Marekani kuendelea na uchunguzi dhidi ya Urusi | Matukio ya Kisiasa | DW | 15.02.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Marekani kuendelea na uchunguzi dhidi ya Urusi

Mashirika ya kijasusi ya Marekani  pamoja na bunge la nchi hiyo yataendelea kufanya uchunguzi kuhusiana na madai ya Urusi kujihusisha katika uchaguzi wa Marekani  mwaka jana.

Wademocrats wanasema  uchunguzi huru ndio njia nzuri ya kujibu maswali yanayohusiana na mahusiano yaliyopo kati ya utawala wa Trump na Urusi lakini hata hivyo chama cha Republican  kinaendelea kuipinga hoja hiyo na kusema kuwa uchunguzi unaoendelea hadi sasa juu ya madai hayo  unatosha.

Mshauri wa usalama wa taifa  Rais Donald Trump alifutwa kazi jumatatu wiki hii kutokana na kile kilichoelezwa na ikulu ya White House kuwa alimpotosha makamu wa Rais Mike Pence kuhusiana na mawasiliano yake na  na balozi wa Urusi. Msemaji wa ikulu ya Marekani Sean Spicer alisema Rais Donald Trump alifahamishwa mwishoni mwa Januari  kuwa Flynn alikuwana  na majadiliano na balozi wa Urusi kuhusiana na suala la vikwazo dhidi ya Urusi lakini makamu wa Rais Mike Pence hakuwa na ufahamu wa taarifa hizo na hivyo kumtetea afisa huyo katika mahojiano yaliyofanywa kwa njia ya televisheni.

Hii si mara ya kwanza Rais Donald Trump kujiweka kando na mshauri wake kuhusina na suala linalohusina na Urusi. Mwishoni mwa August mwaka jana Paul Manafort alilazimika kujiuzulu kama meneja wa kampeni ya Trump baada ya shirika la habari la Asociated Press kufichua kwamba alikuwa akihusika katika kuifanyia kmpeni kwa siri chama tawala cha zamani cha Ukraine kilichokuwa kikiunga mkono Urusi.

Trump akiri urusi kufanya udukuzi wa barua pepe za Democrats

USA Donald Trump und Michael Flynn in Palm Beach (Reuters/C. Barria)

Rais Donald Trump akiwa pamoja na aliyekuwa mshauri wa usalama Michael Flynn

Katika utawala wa Rais Barack Obama mashirika ya kijasusi ya Marekani yalisema Urusi iliingilia uchaguzi wa mwaka 2016 ikiwa na lengo la kumuwezesha Donald Trump kushinda uchaguzi huo.  Trump alikiri Urusi kufanya udukuzi wa barua pepe  za chama cha Democrats  lakini alikanusha hatua hiyo kuwa ilikuwa na lengo la kumuwezesha kushinda uchaguzi huo.

Gazeti la New York Times liliripoti hapo jana kuwa baadhi ya maafisa katika serikali ya Rais Donald Trump ikiwa ni pamoja na Paul Manafort  walikuwa na mawasiliano ya mara kwa mara na maafisa wa kijasusi wa urusi  kabla ya kufanyika uchaguzi wa mwaka jana ambayo Marekani ilifanikiwa kuyanasa kutokana na kufuatilia mawasiliano hayo yaliyofanywa kwa njia ya simu.

Hata hivyo Manafort alilieleza shirika la habari la Associated Press kuwa alikuwa bado hajahojiwa na Idara ya  upelelezi - FBI juu ya madai hayo na kusisitiza kuwa hajawahi kufanya mazungumzo na maafisa wa kijasusi wa Urusi wala  kujihusisha  kwa njia yoyote ile na utawala wa Rais Putin au suala lolote linalofanyiwa uchunguzi hivi sasa.

Maafisa waliozungumza na gazeti la Times kwa sharti la kutotajwa majina wanasema hawajabaini ushahidi wowote unaohusiana na madai ya timu ya kampeni ya Trump kushirikiana na Urusi katika kufanya udukuzi au kujihusisha kwa namna yoyote katika kushawishi matokeo ya uchaguzi wa mwaka jana.

Uchunguzi unaoendelea na hatua ya kufutwa kazi kwa mshauri wa masuala ya usalama w ikiwa ni siku 24 tangu aanze rasmi majukumu yake yamekiweka chama cha Republican katika hali tete yanayolazimu kuchunguzwa kiongozi wa chama hicho.

Mwandishi: Isaac Gamba/ APE/ EAP

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com