1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Libya ina mustakbali upi baada ya kifo cha Gaddafi?

26 Oktoba 2011

Maswali yanayoulizwa baada ya kifo cha Muammar Gaddafi ni mustakabali wa Libya na kwa kiasi gani nchi hiyo iko huru kweli na ikiwa ule uadui uliopelekea uasi hatimaye umeshazikwa na Gaddafi jangwani!

https://p.dw.com/p/12zkE
Mwenyekiti wa Baraza la Mpito la Libya, Mustafa Abdul-Jalil.
Mwenyekiti wa Baraza la Mpito la Libya, Mustafa Abdul-Jalil.Picha: dapd

Riadh Sidaoui, mtaalamu wa masuala ya siasa na mkurugenzi wa Kituo cha Uchambuzi wa Masuala ya Kisiasa na Kijamii ya Ulimwengu wa Kiarabu, ana majibu yale yale waliyonayo wengine.

"Naamini kuna vikwazo vingi mno kabla ya ndoto ya Libya huru haijageuka kweli. Kikwazo kimojawapo ni ombwe la kitaasisi na la kisiasa pamoja na uadui kati ya raia wenyewe kwa wenyewe."

Libya ilivyo sasa haina mfumo wa kisiasa unaoeleweka. Hakuna utawala. Gaddafi mwenyewe hakuruhusu kuwepo kwa vyama vya kisiasa, akihofia kwamba vingelikuwa hatari kwake.

Katika miezi ya hivi karibuni, matukio kadhaa yaliyotokea yamethibitisha ombwe la kisiasa ndani ya Baraza la Mpito la Libya lenyewe, ambalo hivi sasa ndicho chombo kinachoitawala Libya. Kamati ya watu 40 inayounda Baraza hilo, ina tafauti zisizofichika.

"Ndani ya Baraza la Mpito kuna mgawanyiko wa wazi kwa misingi ya wapi mjumbe anatoka. Mashariki dhidi ya Magharibi. Wa Magharibi walisaidiwa sana na Gaddafi. Wa Mashariki walibaguliwa. Kuna tafauti pia ya kiitikadi. Kuna wale wanaoelemea kwenye Uislamu wa siasa kali, wafuasi wa Salafi, na wale wafuasi wa usoshalisti na uliberali." Anasema Günter Meyer, mkuu wa Kituo cha Utafiti wa Masuala ya Nchi za Kiarabu katika Chuo Kikuu cha Mainz.

Taswira iliyofichika sasa yaibuka

Wapiganaji wa Baraza la Mpito wakishangilia uhuru mpya wa Libya.
Wapiganaji wa Baraza la Mpito wakishangilia uhuru mpya wa Libya.Picha: dapd

Kabla ya kifo cha Gaddafi, taswira hii ya uadui ilikuwa haionekani sana. Lakini sasa, ambapo mkakati wa kisiasa uko wazi: serikali inapaswa kuundwa ndani ya siku 30 zijazo, uchaguzi wa Bunge ndani ya miezi minane ijayo, swali ni ikiwa Libya ya baadaye itakuwaje na nani wa kumuamini kumkabidhi madaraka ya kuwaongoza Walibya?

Waziri Mkuu wa Baraza la Mpito, Mahmoud Jibril, mchumi aliyesomea Marekani na kuitumikia serikali ya Gaddafi kwa muda mrefu, ameshasema mwenyewe kwamba hatokuwemo kwenye serikali ijayo.

Sababu ni kwamba haaminiki na wenzake, maana kwa kundi la Waliberali ndani ya Baraza la Mpito, Jibril ni mtu aliyekuwa karibu sana na Gaddafi, na kundi la wanaoegemea siasa za Uislamu, huyu ni kibaraka wa Marekani.

Wanasiasa sio wenye nguvu

Waziri Mkuu wa Baraza la Mpito la Libya, Mahmoud Jibril.
Waziri Mkuu wa Baraza la Mpito la Libya, Mahmoud Jibril.Picha: dapd

Nguvu hasa za kisiasa hazitakuwa kwa mtu kama Jibril, bali katika taifa lenye makabila 130 tafauti, na ambalo hisia za utiifu kwa kabila ni za hali ya juu, mtu anayeweza kuwa na nguvu ya kisiasa katika Libya mpya, ni lazima awe na nguvu za makabila hayo.

Kwa upande mwengine, utajiri wa mafuta wa Libya unapaswa kuhakikisha maendeleo ya kiuchumi ya taifa hilo, ambayo mataifa ya Magharibi wanayachukulia kwa shauku kubwa.

Mataifa hayo, hata hivyo, yanaoneana kutiwa shaka na kauli ya Mustafa Abdul-Jalil, kwamba msingi wa sheria za Libya, utakuwa ni Sharia ya Kiislamu.

Upande mmoja, kauli hii imewatisha hata Walibya wenyewe, na kwa hivyo ni kikwazo chengine kwa Libya mpya baada ya Gaddafi, lakini kwa upande mwengine, si lazima watu katika jamii za Kiislamu wachukuwe kila kitu kutoka demokrasia wa Kimagharibi. Badala yake wanaweza kuchukuwa baadhi na kuchanganya na ya itikadi na imani zao.

Mwandishi: Stefan Duckstein/DW
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Othman Miraji