Kyriakos Mitsotakis ana kibarua kigumu Ugiriki | Makala | DW | 09.07.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Makala

Kyriakos Mitsotakis ana kibarua kigumu Ugiriki

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wameandika juu ya kuchaguliwa kwa Kyriakos Mitsotakis nchini Ugiriki, kupelekwa vikosi vya kijeshi vya Ujerumani nchini Syria na mabadiliko katika benki ya Ujerumani Deutsche Bank.

Miongoni mwa magazeti yaliyoandika juu ya kuchaguliwa kwa waziri mkuu mpya wa Ugiriki ni Lübecker Nachrichten na Frankfurter Rundschau. Lakini Mhariri wa gazeti la Reutlinger General-Anzeiger anaandika, Ingawa waziri mkuu mpya wa Ugiriki Kyriakos Mitsotakis anataka kufanya kazi kwa bidii, hilo pekee halitoshi. Anachoweza kufanya ni kutumia imani iliyowekwa kwake na wapiga kura, katika miezi hii michache ya kwanza baada ya kuchaguliwa akiwa na nguvu mpya ya kisiasa. Mwandishi anaendelea kusema, huenda wananchi wake wasimpe muda mwingi, kwani kwa sasa, wagiriki wamekuwa na uvumilivu mdogo wakijihisi walitumiwa na kudanganywa.

Benki ya Ujerumani Deutsche Bank kufanya marekebisho

Wahariri wa magazeti ya Südwest Presse na Volksstimme wameandika juu ya marekebisho yanayotarajiwa kufanywa na benki ya Ujerumani "Deutsche Bank", baada ya benki hiyo kutangaza kuwa inapanga kuwapunguza wafanyakazi 18,000 kama sehemu  ya marekebisho hayo.

Gazeti la Volksstimme la mjini Magdeburg limeandika, mtu yeyote ambaye aliwekeza katika Benki ya Ujerumani miaka kumi iliyopita, ni wazi kwamba akitazama  katika akaunti yake ya usalama inayodhihirisha uthabiti wa mtaji wa benki, anaiona hali ilivyo hivi sasa kuwa kama ndoto ya kutisha. Mhariri anaaeleza kuwa hisa za benki hiyo zimeshuka thamani yake toka Euro 45 hadi chini ya Euro Euro 7. Benki hiyo ambayo ilikuwa imejijengea heshima kubwa imepoteza hadhi yake katika miaka ya hivi karibuni. Mhariri anaendelea kusema, kwa benki ya Ujerumani kurejesha uaminifu iliyokuwa imejijengea litakuwa ndiyo jukumu kubwa hivi sasa. 

EU na Ujeruman zitaweza kutatua mgogoro wa Syria?

Mhariri wa gazeti la Märkische Oderzeitung anaandika juu ya uwepo wa vikosi vya kijeshi vya Ujerumani nchini Syria. Anasema, mbali na vikosi vya kijeshi vya ardhini vya Ujerumani kuwepo Syria, swali kubwa linabaki kuwa ni mchango gani ambao Ujerumani na washirika wake wa Ulaya wanao katika kuleta suluhisho la mgogoro wa Syria, ikiwa Marekani yenyewe ambayo kama ijulikanavyo sasa haina nia ya kuendelea kuhusika kwenye mgogoro huo. Mhariri anasema, Assad amefanikiwa kutengeneza vita vya wenyewe kwa wenyewe na kwa hili, wa kushukuriwa ni washirika wake, Urusi na Iran wanaomuunga mkono. Mhariri anamalizia kwa kusema ni vyema mtazamo wa Ulaya ukawekwa wazi katika hili, na si maneno matupu.