1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Rais Samia ameirejesha Tanzania ulimwenguni

Sylvia Mwehozi
7 Mei 2021

Licha ya Rais wa Tanzania Samia Hassan Suluhu kusisitiza kuwa yeye na mtangulizi wake John Magufuli ni kitu kimoja, tofauti za kimtazamo baina ya wawili hao ziko wazi katika mwelekeo wa kisera, anaandika Sylvia Mwehozi.

https://p.dw.com/p/3t72M
Uganda Unterschrift EACOP in Kampala
Picha: Presidential Press Unit/Uganda

Ni zaidi ya mwezi mmoja sasa tangu rais Samia Suluhu Hassan achukue madaraka ya kuiongoza Tanzania. Tofauti na mtangulizi wake Hayati John Magufuli ambaye alipenda sana kujifungia, rais Samia anaonekana kuwa kiongozi mwenye kupenda ushirikiano wa kimataifa haswa akianza na ushirikiano wa majirsni zake wa karibu.

Rais Samia tayari amefanya ziara rasmi nchini Uganda na kufanya mazungumzo ya pande mbili ikiwemo kutia saini mkataba muhimu wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda, hadi bandari ya Tanga (Tanzania), ambao utagharimu dola za Marekani bilioni 3.5.

Kenia Nairobi | Besuch Samia Suluhu Hassan, Präsidentin Tansania | mit Uhuru Kenyatta
Rais Samia Hassan Suluhu akisalimiana na mwenzake wa Kenya Uhuru Kenyatta, wakati wa ziara yake nchini Kenya, Mei 4, 2021.Picha: Simon Maina/AFP/Getty Images

Ziara kama hiyo pia ameifanya katika taifa jirani la Kenya ambalo kijadi nchi hizi mbili huitana watani wa jadi. Lakini kwa muda sasa chini ya uongozi wa Hayati Magufuli, Kenya na Tanzania ziliingia katika mivutano kuhusu masuala kadhaa.

Ziara hiyo ya kwanza ya Samia inakuja wakati mataifa haya mawili yakijaribu kurejesha tena uhusiano wake na kuitafutia ufumbuzi mivutano iliyojitokeza hasa inayohusu biashara katika maeneo ya mpaka.

Soma pia: Rais Uhuru Kenyatta amlaki Rais Samia Suluhu jijini Nairobi

Kwa kuzingatia ziara zake mbili alizokwisha zifanya kwa majirani zake, ni wazi kwamba rais samia yuko tayari kuendeleza ushirikiano wa kimataifa na kuwa rais asiyejifungia. Kama alivyosema wakati wa hotuba yake bungeni kwamba ataendeleza yake yaliyofanywa na mtangulizi wake, lakini kwa kufanya mabadilliko. Miongoni mwa yaliyokuwa yakisubiriwa ni kuona jinsi gani rais Samia ataendeleza miradi iliyoanzishwa na hayati magufuli kama mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta.

Mitarbeiter von DW Kiswahili
Mwandishi wa DW Sylvia MwehoziPicha: DW/L. Richardson

Sera mpya kuhusu janga la virusi vya Corona

Wakati wa ziara yake rais Samia ameonekana kutilia mkazo uvaaji wa barakoa licha ya kwamba akiwa nchini mwake rais huyo bado haonekani kuvaa barakoa wakati wa shughuli nyingi za umma.

Hatia yake ya kuvaa barakoa anapokuwa ziara za kigeni inaashiria kwamba sasa Tanzania inaweza kuwa katika njia ya pamoja na wanachama wenzake wa jumuiya ya kikanda katika hatua za kukabiliana na covid19.

Hivi karibuni Tanzania ilitoa mwongozo mpya kuhusu janga hilo na ni wazi kwamba taifa hilo sasa linarejea katika njia ya mapambano ya pamoja dhidi ya covid 19.

Rais Samia pia amefanya mazungumzo na rais wa shirika la fedha ulimwenguni Kristalina Georgieva ambapo tayari shirika hilo limeahidi kuendelea kuisaidia Tanzania katika nyanja mbalimbali za utalii, afya na huduma za kijamii. IMF inatarajia kuidhinisha mkopo wa riba nafuu kuisadia tanzania kukabiliana na athari za COVID-19.

East Africa Oil Pipeline Abkommen | Samia Suluhu Hassan und Yoweri Museveni
Rais Samia Suluhu Hassan akiwa katika mazungumzo na rais wa Uganda Yoweri Museveni katika ikulu ya Entebbe, Aprili, 11, 2021.Picha: Presidential Press Unit/Uganda

Kulingana na Samia mwenyewe, janga la covid limekuwa na athari katika uchumi wa Tanzania ambao ukuaji wake uliporomoka kutoka asilinia 6.9 hadi asilimia 4.7.

Ninaamini kwamba ziara hizi za mwanzo za rais Samia zitairejesha Tanzania katika ramani ya dunia na kurejesha wajibu wake katika usulubishi wa migogoro ya kikanda na kuwa nchi iliyosifika ya kisiwa cha amani.

Soma pia:Kenya na Tanzania zatia mikataba ya kibiashara na uwekezaji

Zaidi ya hayo, mwelekeo wa rais samia wa sera ya kigeni utaifanya Tanzania kuwakilishwa ipasavyo katika nyanja za kimatifa kuanzia katika Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa.

Muhimu ni kwamba mwelekeo huo unarejesha matumaini kwa wawekezaji wa kigeni katika kuifikiria Tanzania kama nchi iliyo rafiki kwenye uwekezaji.