Majeshi ya Gaddafi yaingia Benghazi | Habari za Ulimwengu | DW | 19.03.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Habari za Ulimwengu

Majeshi ya Gaddafi yaingia Benghazi

Majeshi ya Kanali Mohammar Gaddafi yameingia katika mji wa Benghazi ambao ni ngome ya waasi, na kukaidi matakwa yanayotaka kusitishwa haraka kwa mapigano

default

Mripuko baada ya ndege ya majeshi ya Gaddafi kuangushwa na waasi nje ya mji wa Benghazi

Msemaji wa waasi hao amesema kuwa majeshi ya kanali Gaddafi yameingia mjini humo ambapo mashuhuda wameona mripuko karibu na makao makuu ya waasi hao.

Mkaazi mmoja wa mji huo amekiambia kituo cha televisheni cha Al Jazeera kwamba mashambulio ya mizinga na mambo yaliendelea usiku kucha baada ya majeshi hayo kuingia katika viunga vya mji huo.

Hapo jana Libya ilitangaza kusitisha harakati zake za kijeshi dhidi ya waasi ikiwa ni siku moja baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupitisha azimio la vikwazo vya anga dhidi ya nchi hiyo.Hata hivyo Libya imelipinga vikali azimio hilo, na kusema ni la uonevu dhidi yake.

Katika hatua nyingine, kiongozi wa Libya Kanali Mohammar Gaddafi amewaandikia barua viongozi wa mataifa ya magharibi akiwaonya juu ya madhara yatakayotokea iwapo wataishambulia nchi yake.

Katika barua hiyo aliyowaandikia viongozi wa Marekani, Uingereza na Ufaransa Kanali Gaddafi amesema wananchi wa Libya wako tayari kufa kwa ajili ya nchi yao na kwamba mataifa hayo yatajuta iwapo yataivamia.

Wakati huo huo Waziri wa Mambo ya Nje wa Libya Mussa Kussa amemuomba Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon kutuma waangalizi wa umoja huo nchini Libya kwenda kuthibitisha na kusimamia usitishwaji wa mapigano ambayo serikali yake imeutangaza katika kutimiza matakwa ya Baraza la Usalama la umoja huo.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/DPA

Mhariri:Mohamed Dahman

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com