1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kwa nini Ujerumani haitahusisha siasa na Kombe la Dunia 2026

21 Januari 2026

Baada ya upinzani wao waliounesha waziwazi kwenye Kombe la Dunia lililopita nchini Qatar, timu ya taifa ya Ujerumani inaonekana haina uwezekano wa kufanya jambo kama hilo tena nchini Marekani mwaka 2026.

https://p.dw.com/p/57Cak
Marekani, Winston-Salem 2026 | Mwonekano wa uwanja wa Chuo Kikuu cha Wake Forest kwa mazoezi ya timu ya taifa ya Ujerumani (DFB)
Ujerumani itakuwa na kambi yake North Carolina mwanzoni mwa Kombe la Dunia, na huenda ikakabiliwa na maswali kuhusu kushiriki mashindano hayo katika hali ya sasa ya kijamii na kisiasa nchini Marekani.Picha: Wake Forest Athletics

Mkurugenzi wa michezo wa timu ya taifa ya Ujerumani, Rudi Völler, alisisitiza hivi karibuni katika kipindi cha michezo cha kila wiki kuwa, ingawa hakutakuwa na amri ya kuwanyamazisha wachezaji au maafisa, “haiwezekani masuala hayo yakajadiliwe karibu kabisa na siku ya mechi kama ilivyotokea kwenye janga la Qatar.”

Völler alikuwa akirejelea mjadala wa utepe wa mkononi wa One Love wakati wa Kombe la Dunia la Qatar, ambao Ujerumani—pamoja na mataifa mengine—iliachana nao dakika za mwisho baada ya FIFA kutishia kuchukua hatua za kinidhamu. Baadaye, kabla ya mechi dhidi ya Japan, wachezaji wa Ujerumani walifanya maandamano kwa kupiga picha ya pamoja wakiwa wamefunika midomo yao.

Hatua hiyo ilikumbana na ukosoaji mkubwa, lakini Jürgen Mittag, profesa wa siasa za michezo katika Chuo Kikuu cha Michezo cha Ujerumani cha mjini Cologne, anaamini hali ingekuwa tofauti kama Ujerumani ingefika robo fainali.

“Lakini ilivyokuwa, walikabiliwa na kejeli nyingi kwa sababu walikuwa na ujumbe wenye nguvu kimaana, lakini walionekana dhaifu kiuchezaji,” Mittag aliiambia DW.

Soka – Kombe la Dunia la FIFA Qatar 2022 | Ujerumani dhidi ya Japan
Hatua ya Ujerumani kuonyesha ishara za upinzani kabla ya mechi dhidi ya Japan nchini Qatar ilikumbana na ukosoaji mkubwa.Picha: Javier Garcia/Shutterstock/IMAGO

EU yadhoofisha msimamo wa Ujerumani

Matarajio ni kwamba nchini Marekani, Canada na Mexico, timu ya taifa ya Ujerumani itafanya vizuri zaidi uwanjani. Lakini swali linabaki: hali hiyo ina maana gani kwa msimamo wao nje ya uwanja?

Michael Mutz, profesa wa sayansi ya jamii katika michezo katika chuo kikuu cha Justus-Liebig mjini Giessen, ana mashaka kama kutakuwa na tamko lolote la kisiasa.

“Siwezi kufikiria kuwa DFB (Chama cha Soka cha Ujerumani) kitarudia tena kuendesha ajenda ya kisiasa dhidi ya nchi mwenyeji baada ya uzoefu mbaya walioupata Qatar,” Mutz aliiambia DW.

Aliongeza kuwa, “DFB iko kwenye hatari ya kutuhumiwa kwa undumilakuwili—kwa sababu iliikosoa vikali hali ya Qatar, lakini sasa huenda ikanyamaza kuhusu Marekani. Hata hivyo, chama hicho kitalazimika kukubali hali hiyo.”

Kwa upande wake, Jürgen Mittag anaamini kuwa msimamo wa Ujerumani umeendelea kudhoofishwa na hali ya sasa ya Umoja wa Ulaya. Umoja huo unakabiliwa na changamoto zaidi kufuatia hatua mpya za ushuru zilizotangazwa na Rais wa Marekani Donald Trump dhidi ya nchi sita wanachama wa EU, pamoja na Uingereza na Norway.

Hatua hizo zinahusishwa pia na suala la Greenland, ambako mataifa hayo yalituma wanajeshi au maafisa kwa sababu za kiusalama—eneo ambalo Trump ana nia ya kulitwaa.

“Demokrasia ya Ulaya pia imeathirika kwa kiasi fulani… inazidi kugawanyika, na hivyo kupunguza uwezo wake wa kuchukua hatua madhubuti katika sera za kigeni,” Mittag alieleza.
Alisema hali hiyo inaonekana kwa jumla katika siasa za kimataifa, na pia ndani ya masuala ya soka na michezo mingine.

Mittag aliongeza kuwa, “Ujerumani imekuwa mstari wa mbele katika diplomasia ya michezo katika miaka ya hivi karibuni, lakini imegundua kuwa licha ya kuwa na nafasi ya kuongoza, hupata uungwaji mkono kidogo sana.”

Alitolea mfano msimamo wa Ujerumani kuhusu kurejea kwa Urusi na Belarus kwenye Michezo ya Olimpiki. Ingawa Ujerumani ilipinga vikali na kujaribu kujenga muungano mpana, iliishia kupata uungwaji mkono mdogo.

