Marekani, Iran zarudi mezani Qatar baada ya 'kutoana ngeu'
29 Juni 2026
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, wapatanishi walifanikiwa kuanzisha njia za mawasiliano kwa lengo la kupunguza makali ya tukio lolote linaloweza kuyachafua majadiliano na kwamba siku ya Jumanne (Juni 30) wajumbe wa timu za wataalamu wangelikutana mjini Doha kuendelea na mazungumzo ya wataalamu.
"Pande hizi mbili zitasitisha makabiliano kwa sasa na meli zinaweza kupita kwenye Mlango Bahari wa Hormuz kwa uhuru, wakati huu mazungumzo ya kitaalamu yakipangwa kufanyika Doha." Alisema mmoja wa maafisa wa Marekani.
Awali, mazungumzo hayo yalikuwa yamepangwa kufanyika tena nchini Uswisi yakiwa yamejikita tu kwenye mpango ya nyuklia wa Iran, lakini wasiwasi mpya uliozuka kutokana na Marekani na Iran kushambuliana wiki iliyopita, umepelekea mazungumzo hayo kuhamishiwa Doha na mada kubadilishwa na kuwa sasa hatima ya Mlango Bahari wa Hormuz.
Iran yashikilia msimamo wake
Akiwa nchini Iraq siku ya Jumapili (Juni 28), Waziri wa Mambo wa Kigeni wa Iran, Abbas Araghchi, aliwaambia waandishi wa habari kwamba "hakuna kilichobadilika kwenye msimamo" wa nchi yake kuhusiana na Mlango Bahari wa Hormuz na masharti yaliyomo kwenye Makubaliano ya Awali.
"Tehran ndiyo pekee yenye haki ya kuamua na kusimamia shughuli zote za usafirishaji kupitia Mlango Bahari wa Hormuz," alisema Araghchi.
Kwa upande mwengine, Iran inasema ilikuwa na mkutano wake wa mwanzo na Oman juu ya usimamizi wa Mlango Bahari huo muhimu sana kwa usalama wa nishati ulimwenguni kufuatia Makubaliano ya Awali kati yake na Marekani.
"Wakati wa ziara yetu ya Muscat, mkutano wa kwanza wa Kamati ya Pamoja ya Hormuz. Ambapo tunaendelea kuyahakiki matukio ya sasa kuhusiana na Mlango huo, tulibadilishana maoni juu ya mustakabali wa usimamizi wake." Aliandika kupitia mtandao wa X, Naibu Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran, Kazem Gharibabadi, siku ya Jumatatu (Juni 29).
Fedha za Iran kurejeshwa?
Wakati wa mazungumzo ya Uswisi wiki moja iliyopita, ujumbe wa Marekani ulikubaliana na Iran kuanzisha chaneli ya "mawasiliano ya moja kwa moja" kati ya majeshi yao ili kuratibu safari za meli kupitia Hormuz. Lakini hadi kufikia Jumamosi, hakukuwa na chaneli hiyo iliyoanzishwa.
Marekani iliishambulia Iran siku ya Ijumaa na Jumamosi (Juni 26 na 27), ikidai Tehran ilikuwa inaendelea kuzizuwia meli za kibiashara, nayo Iran ikayashambulia maeneo manane ya Marekani ndani ya mataifa ya Ghuba kujibu mashambulizi hayo.
Hayo yakijiri, Rais Masoud Pezeshkian wa Iran alisema siku ya Jumatatu kwamba dola bilioni sita za nchi yake zilizozuiliwa zitaachiliwa na Qatar, akitafautiana na msimamo wa maafisa wa Marekani wanaokanusha kutolewa kwa fedha hizo.
Shirika la habari la Iran, IRNA, limemnukuu kiongozi huyo akisema: "kwa mujibu wa mipango iliyowekwa, dola bilioni sita kati bilioni 12 zinazoshikiliwa nchini Qatar kwa amri ya Marekani zitarejeshwa Iran na kwamba hatua muhimu za ufuatiliaji zinaendelea hivi sasa."