Kansela Angela Merkel amkaribisha rais Deby wa Chad | Matukio ya Kisiasa | DW | 12.10.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Kansela Angela Merkel amkaribisha rais Deby wa Chad

Kansela Angela Merkel amemkaribisha kwa hishma za kijeshi rais Idriss Deby wa Chad. Wanaharakati wa haki za binaadam nchini Chad wanalalamika wakidai Deby si kiongozi mstahiki.

 

Katika mkutano na waandisi wa habari mwishoni mwa mazungumzo yao mjini Berlin,kansela Angela Merkel ameahidi serikali yake itaisaidia Chad kukabiliana na kitisho cha kuzidi harakati za wafuasi wa itikadi kali katika eneo hilo na wimbi la wakimbizi wanaokimbia kitisho hicho."Tunaivulia kofia Chad katika juhudi zake za kupambana na ugaidi na  juhudi zake za kukabiliana na changamoto zinazolikabili bara la Afrika" amesema kansela Merkel.

Chad inazungukwa na maeneo yanayozongwa na mizozo mfano wa eneo linalopakana na ziwa Chad,Libya na Sudan ameeleza kansela Merkel katika mkutano na waandishi habari. Ameongeza kusema Chad imewapokea wakimbizi laki saba  kutoka nchi nyengine za eneo hilo.

Kansela Angela Merkel na mgeni wake wa kutoka Chad wakizungumza na waandishi habari mjini Berlin

Kansela Angela Merkel na mgeni wake wa kutoka Chad wakizungumza na waandishi habari mjini Berlin

Chad ni mfano wa kuigwa barani Afrika

Kansela Merkel amezungumzia pia umuhimu wa kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kukumbusha hadi wakati huu hakuna bado kampuni lolote wala taasisi yoyote ya misaada ya ujenzi mpya inayoendesha shughuli zake katika nchi hiyo. Amesema ameyahimiza makampuni ya Ujerumani hata kabla ya kuondoka kuelekea Afrika yawajibike zaidi barani Afrika. Kansela Merkel amesifu juhudi za serikali ya Chad kuinua elimu kwa wasichana na kurefusha umri wa watoto wa kike kuolewa kuanzia miaka 18 pamoja pia na kuimarisha nafasi ya mwanamke katika jamii:"Huu  ni mfano mzuri wa kuigwa barani Afrika" amesema kansela Merkel aliyeahidi.

"Ujerumani itatenga Euro milioni 8.9  za ziada kusaidia kukabiliana na matatizo ya ukosefu wa maji na chakula" .Kwa upande wake Rais Deby amekumbusha tatizo la wahamiaji akisema hawapitii pekee  Mali na Niger wanapokuwa njiani kuelekea Ulaya bali wanapitia pia Chad . "Kuna hatari ya kuenea mzozo wa wakimbizi ikiwa Niger tu ndiyo itakayosaidiwa. Muhimu ni kutolewa msaada kwa eneo lote la Sahel. Idriss Deby amezungumzia pia madhara yanayotokana na mashambulio ya kigaidi ya Boko Haram katika eneo linalopakana na ziwa Chad.

Kansela Merkel asifu juhudi za Chad za kupambana na ugaidi

Kansela Merkel asifu juhudi za Chad za kupambana na ugaidi

 Waimla hawawezi kuyapatia ufumbuzi matatizo ya Afrika

Ziara ya Idriss Deby mjini Berlin ni ya kwanza kuwahi kufanywa na rais wa Chad tangu nchi hiyo ya Afrika kati ilipojipatia uhuru mwaka 1960.Wanaharakati wa haki za binaadam wanakosoa ziara hiyo na kusema "ufumbuzi wa mizozo ya Afrika hauwezi kupatikana kupitia watala wa kimabavu."

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters

Mhariri: Iddi Ssessanga

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com