1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo kati ya Israel na Palestina wazidi kupamba moto

11 Novemba 2014

Mzozo kati ya Israel na Palestina unazidi kutokota baada ya waisrael wawili kuuliwa na vijana wa kipalestina kwa kuchomwa visu huku Palestina ikijiandaa kuadhimisha miaka kumi tangu kufariki kwa kiongozi Yasser Arafat

https://p.dw.com/p/1Dl6G
Picha: Reuters/R. Zvulun

Maombolezi ya miaka kumi tangu kifo cha kiongozi wa Palestina aliyeenziwa Yasser Arafat yamefutiliwa mbali katika ukanda wa Gaza kutokana na sababu za kiusalama lakini yanatarajiwa kufanyika katika ukingo wa magharibi.

Kiongozi huyo anayekumbukuwa kwa kutia saini makubaliano ya amani ya Oslo mwaka 1993 na Israel, aliyewahi pia lakini kuondoka katika mazungumzo yaliyokuwa yakiongozwa na Marekani mwaka 2000 alifariki dunia mwaka 2004 katika hospitali moja mjini Paris akiwa na umri wa miaka 75.

Chanzo cha kifo chake ni kitendawili mpaka sasa huku kukiwa na madai yanayodokeza huenda aliwekewa sumu aina ya Polonium jambo ambalo wapalestina wengi wanakubaliana nalo.

Hali ni tete kati ya Israel na Palestina

Maadhimisho hayo yanakuja huku hali ya kiusalama kati ya wapalestina na waisrael ikizidi kuwa tete. Waisrael wawili hapo jana waliuliwa kwa kuchomwa kisu na vijana wa kipalestina katika matukio mawili tofauti.

Vurugu kati ya vijana wa kipalestina na wanajeshi wa Israel Jerusalem
Vurugu kati ya vijana wa kipalestina na wanajeshi wa Israel JerusalemPicha: Coex/AFP/Getty Images

Katika tukio la kwanza, kijana wa kipalestina alimdunga kisu mwanajeshi mmoja wa Israel mwenye umri wa miaka ishirini tumboni katika ukingo wa magharibi ambaye alifariki baadaye akiwa hospitalini.Mshambuliaji aliyetambulika kwa jina Nureddine Abu Hashiyeh mwenye umri wa miaka 17 alitoroka lakini baadaye alikamatwa.

Saa chache baadaye,mpalestina mwingine aliwashambulia waisrael watatu waliokuwa katika kituo cha magari kusini mwa ukingo wa magharibi na kumuua mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 25 na kuwajeruhi vibaya wengine wawili kabla ya kupigwa risasi na mlinzi aliyemjeruhi vibaya.

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netayanyahu ameapa kukabiliana vilivyo na vitendo vya kigaidi vinavyolenga kuhataraisha maisha ya waisrael

Jumuiya ya kimataifa imelaani mashambulizi

Mashambulizi hayo yamelaaniwa vikali na Marekani na Umoja wa Ulaya.Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani Jen Psaki amesema ni muhimu kwa pande zote kuchukua hatua zinazofaa kuwalinda raia na kupunguza mzozo kati yao.

Mkuu wa sera za kigeni wa umoja wa Ulaya Federica Mogherini
Mkuu wa sera za kigeni wa umoja wa Ulaya Federica MogheriniPicha: AFP/Getty Images/T. Coex

Ofisi ya mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini imeonya hali huenda ikazidi kuzorota kati ya Israel na Palestina kutokana na kutokuwepo kwa nia ya kisiasa kuumaliza mzozo.

Israel imesema inaimarisha usalama katika miji yote mikubwa na katika ukingo wa magharibi kufuatia mashambuliuzi hayo .Msemaji wa polisi Micky Rosenfeld amesema vikosi vya usalama vimetumwa katika miji kadhaa ikiwemo Tel Aviv na Jerusalem kukabiliana na mashambulizi zaidi.

Tangu mwezi Julai askari wa Israel wamewakamata wapalestina 900 kwa kuvuruga amani mashariki mwa Jerusalem na thuluthi moja kati yao wamefunguliwa mashitaka.

Mwandishi:Caro Robi/afp/ap

Mhariri: Hamidou Oummilkheir