Majadiliano kupunguza silaha za nyuklia | Matukio ya Kisiasa | DW | 07.05.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Majadiliano kupunguza silaha za nyuklia

Hata baada ya miongo miwili tangu kumalizika kwa Vita Baridi, Urusi na Marekani bado zinadhibiti silaha za nyuklia zinazoweza kusababisha maangamizi makubwa.

Leo mawaziri wa nje Hillary Clinton wa Marekani na Sergei Lavrov wa Urusi wanakutana mjini Washington, kujadili suala la kupunguza silaha hizo.Majadiliano ya mawaziri hao mawili hasa yanahusika na mkataba utakaochukua nafasi ya mkataba wa sasa unaomalizika mwisho wa mwaka 2009.Kwa ufupi, mkataba huo unajulikana kwa jina START. Mazungumzo ya mwanzo ya mkataba mpya yalifanywa majuma machache yaliyopita pale Clinton na Lavrov walipokutana Rome nchini Italia.Baadae,wote wawili wakasema kuwa wameridhika na jinsi mazungumzo hayo yalivyokwenda.

Mkataba wa START uliotiwa saini Julai mwaka 1991 na unaomalizika mwisho wa mwaka huu ni makubaliano kamilifu kutiwa saini na nchi hizo mbili kwa azma ya kupunguza silaha za nyuklia.Kwa kweli, mada hiyo ilipata msukumo mpya baada ya Rais wa Marekani Barack Obama kutoa hotuba ya kusisimua tarehe 4 April wakati wa ziara yake mjini Prague, Jamhuri ya Czech.Itakumbukwa kuwa muda mfupi tu baada ya kuingia madarakani,

Obama alisema kuwa katika sera za nje za serikali yake, juhudi za kushirikiana na Urusi ili kupunguza silaha za nyuklia za pande zote mbili zitapewa kipaumbele.Akaongezea kuwa mataifa yote mawili yanapaswa kuwa katika mstari wa mbele kuzuia uenezaji wa silaha.

Rais Barack Obama na Rais Dmitri Medvedev wa Urusi baada ya kukutana uso kwa uso kwa mara ya kwanza,kando ya mkutano wa kilele wa kundi la G-20 mjini London,walisema kuwa watakubaliana upesi iwezekanavyo kuhusu mkataba huo mpya. Lengo ni kukamilisha mkataba mpya kabla ya Desemba mwaka 2009.

Lakini kabla ya mkutano huo wa London,Moscow ilisisitiza kuwa inaazimia kujipatia silaha za kisasa.Katika mwezi wa Machi Rais Medvedev aliiruhusu wizara ya ulinzi mjini Moscow kutangaza kuwa kuanzia mwaka 2011 majeshi ya nchi kavu na majini nchini yatapatiwa silaha mpya za aina mbali mbali. Medvedev akieleza wasiwasi wa Urusi kuhusu Shirika la Kujihami la Magharibi NATO linalozidi kupanuka alisema lengo lao ni kuimarisha nguvu na uwezo wa silaha zake za nyuklia.

Ni dhahiri kwamba,safari ni ndefu kabla ya majadiliano ya kupunguza silaha za nyuklia kuweza kufikia hatua halisi za kupunguza silaha hizo.

Mwandishi:H.Spross/P.Martin

Mhariri:Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com