Maoni ya wahariri wa Ujerumani. | Magazetini | DW | 07.05.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Maoni ya wahariri wa Ujerumani.

Wahariri wa magazeti leo katika maoni yao wanazungumzia juu ya matokeo ya uchaguzi wa rais nchini Ufaransa ambapo mjumbe wa chama cha kihafidhina Nicolas Sarkozy ameshinda.

Katika maoni yao wahariri pia wanazungumzia juu ya lawama zilizotolewa dhidi ya rais wa Ujerumani bwana Horst Köhler kwa sababu ya kumtembelea jela alieyekuwa gaidi wa kundi la kigaidi linaloitwa Red Army Christian Klar.

Mhariri wa gazeti la NUEUE PRESSE kutoka mji wa Hanover anasema kwa kumchagua bwana Sarkozy wafaransa wameamua kuwa na mtu mwenye msimamo ngangari katika uongozi. Lakini, anaeleza mhariri wa gazeti hilo kuwa Ufaransa imegawanyika katika pande mbili.

Katika upande mmoja wapo wale waliomwuunga mkono bibi Segolene Royal , mpinzani wa bwana Sarkozy . Watu hao hasa, wanaoishi katika vitongoji vya walala hoi, wanamwona Sarkozy kuwa mwanasiasa mwenye msimamo mkali.


Lakini katika maoni yake mhariri wa gazeti la LEIPZIGER VOLKSZEITUNG anasema kuwa bwana Nicolas Sarkozy ni mtendaji kazi. Lakini pia anaeleza machache juu ya bibi Segolene Royal alieshindwa katika uchaguzi wa jana.

Mhariri huyo anasema kuwa mshindani wa bwana Sarkozy , bibi Royal hakufua dafu.

Mhariri anaeleza kwamba katika programu zao wajumbe hao wawili walikuwa mshabaha. Wote walizungumzia juu ya ajira kwa wwananchi wao , juu ya kupunguza deni la serikali , na wote walizungumzia juu ya kuleta mfumo wa elimu ya ufanisi. Lakini anasema tofauti ipo katika njia ya kutekeleza malengo hayo . Jee nani atabeba mzigo, ni serikali ama uchumi wa soko?

Bibi Royal hakufanikiwa kufikia shabaha yake japo alizungumzia juu ya kuleta haki za kijamii.

Gazeti linasema mjumbe huyo wa chama cha kisoshalisti alijenga taharuki miongoni mwa wastahiki kwa kusema kuwa Sarkozy atasababisha vurumai ndani ya nchi ikiwa ataingia ikulu ya Elysee.


Mhariri wa gazeti la MÄRKISCHE ALLGEMEINE anaeleza katika maoni yake kwamba uchaguzi wa jana ulikuwa juu ya mwelekeo mpya wa sera nchini Ufaransa na kuwa, alieshinda ni yule alietetea sera za mageuzi.

Amefafanua hayo kwa kusema kuwa bwana Sarkozy alisimama kidete katika kutetea sera za magezuzi nchini Ufaransa. Anachotaka Sarkozy ni agenda ya mwaka 2010,anasisitiza mhariri huyo katika maoni yake. Ushindi wake unaonesha kuwa wafaransa wanataka mageuzi .Lakini huenda akakabiliwa na vizingiti katika kutekeleza shabaha zake!

Mhariri anasema utekelezaji wa melengo yake utategemea matokeo ya uchaguzi wa bunge katika wiki sita zijazo.

Katika maoni yao wahariri leo pia wanazungumzia juu ya lawama zilizotolewa dhidi ya rais wa Ujerumani Horst Köhler kwa sababu ya kumtembelea aliekuwa gaidi wa kundi la Red Army RAF Christian Klar anaetumikia kifungo cha maisha kwa mauaji.

Rais Köhler anatarajiwa kutoa uamuzi wiki hii iwapo gaidi huyo atasamehewa.

Baadhi ya wanasiasa wamekuja juu ,juu ya mkutano wa rais Köhler na gaidi huyo. Baadhi yao kutoka vyama vya CDU na CSU wametishia kumyima kura rais huyo itakapofikia siku ya kurefusha wadhifa wake.

Juu ya hayo Mhariri wa gazeti linaloitwa Centi 20 anasema wanasiasa hao hawana haya. Anawakumbusha kuwa rais huyo ana uhuru wa kutoa msamaha bila ya kuingiliwa na mtu yeyote.

Lakini mhariri wa gazeti la SÜDKURIER anaunga mkono lawama zilizotolewa na wanasiasa. Anasema ziara hiyo imemnufaisha gaidi huyo ambae hadi leo hajaonesha masikikito yoyote juu ya matendo yake.