima kuwa na nguvu na uwezo ili kubakia Libya, kwani walidhani Kanali Gaddafi angeondoka madarakani haraka, ambapo hilo lingekuwa jambo zuri, lakini suala ni kusubiri na kuona kwa wiki moja au mbili zijazo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (RTRE)
Mhariri:Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com