Mapambano mapya dhidi ya marufuku ya Trump | Matukio ya Kisiasa | DW | 08.03.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mapambano mapya dhidi ya marufuku ya Trump

Wanasheria wa majimbo na makundi ya haki za kiraia wanajipanga kufungua shauri kuipinga marufuku mpya ya rais Donald Trump dhidi ya wahamiaji kutoka mataifa sita yenye Waislamu wengi. Lakini watafanikiwa safari hii?

Ikulu wa White House imezindua mchakato mpya unaonuwia kuepusha kurudiwa kwa mkangnyiko uliosababishwa na marufu yake ya kwanza ya kusafiri, iliotangazwa kwa kustukiza na ikiwa na maandalizi kidogo sana wiki moja tu baada ya Trump kuingia madarakani. Safari hii hakutarajiwi kuwepo na vurugu kama zilizoshuhudiwa katika viwanja vya ndege na uzuwiaji wa watu, kuwasaidia mawakili kujenga hoja kwamba haki za watu zinakiukwa.

Amri mpya iliotolewa siku ya Jumatatu inazuwia wakimbizi wote kuingia nchini Marekani kwa siku 120, na inasitisha utoaji wa viza mpya kwa raia wa Syria, Libya, Somalia, Yemen na Sudan kwa siku 90. Ingawa marufuku  hii inafanana na ile ya kwanza, imefanyiwa mabadiliko kwa namna inayoiwezesha kuvuka vihunzi vya mahakani. Kwanza kabisaa marufuku hiyo mpya haitatekelezwa hadi Machi 16, na hivyo kuwapa wasafiri muda wa siku 10 kujiandaa na mabadiliko hayo.

USA Doug Chin (picture-alliance/AP Photo/A. McAvoy)

KAtika picha hii ya Februari 3, mwansheria mkuu wa Hawaii Doung Chin akizungumza katika mkutano na waandishi habari mjini Honolulu kutangaza kuwa jimbo la Hawaii limefungua shauri kupinga marufuku mpya ya Trump.

Muhimu zaidi, amri hiyo mpya haiwahusishi walio na vibali vya ukaazi wa kudumu wa Marekani pamoja na wale walio tayari na viza, na inaweka fursa ya kupatiwa viza kwa raia wa mataifa yaliopigwa marufuku katika mazingira makhsusi. Pia imeiondoa Iraq kwenye orodha hiyo. Mkakati huo unaonekana umesanifiwa kushughulia hali iliosababisha hasira na kuifanya marufuku ya kwanza kuwa bomu la kisiasa.

Mabadiliko katika sheria mpya

Miongoni mwa visa maarufu ni cha mtoto mchanga wa Kiirani ambaye alishindwa kwenda Marekani kwa ajili ya kupatiwa matibabu makhsusi. Hilo linaweza kushughulikiwa kwa kupitia mpango wa msamaha wa viza. Wanafunzi wa kigeni na watendaji wa Bonde la Silicon walikwama pia nje, na familia nzima zilizuwiwa katika uwanja wa ndege. Lakini maadamu wana viza chini ya sheria mpya, hawatakabiliwa tena na hatari hiyo.

Wanasheria wa jimbo la Hawaii siku ya Jumanne waliiambia mahakama ya wilaya kuhusu mpango wao wa kufungua shauri la kipingamizi dhidi ya marufuku hiyo iliorekebishwa siku ya Jumatano, ambalo yumkini litakuwa mtihani wa kwanza wa kisheria kwa mari hiyo. Jimbo hilo limeomba shauri lake lisikilizwe kwa haraka ili kuzingatia kuizuwia kwa muda marufuku hiyo.

Ikiwa majaji watakubali, "hii itairuhusu mahakama kusikiliza shauri la jimbo hilo kabla ya kuanza kutekelezwa kwa marufuku hiyo Machi 16," alisema mwanasheria mkuu wa Hawaii katika taarifa. Jaji wa shirikisho aliezuwia marufuku ya kwanza katika jimbo la Washington mwezi uliopita, alishwawishiwa na na hoja ya wanasheria wakuu wawili wa majimbo kwamba ilikuwa inasababisha "madhara makubwa." Haijabainika wazi iwapo hoja kama hizo zitakuwa na mashiko safari hii.

