1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Merkel kukutana na rais Medvedev wa Urusi

Charo, Josephat15 Agosti 2008

Mada kuu ya mkutano wao ni mgogoro baina ya Urusi na Georgia.

https://p.dw.com/p/ExnF
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: AP

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel anatarajiwa kukutana na rais wa Urusi Dmitry Medvedev mjini Sochi kusini mwa Urusi, katika ziara iliyopangwa kwa muda mrefu ambayo inatarajiwa kugubikwa na vita nchini Georgia. Huku Ujerumani ikiwa imesisitiza umuhimu wa kuwepo mazungumzo ya wazi na serikali ya Moscow, imeikosoa Urusi kwa kuishambulia kwa mabomu Georgia na kuwepo kwa majeshi yake katika maeneo yaliyo nje ya majimbo yaliyojitenga na Georgia.

Msemaji wa kansela Merkel, Thomas Steg, amesema kuwa uhuru wa Georgia na mipaka yake haipaswi kutiliwa shaka na kuongeza kuwa haikubaliki kuutilia shaka uhalali wa serikali ya Georgia iliyochaguliwa kwa njia ya kidemorasia.

Kansela Merkel anataka kuzungumza na rais Medvedev wa Urusi kabla kwenda mjini Tbilisi nchini Georgia siku ya Jumapili kuzungumza na rais wa Georgia Mikhael Saakaschvili. Mwenyekiti ya kamati ya bunge ya wizara ya mashauri ya kigeni ya Ujerumani, Rupert Polenz, amesema Ujerumani haina jukumu la upatanishi katika mgogoro baina ya Georgia na Urusi.

´´Kansela Merkel ameweka wazi kwamba Ujerumani peke yake haibebi jukumu la upatanisho tu, bali inabeba jukumu zima la Umoja wa Ulaya. Lakini Ujerumani ina uhusiano mzuri na Urusi na Georgia na inataka kuzileta pamoja pande hizi zikutane ana kwa ana licha ya machafuko yaliyotokea.´´

Ujerumani inausaidia Umoja wa Ulaya kuhakikisha kuna usitishwaji wa mapigano na kuwasaidia raia, lakini haitaki kujihusisha na mjadala ikiwa umoja unatakiwa kujitenga mbali na Urusi. Kuhusu swala hilo kansela Merkel na waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Frank Walter Steinmeier, wana msimamo wa pamoja.

Waziri Steinmeier anasema ´´Anayeipa mtazamo wa kitaalamu hali iliyopo hivi sasa ataona kuwa tunaihitaji Urusi katika jukumu la pamoja. Ndio maana kwa mtazamo huu sina shaka tutashindwa iwapo tutaendeleza mijadala ya kutupiana lawama.´´

Msemaji wa serikali ya Ujerumani, Thomas Steg, amesema hiyo haina maana kwamba kansela Merkel na rais wa Urusi Dimtry Medvedev wanataka kubadilishana matumaini tu. Uhuru wa Georgia na majimbo yanayozozaniwa ya Ossetia Kusini na Abkhazia hautakuwa katika ajenda ya kansela Merkel. Anachotaka Bi Merkel ni kumfafanulia wazi rais Medvedev kwamba mgogoro katika aneo la Caucusus Kusini hautatanzuliwa kutumia harakati ya kijeshi bali kuna haja ya kutafuta suluhu kwa njia ya kisiasa na kidiplomasia.

Huku kansela Merkel akitarajiwa kuwasili nchini Urusi, waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Condoleezza Rice, yumo njiani kuelekea nchini Georgia kukutana na rais wa nchi hiyo Mikhael Sakaaschvilli huku majeshi ya nchi hiyo yakiendelea na juhudi za kuyachukua maeneo yanayodhibitiwa na majeshi wa Urusi.