Marekani, Canada na Mexico kuandaa kombe la dunia 2026 | Michezo | DW | 13.06.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Marekani, Canada na Mexico kuandaa kombe la dunia 2026

Marekani, Canada na Mexico zimechaguliwa kuandaa michuano ya kombe la dunia ya mwaka 2026, baada ya kuishinda Morocco kwa kura 134 kwa 65, katika kongamano la shirikisho la soka duniani, FIFA hii leo nchini Urusi. 

Michuano hiyo ambayo itaongezwa kutoka timu 32 hadi 48, kwa mara ya kwanza itafanyika kwenye nchi 3, baada ya wanachama wa FIFA kuchagua kuwa na michuano yenye faida kutoka viwanja vilivyopo kwa sasa badala ya kuandaliwa kwa mara ya pili barani Afrika.

Kati ya nchi wanachama 211 wa FIFA, 203 walikuwa na haki ya kupiga kura, huku Ghana ikikosa kushiriki kutokana kashfa ya rushwa nyumbani. Nchi nyingine nne zilizotaka kuyaandaa mashindano hayo na maeneo ya Marekani ya Samoa, Puerto Rico na visiwa vidogo vya Marekani vya Virgin Islands hawakustahili kupiga kura. 

Hii itakuwa ni mara ya tatu kwa Mexico kuwa mwenyeji wa michuano hiyo baada ya kuandaa mwaka 1970 na 1986, wakati Marekani ikiaandaa kwa mara nyingine baada ya mwaka 1994. Canada inaandaa mashindano haya kombe la dunia kwa wanaume kwa mara ya kwanza. 

Mkuu wa shirikisho la soka la Marekani Carlos Cordeiro amewashukuru wajumbe wa mkutano huo kwa kuipa Marekani nafasi ya kuandaa mashindano hayo makubwa ya soka duniani.

 Gianni Infantino Fifa (Getty Images/AFP/M. Buholzer)

Infantino pia ametangaza nia ya kugombea tena nafasi hiyo katika uchaguzi wa mwakani.

Rais wa Marekani Donald Trump, ameandika kwenye ukurasa wake wa twitter baada ya matokeo hayo akielezea furaha yake juu ya matokeo hayo ya ushindi wa kuandaa kombe la dunia kwa mwaka 2026 kwa mataifa hayo matatu.

Rais wa Urusi, Vladimir Putin alifika kwenye mkutano huo na kutoa hotuba fupi ya ukaribisho, wakati ambapo pia rais wa FIFA Gianni Infantino akitangaza rasmi azma yake ya kugombea nafasi hiyo kwa mara nyingine katika uchaguzi mwaka ujao.

Morocco kwa upande wake imeyapongeza mataifa hayo baada ya kuibuka na ushindi huo, na kupata fursa ya kuandaa michuano hiyo. Morocco ilikuwa na matumaini ya kuwa taifa la pili barani Afrika kuyaandaa mashindano hayo makubwa ya soka, baada ya Afrika Kusini iliyoyaandaa mwaka 2010.

Mcheza soka wa zamani wa Morocco, Abdelkarim El Hadrioui amesema amesikitishwa na matokeo, ingawa kwa upande mwingine amesema hakushangazwa kwa kuwa Morocco, ilipambana na mataifa makubwa, ambayo katika wiki za karibuni yaliwashawishi wapiga kura kuwachagua.

Kati ya mechi zaidi ya 80, mechi 60 zitachezwa katika miji 10 ya Marekani, huku Mexico na Canada wenyewe wakiwa wenyeji wa mechi 10 kila mmoja zitakazochezwa kwenye miji mitatu kwa kila nchi. Waandaaji wanapanga kufanyika mechi moja kila nchi kwenye hafla ya ufunguzi. 

Mwandishi: Lilian Mtono/AFPE/DPAE
Mhariri: Josephat Charo