Juhudi za kidiplomasia nchini Mauritania | Matukio ya Kisiasa | DW | 11.08.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Juhudi za kidiplomasia nchini Mauritania

Viongozi wa kijeshi wanajaribu kujieleza kuepusha Mauritania isizidi kutengwa kimataifa

default

Kiongozi mpya wa kijeshi jenerali Ould Abdel Aziz       Jumuia ya kimataifa imeingia mbioni baada ya mapinduzi ya kijeshi nchini Mauritania.Jenerali Ould Abdel Aziz aliyeongoza mapinduzi dhidi ya rais aliyechaguliwa kwa njia za kidemokrasi Sidi Ould Sheikh Abdallahi amewatolea mwito wananchi washirikiane na viongozi wepya.Harakati za kidiplomasia zimeshika kasi mjini Nouakchott mji mkuu wa Mauritania.Siku sita baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyomng'owa madarakani rais aliyechaguliwa na umma,Sid Ould Cheikh Abdillahi,viongozi wa kijeshi wanajaribu kujieleza kwa lengo la kuhalalisha mapinduzi yao.


Jana mabalozi wa Ufaransa,Ujerumani,Hispania,Marekani,mjumbe wa halmashauri kuu ya umoja wa ulaya na muakilishi wa Mpango wa  Maendeleo wa Umoja wa Mataifa-UNDP kwa pamoja walikutana na jenerali Mohammed Ould Abdel Aziz.


Duru za kibalozi za Ufaransa zinasema wawakilishi hao wamepinga  uchaguzi ulioamuliwa kuitishwa na viongozi wa kijeshi.Wamelaani vikali mapinduzi ya kijeshi wakisema "hawawezi kukubali kumuona rais aliyechaguliwa kwa njia za kidemokrasi anapinduliwa kwa mtutu wa bunduki."Wawakilishi hao wamewataka viongozi wa kijeshi wamuachie huru haraka rais Sidi Ould Cheikh Abdillahi na waziri wake mkuu pamoja na kuheshimiwa katiba ya nchi hiyo.


Wawakilishi hao wa kutoka Ujerumani,Ufaransa,Hispania,Marekani,halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya na shirika la maendeleo la umoja wa mataifa wamtaka jenerali Ould Abdel Aziz aanzishe mazungumzo pamoja na jumuia ya kimataifa ili kuepushia balaa Mauritania isizidi kungwa.


Wawakilishi wa Umoja wa Afrika na Jumuia ya nchi za kiarabu nao pia walikutana mjini Nouakchott kuzungumzia mzozo wa Mauritania baada ya mazungumzo baidi pamoja na viongozi wepya wa Mauritania mwishoni mwa wiki.


Umoja wa Afrika umetishia kuisitishia uanachama Mauritania kufuatia mapinduzi ya kijeshi ya jumatano iliyopita.


Akihutubia taifa, kiongozi wa utawala wa kijeshi jenerali Mohammed Ould Abdel Aziz amewatolea mwito wananchi wawaunge mkono katika juhudi zao za kuyashughulikia ipasavyo matatizo ya nchi yao.


""Nnawatolea mwito wamauritania wote waweke kando hitilafu zao za maoni ambazo ni za muda,na washirikiane na wausaidie utawala mpya ili kupambana na matatizo ya njaa,ujinga na maradhi,pamoja na kuusaidia utawala mpya katika kuitakasa hali ya kisiasa,kuimarisha demokrasia na kupiga vita rushwa."


Kiongozi huyo wa kijeshi hajaondowa uwezekano wa kutetea mwenyewe wadhifa wa raia uchaguzi ukiitishwa.


Wadadisi wanaamini viongozi wepya wa kijeshi wa Mauritania watakua na msimamo mkali zaidi dhidi ya wanamgambo wa al Qaida nchini humo.


Harakati za wanamgambo wa itikadi kali zimeshika kasi tangu mwaka jana na kufika hadi ya kulazimisha kufutiliwa mbali mashindano mashuhuri ya mbio za magari na piki piki-Paris Dakar,baada ya watalii wanne wa kifaransa na wanajeshi kadhaa wa seerikali kuuliwa mwezi December mwaka jana.


 • Tarehe 11.08.2008
 • Mwandishi Hamidou, Oumilkher
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Euuj
 • Tarehe 11.08.2008
 • Mwandishi Hamidou, Oumilkher
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Euuj
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com