1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je, Ujerumani inapaswa kupanua ushirikiano kanda ya Sahel?

Bakari Ubena Nikolas Fischer
29 Januari 2024

Katika miaka ya hivi karibuni, hali ya kisiasa katika ukanda wa Sahel iligubikwa na matokeo ya mapinduzi ya serikali. Kwa sasa mataifa kama Mali, Niger na Burkina Faso yanaongozwa na tawala za kijeshi.

https://p.dw.com/p/4bn30
Jeshi la Ujerumani
Jeshi la Ujerumani Picha: Noah Wedel/picture alliance

Kutokana na hali hiyo ambayo haikutarajiwa na Ujerumani, kumekuwa na masuali ya kwanini na jinsi gani serikali mjini Berlin inapaswa kuendelea na miradi ya ushirikiano eneo hilo. 

Ujerumani inauchukulia ukanda wa Sahel kuwa eneo la kimkakati. Na kwa muda mrefu imekuwa mdau muhimu katika juhudi za kuleta utulivu na maendeleo katika eneo hilo kubwa barani Afrika ambalo watu wengi ni wazungumzaji wa lugha ya Kifaransa.

Mwezi Julai mwaka 2023, Ujerumani ilichukua uongozi wa urais wa kupokezana wa shirikisho linalofahamika kama Muungano wa Sahel, ambacho ni chombo muhimu kwa maendeleo ya ukanda huo.

Soma pia:  Ufaransa yawaondoa wanajeshi wake wa mwisho Niger

Muungano huo ulianzishwa mwaka wa 2017 ili kuzisaidia Burkina Faso, Chad, Mali, Mauritania na Niger - zinazojulikana kwa pamoja kama Kundi la G5 la Sahel, katika mapambano yao dhidi ya umaskini na vitendo vya ugaidi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock aliashiria mwaka jana umuhimu wa eneo hilo kwa nchi yake, akisema kuwa chochote kinachotokea Sahel kina umuhimu mkubwa kwa watu wote wa Ujerumani.

Ushawishi unaoongezeka wa Urusi huko Sahel

Jeshi la Ufaransa likifanya doria katika eneo la Barkhane
Jeshi la Ufaransa likifanya doria katika eneo la BarkhanePicha: Philippe De Poulpiquet/MAXPPP/dpa/picture alliance

Hata hivyo Ujerumani inatakiwa kukabiliana na ushawishi unaokua wa Urusi katika ukanda wa Sahel. Kwa mfano, utawala wa kijeshi wa Mali, ambao tangu uingie madarakani kufuatia mapinduzi ya mwezi Mei mwaka 2021, umekuwa ukiigeukia Moscow kwa ajili ya misaada na ushirikiano badala ya kutegemea washirika wake wa jadi wa barani Ulaya kama vile Ujerumani.

Mamluki wa Urusi wa Wagner wamekuwa pia wakishirikiana na jeshi la Mali katika mapambano yao dhidi ya ugaidi. Hali hii ilipelekea kuondoka nchini humo kwa vikosi vya Ufaransa, Ujerumani na hata vile vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa MINUSMA.

Soma pia: Hali ya usalama nchini Mali imerejea kuwa ya wasiwasi

Baada ya mambo kuparaganyika nchini Mali, Ujerumani ilielekeza nguvu zake na kuanza kushirikiana na Niger. Mwezi Mei mwaka 2023, Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius aliitaja Niger kama "mshirika wa kutegemewa", lakini kauli hiyo aliijutia, kwani miezi miwili tu baadaye, jeshi lilifanya pia mapinduzi na kuchukua madaraka.

Katika kukabiliana na matukio ambayo hayakutarajiwa, Ujerumani pamoja na mataifa mengine yenye nguvu ya Magharibi, yalisitisha misaada kwa Niger. Mwezi Disemba, utawala wa Niger ulitangaza pia kusitishwa kwa misheni za kijeshi na kiraia za Umoja wa Ulaya. Siku hiyo hiyo, kiongozi wa kijeshi Abdourahamane Tiani aliwakaribisha washirika wa kijeshi wa Urusi ili kupanga mustakabali wa ushirikiano wao.

Ujerumani yabadili mwelekeo kuhusu ukanda wa Sahel

Ukanda wa Sahel
Ukanda wa Sahel

Mtafiti katika Taasisi ya Ujerumani ya Masuala ya Kimataifa na Maeneo (GIGA) iliypo huko Hamburg, Malte Lierl ameiambia DW kwamba mikakati ya kiusalama ya mataifa ya Magharibi huko Sahel haikufanikiwa na kwamba kwa sasa kinachofanyika si kujiondoa moja kwa moja bali ni kuandaa mwelekeo mpya wa ushirikiano.

Soma pia:  Yafahamu mataifa mengine ya magharibi yenye vikosi vya kijeshi Afrika Magharibi

Kwa upande wake Julian Bergmann, mtaalamu wa mahusiano ya Umoja wa Ulaya na Afrika katika Taasisi ya Maendeleo endelevu ya Ujerumani (IDOS) iliyopo hapa mjini Bonn, anasema hatua mojawapo ya kuanzisha mwelekeo huo mpya inaweza kuwa mabadiliko ya kuacha kushirikiana na serikali za mataifa hayo, na badala yake kupanga mikakati ya kuwasaidia moja kwa moja watu wa Sahel. 

Bergmann ameiambia DW kuwa tangu miaka ya 1960, aina hii ya ushirikiano imekuwa ikitumiwa mno na Ujerumani katika miradi ya maendeleo katika ukanda wa Sahel na kwingineko, hasa kwa kushirikiana na watendaji wa asasi za kiraia katika mataifa husika.