Kerry kukutana na Abbas | Matukio ya Kisiasa | DW | 13.11.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Kerry kukutana na Abbas

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, leo anakutana na kiongozi wa Palestina Mahmoud Abbas, kutuliza mvutano wa Mashariki ya Kati, baada ya Israel kuidhinisha ujenzi wa makaazi ya walowezi, Jerusalem Mashariki.

Waziri John Kerry akiwa na Rais Mahmoud Abbas

Waziri John Kerry akiwa na Rais Mahmoud Abbas

Kerry atakutana na Abbas mjini Amman, baada ya kuwasili Jordan jana jioni, kwa lengo la kuujadili mzozo unaoendelea. Ziara ya Kerry Mashariki ya Kati, inafanyika wakati ambapo Israel inapambana kudhibiti wimbi la machafuko. Ujenzi wa makaazi mapya ulitangazwa jana saa chache baada ya Wayahudi wanaotuhumiwa kuwa na msimamo mkali, kuuchoma moto msikiti katika Ukingo wa Magharibi.

Ghasia nyingi zimekuwa zikiendelea kupamba moto kwenye mji wa Jerusalem wenye msikiti wa Al-Aqsa, eneo ambalo ni takatifu kwa Waislamu na Wayahudi. Palestina inahofu kuwa ghasia hizo zinafanyika kwenye eneo hilo takatifu la kuabudu kwa sababu Israel inataka kufanya mabadiliko ya sheria ili kuwaruhusu Wayahudi kusali kwenye eneo hilo, hali itakayochangia katika kuugawa mji huo mkongwe.

Ghasia za miezi kadhaa zimeongezeka katika siku za hivi karibuni na kusambaa kutoka Jerusalem Mashariki hadi Ukingo wa Magharibi na jamii za Waarabu kuzunguka Israel hali inayozusha wasiwasi wa kuzuka kwa vuguvugu jipya la Wapalestina.

Kerry bado hajapangiwa kukutana na Netanyahu

Hata hivyo, Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema hadi sasa hakuna mkutano wowote uliopangwa kati ya Kerry na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu

Msemaji wa Abbas, Abu Rudeina, amesema kuwa msimamo wa Palestina utaendelea kuwa wazi kwamba uchokozi na ukiukwaji unaofanywa na Israel hauwezi kuvumiliwa, hasa kutokana na mzozo katika msikiti wa Al-Aqsa na Jerusalem.

Rudeina amesema Abbas atamueleza Kerry kuwa Wapalestina hawatokatishwa tamaa na mipango ya kuzuia kuwasilisha rasimu ya azimio kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, baadae mwezi huu, la kutaka kuwekwa tarehe ya mwisho kwa Israel kuacha kuendelea kuyakalia maeneo yake.

Hata hivyo, wizara ya mambo ya nje ya Marekani, imelaani vikali kuhusu mpango wa Israel wa kutaka kujenga makaazi mapya 200 huko Ramot. Msemaji wa wizara hiyo, Jen Psaki amesema wana wasiwasi kuhusu ujenzi huo kutokana na ghasia zinazoendelea Jerusalem.

Mfalme Abudullah wa Jordan atoa wito

Kabla ya kuwasili kwa Kerry, Abbas alisema kuwa Mfalme Abdullah wa Jordan amekuwa akiendeleza juhudi za kuhakikisha vitendo vya uchokozi vinamalizwa kabisa.

'' Tangu kuanza kwa matukio haya na hata kabla, Mfalme Abdullah amekuwa akitoa wito kwa pande zote ikiwemo upande wa Israel, kukomesha na kuzuia kabisa mashambulizi dhidi ya maeneo matakatifu ya Wakristo na Waislamu,'' alisema Abbas

Mfalme Abdullah wa Jordan

Mfalme Abdullah wa Jordan

Ama kwa upande mwingine, mjumbe wa mazungumzo ya pande nne, Tony Blair, amewataka viongozi wa Israel na Palestina kujizuia na kumaliza vitendo vya chuki, uadui na uchochezi.

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, amezitaka pande hizo mbili kufanya kila linalowezekana ili kuzuia machafuko zaidi kutokana na mazingira yaliyoko sasa ambayo tayari yanatawaliwa na ghasia.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Ufaransa la AFP, kiasi Wapalestina 17 wameuawa katika Ukingo wa Magharibi, tangu kuzuka kwa ghasia za hivi karibuni miezi mitano iliyopita, zilizosababishwa na kutekwa na kuuawa kwa vijana watatu wa Israel, mauaji yaliyofanywa na wanamgambo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/ AFPE
Mhariri: Yusuf Saumu

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com