USA Keith Ellison (Getty Images/A. Wong)

Mbunge Muislamu pekee katika bunge la Marekani Keith Ellison akizungumzia marufuku ya Trump mjini Washington.

"Tunaipita kwa umakini marufuku hii mpya kuangalia athari zake kwa jimbo la Washington na hatua zetu zinazofuata kisheria," Mwanasheria mkuu wa jimbo la Washington Bob Ferguson alisema siku ya Jumatatu. Alisema bado alikuwa anatiwa na wasiwasi lakini alihitaji siku mbili au tatu kuamua hatua zinazofuata.

Marufuku ya siri dhidi ya Waislamu

Camille Mackler, mkurugenzi wa mpango wa kisheria katika Muungano wa Uhamiaji mjini New York, aliitaja marufuku mpya ya Trump kuwa "marufuku ya siri dhidi ya Waislamu." "Bado tunadhani ina matatizo kama marufuku ya kwanza," alisema. "Haikutokea bila sababu, ilitokea katika muktadha wa matamshi yaliotolewa kabla na tangu kumalizika kw auchaguzi, vita hii pana dhidi ya wahamiaji ambayo utawala wa Trump unapigana."

Wimbi lingine la upinzani wa kisheria litakabiliana moja kwa moja na na swali la iwapo amri hiyo ya uhamiaji inaunda marufuku dhidi ya Waislamu, suala ambalo mpaka sasa mahakama zimeliweka kando. "Wakati ikulu ya White House inaweza kuwa imeifanyia mabadiliko marufuku hiyo, nia ya kuwabaguwa Waislamu inaendelea kuwepo," alisema mwanasheria mkuu wa New York Eric Schneiderman.

Utawala umefanya iwe vigumu kuonyesha ubaguzi wa kidini kwa kuondoa lugha ambayo ingetoa kipaumbela kwa jamii za kidini za wachache pale wakimbizi watakaporuhusiwa tena. Wakosoaji walisema upendeleo unaowanufaisha Wakristo unaonyesha kuwa marufuku imelengwa kwa Waislamu. " Ninaamini marufuku mpya itahimili changamoto za kisheria kwa sababu imeandaliwa katika namna ambayo siyo marufuku ya kidini, lakini marufuku dhidi ya watu mmoja mmoja kutoka mataifa yalio na serikali hatarishi na mataifa yalioshindwa," alisema seneta wa chama cha Repblican Lindsey Graham.

USA Proteste gegen Trumps neues Einreiseverbot (Getty Images/AFP/S. Huffaker)

Maandamano yakifanyika nchini Marekani kupinga amri mpya ya kusafiri ya Trump.

Sera ni ile ile

Utawala wa Trump unayachakulia mataifa matatu kati ya yaliolengwa -- Iran, Sudan na Syria -- kama yanayofadhili ugaidi, na mengine matatu kama mahala salama kwa magaidi. Wakosoaji wake lakini wanahoji orodha hiyo, inayohusisha mataifa ambayo raia wake hawajawahi kuhusika na mashambulizi yoyote ya kigaidi nchini Marekani.

Na wanajengea hoja zao kwa matamshi ya zamani ya Trump wakati wa kampeni, alipoahidi kuwazuwia Waislamu kungia Marekani kama ushahidi juu ya uadui ambao itakuwa vigumu kuupuuza. "Nia dhahiri ni kuzishawishi mahakama kwamba marufuku hiyo ni matokeo ya maamuzi yaliofanyika kwa uangalifu mkubwa kuliko uadui wa kidini," alisema Elizabeth Goitein, mkurugenzi mwenza wa programu ya uhuru wa haki na usalama wa taifa ya kituo cha Brennan.

"Lakini mibinyo hii ya kimkakati katika toleo la sasa haiwezi kuokoa uhalali wa kikatiba wa amri hiyo," aliongeza. Nyuma ya matamshi yaliolainishwa na mabadiliko mengine ipo sera sawa ya sumu: juhudi za kuwazuwia Waislamu kuingia nchini Marekani."

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe

Mhariri. Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com