Makombora ya kigeni yarindima Libya | Habari za Ulimwengu | DW | 20.03.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Habari za Ulimwengu

Makombora ya kigeni yarindima Libya

Nchini Libya,mashambulio ya angani na baharini yameanza asubuhi ya leo katika eneo la pwani lililo karibu na mji mkuu wa Tripoli.

default

Wanajeshi wa Kifaransa wakijiandaa kuivamia Libya

Azma ya mashambulio hayo ni kuwashinikiza na kuwalazimisha wanajeshi walio watiifu kwa Kanali Muammar Gaddafi kusalimu amri na kuyasitisha mapigano yanayowalenga raia wa kawaida.Vikosi vya kigeni vimeichukua hatua hiyo baada ya Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuliidhinisha azimio linalowaidhinisha kutumia mbinu zote kuwalianda raia wa Libya pamoja na kuiwekea marufuku ya ndege kuruka kwenye anga yake.

Präsident Nicolas Sarkozy Libyen-Sondergipfel Elysee-Palast Paris Uno-Einsatz gegen Libyen Yves Leterme Flash-Galerie

Kikao cha dharura cha Paris:viongozi wa ulimwengu wakilijadili suala la Libya na utekelezaji wa azimio 1973

Makombora ya kigeni

Ndege za Ufaransa ziliyarusha makombora ya kwanza yaliyovilenga vifaru na magari ya kivita kwenye eneo linalodhibitiwa na waasi la Benghazi.Hili ni shambulio kubwa zaidi la kimataifa kuwahi kufanyika katika taifa na eneo hilo la kiarabu tangu Iraq kuvamiwa kijeshi mwaka 2003. Ifahamike kuwa mashambulio hayo yametokea baada ya kikao maalum cha dharura kufanyika mjini Paris nchini Ufaransa walikokutana viongozi wa mataifa ya magharibi na yale ya Kiarabu wanaoiunga mkono operesheni hiyo ya kijeshi.Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy aliusisitizia umuhimu wa operesheni hiyo kwenye kikao hicho.

'Odyssey Dawn'

Saa chache baada ya hatua hiyo,manowari na meli za vita za Uingereza na Marekani zilivurumisha makombora yaliyoulenga mji mkuu wa Tripoli na ule wa magharibi wa Mesrata unaodhibitiwa na wanajeshi wanaomuunga mkono Kanali Muammar Gaddafi.

Kwa mujibu wa mafisa wa jeshi la Marekani,ndege na vikosi vyao vinashirikiana na vile vya Uingereza,Ufaransa,Canada na Italia katika operesheni hiyo ya Odyssey Dawn.Kwa upande wake,kiongozi wa Libya Kanali Muammar Gaddafi aliielezea operesheni hiyo kuwa mashambulio ya kikoloni.Katika ujumbe wake uliotangazwa na kituo cha taifa cha televisheni,muda umewadia kutumia zana zote za kijeshi na kuupa umma silaha kwa minajili ya kuilinda Libya na kuihifadhi hadhi yake.Duru zinaeleza pia kuwa maeneo wanakoishi raia wa kawaida nayo pia yalivamiwa katika miji ya Tripoli na Mesrata kwenye kambi ya vikosi vya Kanali Muammar Gaddafi.

Militäreinsatz in Libyen hat begonnen Britische Air-Force-Flugzeuge landen in Zypern NO FLASH

Nege za kivita za kigeni:Operation Odyssey New Dawn

Hisia tofauti

Kufuatia mashambulio hayo,hatua hiyo imepokelewa kwa hisia tofauti na wakaazi wa Benghazi.Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron amesema kuwa hatua hiyo ilihitajika kwani Kanali Gaddafi aliikiuka ahadi yake.Baada ya kikao hicho cha Paris,Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron alisisitiza kuwa lazima mauaji ya raia wa kawaida yakomeshwe. 

Kwa upande mwengine,serikali ya Libya imewalaumu waasi wanaoaminika kuwa na mafungamano na kundi la kigaidi la Al Qaeda kwa kuyavunja makubaliano ya kusitisha vita yaliyofikiwa siku ya Ijumaa.

Libyen 19.03.2011

Milipuko ya Benghazi

Wafuasi wa Gaddafi

Maelfu ya watu wanaripotiwa kuwa walikusanyika kwenye uwanja wa kasri la Kanali Muammar Gaddafi wa Ba al-Aziziyah kama njia yao ya kumuunga mkono kiongozi wao.Baadhi yao walisikika wakisema kuwa watawaruhusu wakimbizi haramu wanaoelekea barani Ulaya kupita nchini mwao bila vizuizi vyovyote 

Wakati huohuo,Rais Obama wa Marekani amesisitiza kuwa azma ya operesheni hiyo ni kuwalinda raia wa Libya.Akizungumza akiwa mjini Brasilia alikoanza ziara yake ya siku tano ya eneo la Latin Amerika Rais Barack Obama alisema kuwa ameviidhinisha vikosi vyake kushiriki kwenye operesheni hiyo kama sehemu ya harakati za kimataifa.Hata hivyo aliirejea tena kauli yake ya kusisitiza kuwa kamwe wanajeshi wa  nchi kavu wa Marekani hawatoingia kwenye ardhi ya Libya.

Msimamo wa AU

Yote hayo yakiendelea,jopo maalum la Umoja wa Afrika linaloshughulikia suala la Libya limetoa wito wa mashambulio ya aina yoyote ile kusitishwa nchini humo.Ili kuzipa msukumo zaidi harakati zao,jopo hilo linajiandaa kukutana Ijumaa ijayo tarehe 25 mwezi huu watakapokuwa pamoja na wawakilishi wa Umoja wa nchi za Kiarabu,Arab League,Umoja wa Ulaya na Mataifa pamoja na shirika la masuala ya kiislamu la OIC.

Mwandishi:Mwadzaya,Thelma-RTRE/AFPE/APE

Mhariri:Josephat Charo

DW inapendekeza

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com