Maoni ya wahariri juu ya ziara ya Kansela Merkel barani Afrika. | Magazetini | DW | 13.07.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Maoni ya wahariri juu ya ziara ya Kansela Merkel barani Afrika.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel anaendelea na ziara ya barani Afrika. Wahariri wanatoa maoni yao juu ya ziara hiyo.

default

Kansela Angela Merkel na Rais Jose dos Santos wa Angola

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanazungumzia juu ya ziara ya Kansela Merkel barani Afrika,mgogoro wa madeni barani Ulaya na juu ya mtamauko wa watu wa Misri baada ya mapinduzi kufanyika.

Kuhusu ziara ya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel barani Afrika gazeti la Märkische Oderzeitung linasema ,bibi Merkel anaifanya ziara hiyo muda mfupi tu baada ya Ujerumani kuipitisha sera mpya juu ya Afrika inayosisitiza ushirikiano na maslahi ya kiuchumi. Lakini mhariri wa gazeti hilo anasema ziara hiyo ni fursa kwa bibi Merkel ya kuyazungumzia masuala mengine vile vile .


Gazeti la Münchner Merkur linasema mashindano ya malighafi barani Afrika yanaambatana na hatari ya kulinyonya bara la Afrika kwa mara ya pili. Lakini njia ya kuepusha hayo ni kuendeleza biashara ya haki .

Gazeti la Nürnberger Nachrichten pia linazungumzia juu ya ziara ya Kansela Merkel barani Afrika kwa kutilia maanani baa la njaa kwenye pembe ya Afrika. Mhariri huyo anaeleza kuwa Kansela Merkel ameahidi msaada wa Euro milioni moja ili kuziunga mkono juhudi za kupambana na baa la njaa barani Afrika. Hatua hiyo inastahili kusifiwa lakini kiasi hicho cha fedha ni sawa na kujaribu kuikausha bahari kwa kutumia ndoo moja! Mhariri huyo anasema kinachotakiwa ni mkakati wa kupambana na mambo yanayosababisha njaa.

Gazeti la Heibronner Stimme pia linazungumzia juu ya baa la njaa barani Afrika, wakati Kansela Merkel anafanya ziara katika bara hilo, na linasema mambo yanayosababisha njaa barani Afrika,ni pamoja na hali mbaya ya hewa na migogoro ya kivita. Lakini viongozi wa Afrika pia wanayo hatia. Lingekuwa jukumu la viongozi hao kuepusha picha kama zile zinazoonekana kwenye kambi ya Dadaab. Kambi hiyo ni aibu kwa serikali inayotambua wajibu wake!

Mgogoro wa madeni bado unaendelea barani Ulaya na gazeti la Neue Presse linasema pana haja ya kutafuta njia za kuziepusha nchi kutumbukia katika madeni. Gazeti hilo linaeleza kwamba wakati juhudi zinafanywa ili kuiokoa Ugiriki, Italia imeshatajwa kuwa nchi nyingine inayoweza kuhitaji msaada. Nchi hiyo ina deni la Euro Trilioni 1.84. Lakini bado Italia haiwezi kufananishwa na Ugiriki. Hata hivyo panahitajika utaratibu wa kimataifa utakaozuia ulanguzi wa dhamana za serikali.

Gazeti la Darmstädter Echo linatoa maoni juu ya Misri.Gazeti hilo linasema baada ya nderemo zilizofuatia kung'olewa kwa Mubarak, sasa hali halisi inawakabili wanamapinduzi wa nchini Misri. Wamerudi tena kwenye uwanja wa Tahrir. Wanamapinduzi hao hawana imani na baraza la kijeshi na wao wenyewe wameshindwa kuonyesha kuwa ni nguvu ya kisiasa.

Mwandishi/Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen/

Mhariri/Abdul-Rahman

 • Tarehe 13.07.2011
 • Mwandishi Abdu Said Mtullya
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/11uCj
 • Tarehe 13.07.2011
 • Mwandishi Abdu Said Mtullya
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/11uCj