Mahakama ya Pakistan yafutilia mbali vikwazo dhidi ya Musharraf | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 19.11.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Mahakama ya Pakistan yafutilia mbali vikwazo dhidi ya Musharraf

Mahakama kuu nchini Pakistan imefutilia mbali vipingamizi vyote dhidi ya kuchaguliwa tena rais Pervfez Musharraf. Wakati huo huo, rais Musharraf ametangaza tarehe ya uchaguzi kuwa Januari 8.

default

Jenerali Pervez Musharraf

Mwanasheria mkuu nchini Pakistan, Malik Mohammad Qayyum, amesema mahakama kuu imefutilia mbali malalamiko matano kati ya sita yanayopinga kuchaguliwa tena Pervez Musharraf kuwa rais wa Pakistan. Lalamiko moja lililosalia litajadiliwa Alhamisi ijayo.

Ikiwa na majaji wapya walioteuliwa na jenerali Musharraf, mahakama kuu ya Pakistan imeanza mashauriano mapema leo juu ya uhalali wa hali ya hatari iliyotangazwa na rais Musharraf na ikiwa ana haki kikatiba kuingoza Pakistan kwa awamu ya tatu.

Mawakili nchini Pakistan wamesema mashtaka matano yaliyotupiliwa mbali yalichukuliwa kuwa changamoto kubwa dhidi ya rais Pervez Musharraf. Jenerali Musharraf aliyewatimua majaji wa mahakama kuu wakati alipotangaza hali ya hatari mnamo Novemba 3, ameahidi kujiuzulu wadhifa wake kama kamanda mkuu wa jeshi la Pakistan na kuwa kiongozi wa kiraia mara tu mahakama itakapoidhinisha kuchaguliwa kwake. Uamuzi wa mahakama kuu ya Pakistan unaongeza nafasi ya rais Musharraf kutimiza ahadi yake.

Huku shinikizo la kumtaka arejeshe utawala wa kidemokrasia nchini likizidi dhidi yake, rais Musharraf ametangaza kuwa uchaguzi utafanyika tarehe 8 mwezi Januari mwakani. Hata hivyo kiongozi huyo hakuashiria ikiwa atatangaza kumalizika kwa utawala wa hali ya hatari, licha ya kuwepo shinikizo kubwa kutoka kwa vyama vya upinzani nchini Pakistan na serikali ya Marekani kutaka utawala wa hali ya hatari umalizike kabla ya uchaguzi mkuu.

Wakati haya yakiarifiwa, chama cha Benazir Bhutto, kimesema leo kwamba kimeondoa lalamiko lake dhidi ya rais Musharraf katika mahakama kuu ya Pakistan. Chama cha Pakistan People´s Party, PPP, kimesema kitawasilisha lalamiko lake baadaye kwa sababu hakiwatambui majaji wapya walioteuliwa na rais Musharraf wakati wa utawala wa hali ya hatari. Mbunge wa chama cha PPP, Latif Khosa, amesema uteuzi wa majaji hao si halali na kwa hiyo kutafuta uamuzi kutoka kwao ni kazi bure.

Benazir Bhutto amesema ana wasiwasi upinzani huenda ukabanwa sana katika uchaguzi wa Januari 8.

´Nilishauriana naye juu ya kuirejesha Pakistan katika utawala wa kidemokrasia. Nilifanya hivyo ili kuzuia matatizo yanayotukabili wakati huu. Lakini badala ya kutekeleza makubaliano tuliyoyafikia, jenerali Musharraf akaisitisha katiba. Na nikafikia uamuzi kwamba hakuwa na haja hata kidogo kuupa upinzani nafasi sawa katika uchaguzi.´

Katika matamshi yake ya kwanza aliyoyafanya hadharani baada ya kukutana na naibu waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani, John Negroponte, rais Pervez Musharraf ameapa kwamba uchaguzi utakuwa wa haki, lakini wakati huo huo akautetea utawala wa hali ya hatari.

Negroponte, aliyeondoka Pakistan hapo jana, alikuwa muangalifu asimudhoofishwa rais Musharraf, ambaye ni mshirika muhimu wa Marekani katika vita dhidi ya Al Qaeda na Taliban. Hata hivyo Negroponte alisisitiza watu waliotiwa mbaroni nchini Pakistan katika kipindi cha majuma mawili yaliyopita, waachiliwe huru na ukandamizaji wa uhuru wa vyombo vya habari umalizike.

 • Tarehe 19.11.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CJCy
 • Tarehe 19.11.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CJCy

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com