Marekani yasifu operesheni yake nchini Iran
6 Machi 2026
Kamanda mkuu wa Jeshi la Marekani Brad Cooper, amesema mashambulizi ya Iran iwe ya makombora ya masafa marefu au droni yamepungua maradufu ukilinganisha na siku ya kwanza ya mzozo huo wa Mashariki ya Kati , lakini akasisitiza kuwa wataendelea kuwa makini wakati wote.
Ama Rais wa Marekani Donald Trump kwa upande wake amesifu ufanisi wa operesheni hiyo akisema kuwa jeshi la Marekani, pamoja na washirika wazuri wa Israel, linaendelea kumuangamiza kabisa adui ambaye ni Iran, hata kabla ya muda uliopangwa.
" Pia tunawasihi wanadiplomasia wa Iran kote ulimwenguni kuomba hifadhi na kutusaidia kuijenga Iran mpya, iliyo bora na yenye uwezo mkubwa. Nadhani sasa unaanza mustakabali mzuri zaidi kwa Iran. Na Marekani itahakikisha kwamba kiongozi ajaye wa Iran hatatishia Marekani, Israel, majirani zake au mtu yeyote," alisisitiza Trump.
Aidha, licha ya mashambulizi ya Israel na Marekani kuendelea, umati mkubwa wa raia wa Iran ulikusanyika katikati mwa mji mkuu Tehran na katika maeneo mengine kwa ajili ya sala ya kwanza ya Ijumaa tangu kuanza kwa vita hivyo.
Picha zilizosambazwa mtandaoni na vyombo vya habari vya Iran zimeonyesha umati wa watu waliovalia nguo nyeusi huku baadhi wakiwa wamebeba bendera za Iran, wakimiminika nje ya Msikiti Mkuu wa Imam Khomeini mjini Tehran kwa ajili ya sala ya Ijumaa ambayo pia ni ya kwanza tangu kuuawa kwa kiongozi mkuu wa nchi hiyo Ayatollah Ali Khamenei kufuatia mashambulizi ya Marekani na Israel ambayo yameendelea kwa kasi katika siku hii ya saba ya mzozo huo.
Iran yaendelea kuvurumisha makombora na droni
Iran nayo imeendelea kuishambulia Israel na mataifa jirani ya Ghuba ambako kunapatikana kambi na wanajeshi wa Marekani. Qatar imesema hivi leo kuwa vikosi vyake vya majini havikujeruhiwa licha ya kuwepo ndani ya majengo ya makazi na hoteli yaliyolengwa na Iran huko Bahrain huku Saudi Arabia ikitangaza kudungua droni kadhaa karibu na mji wa Riyadh.
Katika tukio jingine, Umoja wa Mataifa umeitaka Marekani kuchunguza haraka tukio la shambulizi katika shule nchini Iran ambapo uchunguzi wa gazeti la New York Times unasema huenda shambulio hilo lililosababisha vifo vya wanafunzi zaidi ya 150 lilifanywa na Marekani.
Israel imeendeleza pia mashambulizi yake nchini Lebanon ikidai yanalenga kulidhoofisha kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran. Lakini Umoja wa Mataifa umehimiza hivi leo kufanyike uchunguzi wa haraka kuhusu mashambulizi mabaya ya Israel nchini Lebanon, ili kubaini ikiwa yanafanyika kulingana na sheria za kimataifa.
Aidha, Shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa limesema hivi leo kuwa karibu watu 100,000 wameyakimbia makazi yao ndani ya Lebanon ikiwa ni pamoja na maelfu ya wakimbizi wa Syria. Msemaji wa UNHCR Ravina Shamdasani ameielezea hali katika eneo hilo kuwa dharura kubwa ya kibinadamu na kwamba raia ndio wanaolipia gharama kubwa.