Majeshi ya Ushirika yaanza kuishambulia Libya | Matukio ya Kisiasa | DW | 20.03.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Majeshi ya Ushirika yaanza kuishambulia Libya

Marekani, Uingereza na Ufaransa zimeanza mashambulizi ya anga dhidi ya Libya alfajiri ya leo (20.03.2011) na kuamsha ghadhabu kubwa kwa Muammar Gaddafi aliyelitangaza eneo la Mideterranean kuwa medani ya mapambano.

Ndege ya Uingereza, Tornado GR4, ikianza kuruka kuelekea Libya

Ndege ya Uingereza, Tornado GR4, ikianza kuruka kuelekea Libya

Katika kile kinachoonekana kuwa ni uingiliaji mkubwa wa kijeshi wa mataifa ya magharibi kuwahi kushuhudiwa tokea uvamizi wa Iraq ulioongozwa na Marekani hapo mwaka 2003, meli za kivita za Marekani na manuwari za Uingereza zimefyatuwa takribani makombora 110 ya Tomahawk ndani ya Libya.

Adimeri wa Marekani, William Gortney, akizungumza na waandishi wa habari katika wizara ya ulinzi ya Marekani amesema malengo yako wazi.

"Kwanza ni kuzuwiya mashambulizi zaidi yanayofanywa na vikosi vya serikali kwa raia wa Libya na kwa makundi ya upinzani hususan yale yalioko ndani na karibu na mji wa Benghazi na pili ni kuharibu uwezo wa utawala huo kukaidi amri ya kuruka ndege juu ya anga ya Libya ambayo tunaitekeleza." Amesema Gortney kwenye makao makuu ya jeshi la Marekani, Pentagon.

Madai ya marufuku ya anga ya waandamanaji hawa yameitikiwa

Madai ya marufuku ya anga ya waandamanaji hawa yameitikiwa

Mashambuluzi hayo dhidi ya Libya yanakuja siku mbili baada ya azimio namba 1973 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililoungwa mkono na Jumuiya ya Waarabu, kuidhinisha hatua ya kijeshi kuvizuwia vikosi vya Kanali Gaddafi kuwashambulia raia kutokana na uasi dhidi ya utawala wake wa kidikteta wa miaka 41.

Mwandishi wa shirika la habari la AFP amesema mabomu yamedondoshwa mapema leo asubuhi karibu na Bab al-Aziziya, makao makuu ya Kanali Gaddafi, mjini Tripoli, ambapo vikosi vya Gaddafi vilijibu kwa mashambulizi ya mizinga ya kutungulia ndege yaliodumu kwa dakika 40.

Televisheni ya taifa ya Libya imeonyesha picha ya mamia ya wafuasi wa Gaddafi ambao imesema walikuwa wamekusanyika na mapema ili kutumika kama ngao ya kibinaadamu huko Bab al-Aziziya na katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Tripoli.

Afisa wa serikali ya Libya ameliambia shirika la habari la AFP takriban watu 48 wameuwawa na wengine 150 wamejeruhiwa wengi wakiwa ni wanawake na watoto katika mashambulizi hayo ambayo yalianzishwa ndege za kivita za Ufaransa kwa kuishambulia gari moja ambalo jeshi la Ufaransa limesema lilikuwa la vikosi vya Gaddafi.

Wanajeshi wa Gaddafi wakilinda makaazi ya kiongozi huyo, Bab Al Azizia, mjini Tripoli

Wanajeshi wa Gaddafi wakilinda makaazi ya kiongozi huyo, Bab Al Azizia, mjini Tripoli

Vyombo vya habari vya taifa nchini Libya vimesema, ndege za kivita za mataifa ya magharibi hapo jana usiku, zilishambulia maeneo ya kiraia mjini Tripoli na kusababisha maafa. Naye msemaji wa jeshi amesema mashambulizi hayo pia yalifanyika kwa matangi ya mafuta katika mji wa Misrata unaoshikiliwa na waasi mashariki ya Tripoli.

Gaddafi katika ujumbe mfupi wa sauti uliorekodiwa katika televisheni ya taifa ameshutumu vikali mashambulizi hayo kuwa ni ushenzi na ni uvamizi wa vita vya msalaba.

"Huu ni uvamizi wa uwenda wazimu usio wa haki ni mwanzo wa vita vyengine vya msalaba kwa kiwango kikubwa.Sasa maghala ya silaha yamefunguliwa na wananchi wote wa Libya wamepatiwa silaha kupambana dhidi ya vikosi vya mataifa ya magharibi." Amesema Gaddafi.

Gaddafi amepa kulipiza kisasi kwa kufanya mashambulizi kwa maeneo ya kijeshi na kiraia katika eneo la Medirerranean ambalo amesema limegeuzwa kuwa medani ya mapambano.

Moto na moshi mzito baada ya ndege ya kijeshi kuangushwa mjini Benghazi

Moto na moshi mzito baada ya ndege ya kijeshi kuangushwa mjini Benghazi

Wizara ya mambo ya nje ya Libya imesema kufuatia mashambulizi hayo inaliona azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lenye kuamuru usitishaji wa mapigano wa vikosi vyake kuwa halifai na imedai kufanyika kwa mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama.

Hapo Alhamisi Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azmio nambari 1973 ambalo limeidhinisha matumizi ya hatua zozote zile kuwalinda raia na kulazimisha usitishaji wa mapigano na kupiga marufuku kuruka ndege kwenye anga ya Libya.

Urusi imeelezea masikitiko yake juu ya mashambulizi hayo na kusema kwamba azimio nambari 1973 limepitishwa kwa pupa wakati Umoja wa Afrika ambao ulikuwa umepinga hatua ya kijeshi leo umetowa wito wa kusitishwa mara moja kwa mashambulzi hayo.

Rais Barack Obama wa Marekani akiwa ziarani nchini Brazil amesema operesheni ya Marekani nchini Libya haitojumuisha wanajeshi wa ardhini.

Hivi leo (20.03.2011), Jumuiya ya Kujihami ya Mataifa ya Magharibi NATO inatazamiwa kuamuwa iwapo ijunge na mashambulizi hayo dhidi ya Libya.

Maelfu hapo jana walikimbia Benghazi wakati vikosi vya Gaddafi vilipoushambulia mji huo wa mashariki ngome kuu ya waasi kwa mizinga na vifaru baada ya mashambulizi mawili ya anga yaliofanyika mapema asubuhi.

Tokea Ijumaa Libya imekuwa ikisisitiza kwamba ilikuwa inaheshimu usitishaji wa mapigano iliojitangazia yenyewe. Imesema vikosi vyake vya ulinzi vimeshambuliwa hapo jana magharibi mwa Benghazi pamoja na kwa kutumia ndege ya waasi na kwamba imejibu mashambulizi hayo kwa kujihami.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef

DW inapendekeza

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com