1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lugovoi ainyooshea kidole Uingereza kwa mauaji ya Litvinenko

31 Mei 2007

Mshukiwa wa mauaji ya aliyekuwa jasusi wa shirika la KGB la Urussi Alexander Litveneko, ameituhumu Uingereza kuhusika na njama ya mauaji hayo.

https://p.dw.com/p/CB3q

Andrei Lugovoi ambaye anakanusha kuhusika na kifo cha Litveneko amewaambia waandishi habari mjini Moscow kwamba yeye anasingiziwa.

Andrei Lugovoi anasema kitengo cha kijaasusi cha Uingereza cha MI6 kilimuajiri marehemu Litvenenko na vile vile kilijaribu kumuajiri nayeye kutafuta habari juu ya rais Vladmir Putin wa Urussi.

Uingereza ilisema suala hilo lilihusika zaidi na uhalifu kuliko ujasusi tu.

Uingereza imeiomba Urussi imkabidhi bwana Lugovoi kuhusiana na mauaji ya Litveneko lakini kwa mujibu wa katiba ya Urussi haiwezekani kumtoa raia wa nchi hiyo kwa nchi nyingine kwa ajili ya kukabiliwa na mashtaka.

Litveneko aliuwawa kwa kupewa sumu ya miale mnamo mwezi Novemba mwaka jana.Baadae Miale hiyo ya Isotope Polonium 210 iligunduliwa katika maeneo kadhaa ambako bwana Lugovoi alitembelea mjini London lakini kwa upande wake anasema alikuwa shahidi na wala sio mshukiwa kwenye kesi hii.

Lugovoi ambaye yeye mwenyewe alikuwa jaasusi wa shirika la KGB la Urussi anasema kuuwawa kwa kupewa sumu bwana Litveneko hakungetokea bila ya kuhusika kwa shirika la ujasusi la Uingereza.

Alidokeza zaidi akisema

''Waingereza walinitaka nikusanye maelezo ya kumkashifu rais Putin na familia yake walinitaka nimuajiri mtu aliyekaribu na Putin Litveniko alinielezea hata siri za kuandika.’’

Aliongeza kusema kwamba ushahidi anao wa kutosha kudhibitisha kuhusika kwa maajasusi wa Uingereza kwenye mauaji hayo.

Lugovoi amesema mauaji hayo yalifanywa na aidha Mi6 kitengo cha ujasusi wa mambo ya nje cha Uingereza, mafia wa Urussi au Boris Berezovsky mpinzani wa Kremlin aliyekimbilia Uingereza.

Bwana Lugovoi amefafanua zaidi akisema kama alivyokuwa Litveneko bwana Berezovsky alikuwa akiifanyia kazi idara ya ujasusi ya Uingereza lakini wawili hao yaani Litveneko na Berezovsky hawakupikwa chungu kimoja na hivyo Mi6 haikuweza kumdhibiti bwana Litvenenko.

Hata hivyo Berezovsky ambaye amepewa hifadhi nchini Uingereza amekanusha kuhusika na mauaji ya Litvenenko na amesema kuwa ni wazi matamshi yaliyotolewa leo na Lugoi kwamba mauaji ya Litvenenko yana mkono wa Urussi ambayo inamuelekeza nini cha kusema bwana Lugovoi.

Madai yaliyotolewa na bwana Lugovoi dhidi ya Uingereza huenda yakazidi kuharibu uhusiano kati ya serikali za Moscow na London.

Lugovoi ameuwaambia mkutano na wandishi habari kwamba anakila chembe ya ushahidi kwa madai yake na kwamba atatoa habari zaidi kwa wachunguzi wa Urussi.