Kwa mujibu wa Mittag, kushindwa huko kuliathiri sana msimamo wa Ujerumani na kuilazimisha kufikiria upya mkakati wake.

“Hapo ndipo Ujerumani ilitambua kuwa inahitaji mkakati tofauti. Haitaki kuachana na msimamo wake, lakini kuweka mkazo mkubwa sana kwenye maadili na misingi ya kimaadili si mkakati mzuri. Mwishowe, hali hiyo haisaidii kufanikisha malengo, na ukishindwa pia uwanjani, unajikuta ukikabiliwa na kejeli na dhihaka,” alifafanua.

Jezi ya ugenini ya DFB ya rangi ya waridi–zambarau (pink-lila) ya mwaka 2024
Andreas Rettig (kulia) akikutana na Rais wa DFB Bernd Neuendorf (kushoto) pamoja na aliyekuwa Waziri wa Uchumi na Tabianchi wa Ujerumani Robert Habeck.Picha: Dominik Butzmann/BMWK/picture alliance/dpa

Mabadiliko ya kisiasa katika diplomasia ya michezo

Andreas Rettig, mtendaji wa michezo anayejulikana kwa msimamo wake wa wazi na aliyewahi kufanya kazi na klabu ya FC St. Pauli, aliteuliwa mwaka 2023 kuwa Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) mpya wa Chama cha Kandanda cha Ujerumani (DFB). Anaonekana kuwa mtu sahihi wa kujenga ushirikiano mpya na kuiweka Ujerumani katika nafasi bora zaidi ndani ya kamati mbalimbali za michezo.

Hata hivyo, hata yeye amekumbana na changamoto. Juhudi za Rettig za kuanzisha mazungumzo kuhusu masuala nyeti kabla ya michuano ya Euro 2024 hazikupokelewa kwa hamasa kubwa na vyama vya soka vya kikanda.

Kwa mujibu wa Jürgen Mittag, kuna mabadiliko ya wazi katika mwelekeo wa diplomasia ya michezo.

“Kumekuwa na mabadiliko kuelekea siasa za uhalisia (realpolitik) katika diplomasia ya michezo—imekuwa chini kidogo ya misingi ya kimaadili, na zaidi ya uhalisia na utashi, kwa lengo la labda kupata mafanikio makubwa kuliko ilivyokuwa hapo awali,” aliongeza Mittag.

Huenda idadi ya watazamaji ikapungua

Maandamano ya Januari dhidi ya hatua kali za utawala wa Trump kuhusu uhamiaji haramu—ikiwemo uamuzi wa Wizara ya Sheria ya Marekani kutofungua uchunguzi wa jinai wa ukiukwaji wa haki za kiraia kuhusu kifo cha Renee Good, aliyepigwa risasi na afisa wa Idara ya Uhamiaji na Forodha (ICE) mjini Minneapolis Januari 7—yameongeza mvutano katika maeneo mengi.

Kwa kuzingatia kwamba idadi ya watazamaji wa Ujerumani ilishuka wakati wa Kombe la Dunia la Qatar, haitashangaza kuona kushuka tena msimu wa joto ujao. Hili linaweza kuchangiwa pia na nyakati ngumu za kuanza kwa mechi kwa watazamaji wa Ulaya.

“Ninaamini hatutaona viwango sawa vya watazamaji kama kwenye michuano iliyopita ya Kombe la Dunia,” alisema Jürgen Mittag.

Jürgen Mittag, Profesa katika Chuo Kikuu cha Michezo cha Ujerumani Cologne (Sporthochschule Köln).
Jürgen Mittag anaamini kuwa Ujerumani inaweza kuwa na mkakati wenye ufanisi zaidi kwa kuvishawishi na kuvipata vyama na kamati mbalimbali upande wake.Picha: BEAUTIFUL SPORTS/Wunderl/picture alliance

“Ningetarajia pia kwamba mwenendo wa matangazo na vyombo vya habari utaakisi hali ambapo watu wengi mwaka 2026 watasema: ‘Ninalifahamu Kombe la Dunia hili, lakini sitatazama kila kitu. Sijachangamka kama miaka iliyopita, na kwa njia ndogo, ninaonesha ukosoaji wangu,’” aliongeza.

Kilicho wazi ni kwamba mara tu timu ya Ujerumani itakapowasili nchini Marekani, wachezaji na benchi la ufundi watalazimika kujibu maswali kuhusu kushiriki mashindano katika mazingira ya sasa ya kisiasa na kijamii. Uzito wa majibu yao utategemea mambo mengi—lakini zaidi ya yote, utendaji wao uwanjani.

“Kigezo muhimu cha mashabiki kujitambulisha na timu ya taifa si hali ya kisiasa pekee, bali ni jinsi timu ya DFB inavyoonekana kuwa ya kuvutia, inayokaribika na yenye mafanikio,” alieleza Michael Mutz.

Aliongeza kuwa kuna uelewa unaoongezeka katika jamii kwamba dunia inaishi nyakati za misukosuko na mgawanyiko mkubwa wa maoni ya kisiasa. “Katika nyakati kama hizi, timu ya taifa ya soka inaweza kuwa nguzo muhimu ya mshikamano, hisia ya kuhusika na umoja—kuvuka mipaka ya makundi ya kijamii na kambi za kisiasa,” alisema.

Hata hivyo, Mutz alionya kuwa uwezo wa soka kuwakutanisha watu mbalimbali “hupungua pale timu ya taifa inapochukuliwa kuwa ya kisiasa kupita kiasi.”