Kenya: Siku ya mwisho ya uuzwaji wa hisa za Safaricom | Matukio ya Kisiasa | DW | 23.04.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Kenya: Siku ya mwisho ya uuzwaji wa hisa za Safaricom

Wakenya wamiminika katika afisi za kuuza hisa ili wanunue hisa za Kampuni ya Safaricom; moja wapo wa zile zenye faidi chungu nzima nchini humo

Mlemavu asambaza huduma za simu katika baiskeli yake. Biashara ya simu za rununu imenawiri zaidi Afrika.

Mlemavu asambaza huduma za simu katika baiskeli yake. Biashara ya simu za rununu imenawiri zaidi Afrika.

Saa chache kabla toleo kubwa zaidi la hisa katika eneo la Africa Mashariki kufungwa, wakenya wengi wakiwemo wale waliopoteza mali katika ghasia za uchaguzi wa disemba wamekimbilia afisi za hisa ili kununua hisa za safaricom.


Serikali ya Kenya imeuza asilimia 25 ya hisa za kampuni hiyo ya simu ambayo ni moja wapo wa kampuni zenye faida kubwa zaidi nchini Kenya. Uuzaji wa hisa za kampuni hiyo unatarajiwa kuleta faida ya bilioni 50 sawa na dola milioni 812.


Toleo la hisa za kampuni ya safaricom nchini Kenya linatarajiwa kurejesha imani ya wawekezaji baada ya uchaguzi wa disemba uliozua ghasia zilizopelekea kuuwawa kwa 1,200 na wengine takriban elfu mia nne kupoteza makaazi yao.


James Waiganjo mwenye miaka 68 ni mmoja wa watu walioathirika na ghasia hizo. Baada ya kuchomewa nyumba na mtoto wake wa kiume kuuwa, Waiganjo ambaye sasa anaishi katika hema alilokita ndani ya uwanja wa michezo ameuza kipande chake cha shamba kwa bei ya chini mno ili aweze kufikisha shilingi 10,000 za kenya sawa na dola 162 za kununua hisa hizo za safaricom.


Pato la chini zaidi la soko la Safaricom linatarajiwa kuwa dola bilioni 3.3 baada ya toleo hilo la hisa bilioni kumi zinazouzwa kwa shilingi tano za kenya kila moja.


Wawekezaji wa mataifa ya nje wanatajiwa kutoa hela zaidi kwa kampuni hiyo ambayo asilimia 40 yake inamilikiwa na Vodafone kutoka Uingereza.


Wadadisi wanasema toleo la hisa za safaricom litapata asilimia 200 zaidi ya wanunuzi waliokuwa wanatarajiwa kushiriki.


Sawa na Waiganjo, wawekezaji wengi walionunua hisa hizo wanatarajia zitapanda bei ifikapo mwezi wa juni kama inavyofanyika na kampuni zingine nchini kenya.


Wadadisi wanasema kupanda kwa bei ya hisa hizo huenda kusipite kule kwa hisa za KenGen ambazo zilipanda mara nne katika siku ya kwanza ya mauzo mwezi mei mwaka wa 2006.


Kupanda mara mbili kwa bei ya hisa kunamaanisha thamani yake inapanda kutoka dola bilioni 3.3 hadi dola bilioni 6.6 jambo ambalo mdadisi wa wa biashara za hisa Aly-Khan Satchu anasema ni ngumu lifanyike. Kulingana na yeye huenda hisa hizo zikapanda kwa asilimia 50-60.


Wafanyikazi wa nyumbani, walinzi na wanafunzi ni miongoni mwa wale wanaopanga foleni pamoja na wafanyibiashara kwasababu ya kununua hisa za safaricom.


Wadadisi wanasema wanunuzi wengi hususan wale waliokopa ili waweze kununua hisa hizo wataziuza haraka.


Kwakua biashara ya simu za rununu inafanya vyema barani Africa wawekezaji wanatamani kufaidi kutoka kwa biashara hiyo. Satchu anasema mifuko 39 ya fedha barani africa iliyoanzishwa mwaka uliopita huenda iakwekezwa katika kampuni ya safaricom.


Asilimia 33 ya wakenya wanamiliki simu ya rununu. Kampuni ya safaricom inajigamba kwa kupata asilimia 80 ya watu hao kama wateja wake.


Kando na toleo la hisa kampuni hiyo imezindua huduma ya kutuma pesa inayoitwa MPesa na cadi ya masalio inayouzwa kwa shilingi ishirini pesa za Kenya.


Kampuni hiyo ilipata faida ya shilingi bilioni 17.2 mwaka uliopita. Lakini kampuni hiyo huenda ikapata ushinda zaidi kwani kando na kampuni ya celtel ambayo ndio mshindani wake wa karibu Kampuni ya France Telcom ambayo inamiliki asilimia 51 ya kampuni ya Telcom Kenya pamoja na Econet Wireless yenye makao yake Johannesburg ziko na vibali vya kuanzisha huduma zengine kwa watumizi wa rununu katika nchi hiyo ya Africa mashariki.

 • Tarehe 23.04.2008
 • Mwandishi Mwakideu, Alex
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DnTx
 • Tarehe 23.04.2008
 • Mwandishi Mwakideu, Alex
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DnTx
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com